IQNA

Mbinu ya Elimu ya Manabii; Musa /28

Indhar na Tabshir katika Kisa cha Nabii Musa katika Qur'ani Tukufu

20:07 - September 11, 2023
Habari ID: 3477582
TEHRAN (IQNA) – Moja ya mbinu alizotumia Nabii Musa (AS) katika kuwaelimisha watu wake ni Indhar na Tabshir.

Indhar maana yake ni kuonya kuhusu matokeo ya matendo na dhambi mbaya huku Tabshir maana yake ni kutoa habari au bishara njema ya rehema na baraka za Mwenyezi Mungu.

Hizi mbili ni nukta muhimu za motisha katika  elimu. Mwanaadamu ahimizwe kwa kufanya amali njema na aadhibiwe kwa kufanya maovu ili awe na ari na kujiandaa kwenda kwenye njia iliyo sawa na kuepuka njia mbaya.

Kutia moyo pekee hakutoshi katika njia ya ukuaji wa maadili ya mtu au jamii. Kuonya tu mtu kuhusu matokeo ya matendo yake haitoshi pia.

Kuzitumia kwa usawaziko zote mbili kutawasaidia watu kuwa na matumaini juu ya kupata thawabu kwa matendo yao mema na wakati huo huo wawe waangalifu wasifanye mabaya kwa sababu wameonywa kuhusu matokeo ya makosa.

Katika historia, wajumbe wa Mungu wametumia Indhar na Tabshir kwa ajili ya kuwaelimisha watu na kuwaongoza kwenye njia iliyo sawa. Katika aya za Qur'ani Tukufu pia, kuna mifano mingi ya Indhar na Tabshir.

Kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu, Musa (AS) alitoa habari njema kwa watu wake. Bani Israi’l ambao walikuwa wamechanganyikiwa kwa sababu ya shinikizo la Firauni, walimlalamikia Musa (AS), wakiuliza ni nini kilitokea kwa ahadi yake kwamba wataokolewa kutoka kwa Firauni na watu wake. Bani Isra’il walitarajia kwamba kila kitu kingefanyika kwa usiku mmoja na wataokolewa.

Musa (AS) akawapa moyo kwa kusema: Musa akawaambia watu wake: Ombeni msaada kwa Mwenyezi Mungu, na subirini. Hakika ardhi ni ya Mwenyezi Mungu. Naye humrithisha amtakaye katika waja wake. Na mwisho ni wa wachamngu. Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia, na baada ya wewe kutujia! Musa akasema: Huenda Mola wenu Mlezi akamhiliki adui wenu, na akakufanyeni nyinyi ndio wa kufuatia kushika nchi, ili atazame mtavyo kuja tenda nyinyi.” (Aya  ya 128-129, Surat Al-A’araf)

Katika hali nyingine, Musa (AS) aliwaonya watu wake kuhusu matokeo ya matendo yao maovu:

“Musa akamwambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo, asije akakufutilieni mbali kwa adhabu. Na mwenye kuzua lazima ashindwe! ( Aya ya 61 ya Surah Taha).

Anachomaanisha kwa kusema kumzulia uwongo Mwenyezi Mungu maana yake ni kuwa mshirika wa Mungu. Musa (AS) anawaonya washirikina.

captcha