IQNA

Jinai za Israel

UN: Gaza inahitaji miaka 14 kutegua mabomu yaliyondondoshwa na Israel

11:02 - April 27, 2024
Habari ID: 3478740
IQNA-Kwa muda wa karibu miezi saba sasa, utawala katili wa Israel umekuwa ukidondosha mabomu kila siku katika Ukanda wa Gaza na sasa Umoja wa Mataifa unasema zoezi la kutegua mabomu ambayo hayajalipuko eneo hilo linaweza kuchukua muda miaka 14.

Afisa Mkuu wa ofisi ya Umoja Huduma ya Uteguzi wa Mabomu UNMAS Pehr Lodhammar ameyabainisha hayo na kuongeza kuwa vita huko Gaza vimeacha takriban tani milioni 37 za mabomu. Amesema haiwezekani kubainisha kiasi halisi cha mabomu ambayo bado hayajalipuka katika eneo hilo ambalo hapo awali lilikuwa na idadi kubwa ya watu na wakati zaidi ya milioni mbili lakini sasa limeharibiwa na kubaki vifusi baada ya takriban miezi saba ya mashambulizi makali kutoka Israel.

Mtaalamu huyo mkongwe wa Umoja wa Mataifa wa kutegua mabomu amesema kila mita ya mraba huko Gaza iliyoathiriwa mashambulizi ya Israel ina takriban kilo 200 za vifusi. Akizungumza na waandishi habari mjini Geneva Uswisi Ijumaa amesema: "Ninachoweza kusema ni kwamba angalau asilimia 10 ya mabomu yanayodondoshwa hayalipuki ... tunazungumza juu ya miaka 14 ya kutegeua mabomu."

Wakati huo huo mashirika ya misaada ya kibinadamu yamerejea onyo lao kwamba njaa inakaribia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, katika ombi jipya la dharura la misaada zaidi kuruhusiwa kuingia katika eneo hilo.

Israel iliahidi wiki tatu zilizopita kuboresha upatikanaji wa misaada kupitia Kivuko cha Erez kaskazini mwa Gaza na bandari ya mizigo ya Ashdod, kuelekea kaskazini zaidi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limesema kumekuwa na ongezeko dogo la misaada lakini si kwa kiasi cha kutosha – au chakuleta  utofauti.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Carl Skau ameeleza kuwa “Bado tunaelekea kwenye baa la njaa, hatujaona mabadiliko ya kimtazamo ambayo yanahitajika kuepusha njaa, tunahitaji kiasi kukubwa zaidi, uingizaji wa misaada unaotabirika zaidi na juhudi endelevu ili kupata usaidizi wa aina mbalimbali kaskazini mwa Gaza.”

Utawala dhalimu wa Israel ulianza vita vya mauaji wa kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza Oktoba 7, 2023.

Hadi sasa zaidi ya Wapalestina 34,200 wameuawa shahidi na wengine 77,200 kujeruhiwa, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.

Kulingana na Umoja wa Mataifa zaidi ya miezi sita baada ya vita vya Israel, maeneo makubwa ya Gaza sasa ni magofu, huku 85% ya wakazi wa eneo hilo wakiwa wakimbizi wa ndani katika eneo hilo ambalo limezingirwa na kusababisha uhaba mkubwa wa  chakula, maji safi na dawa,

Afrika Kusini ilifungua kesi dhidi ya utawala wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ikiutuhumu utawala huo kuwa unatekeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Uamuzi wa muda wa mwezi Januari uliiamuru Israel  kusitisha vitendo vya mauaji ya halaiki na kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba msaada wa kibinadamu unatolewa kwa raia huko Gaza. Israel ilipuuza uamuzi huo.

3488092

captcha