IQNA

Jinai za Israel

Rais wa Iran amtumia rambirambi kiongozi wa Hamas baada ya Israel kuua shahidi watoto na wajukuu wake

11:32 - April 12, 2024
Habari ID: 3478673
IQNA-Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani mauaji yaliyofanywa na jeshi la utawala katili wa Israel dhidi ya wanafamilia wa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika Ukanda wa Gaza.

Katika ujumbe wake aliomtumia Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Sayyid Ebrahim Raisi amelaani shambulizi la kiendawazimu na kikatili lililofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kambi ya wakimbizi ya al Shati huko Gaza na kuuliwa shahidi raia kadhaa wa Kipalestina wakiwemo watoto watatu na wajukuu watatu wa Ismail Haniya.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, mauaji hayo yamedhihirisha wazi zaidi dhati ya ukatili na kuua watoto ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaofanya mauaji ya kimbari huko Palestina na kuonesha kuwa, ili kujinusuru kutoka kwenye kinamasi cha kuporomoka na kuficha unyonge na kushindwa kukabiliana na mapambano ya ukombozi ya Wapalestina, Israel inakanyaga kanuni zote za kimaadili na kibinadamu.

Rais Ebrahim Raisi amesema, inasikitisha kwamba, nchi zinazodai kutetea haki za binadamu hazikutosheka kuwa watazamaji tu mbele ya jinai kama hii ambayo haina kifani katika historia, bali kwa kunyamaza kimya na uungaji mkono wao kwa Israel, zimetayarisha mazingira ya kukaririwa jinai hizo, na kwa hakika ni washirika wa Israel katika uhalifu huo.

Itakumbukwa kuwa, jeshi katili la Israel jana lililenga gari iliyokuwa imewabeba watoto na wajukuu wa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, Ismail Haniyeh na kuuwa shahidi watu saba wa familia yake.

Watoto watatu wa kiume wa Haniya waliouawa shahidi katika shambulio hilo wametambulika kuwa ni Hazem, Amir na Muhammad Ismail Haniyeh.

Watoto na wajukuu hao wa kiongozi wa Hamas walikuwa wameelekea kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Al-Shati kwenda kuwasalimia na kuwatakia Idi njema wakazi wa kambi hiyo kwa mnasaba wa Sikuu ya Idul-Fitri iliyosherehekewa Jumatano.

3487896

captcha