IQNA

Utamaduni

Jumba la Makumbusho ya Qur'ani ‘Bait Al-Hamd’ yazinduliwa nchini Kuwait

18:13 - March 04, 2024
Habari ID: 3478451
IQNA – Jumba la Makumbusho ya Qur'ani la "Bait Al-Hamd" limezinduliwa nchini Kuwait kwa lengo la kukuza Qur'ani Tukufu na maarifa ya Kiislamu.

Jumba hilo limefunguliwa nchini Kuwait mwezi Februari, sanjari na sherehe za kitaifa za nchi hiyo. Hafla ya ufunguzi ilihudhuriwa na maafisa kadhaa, vyombo vya habari vya Kuwait viliripoti wikendi hii.

Jumba la Makumbusho ya Qur'ani la "Bait Al-Hamd" limeanzishwa kwa msaada wa Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya nchi hiyo na kwa ushirikiano na Jumuiya ya Qur'ani na Hadithi za Mitume SAW.

Akielezea "Bait Al-Hamd" kama msingi wa maendeleo ya kitamaduni ya Kuwait, Fahad Al-Dihani, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Qur'ani na Hadithi za Mtume SAW, alisisitiza msukumo wake wa usanifu majengo wa jumba hilo uliotokana na nyumba za kihistoria za Kuwait.

Ameashiria madhumuni ya jumba hilo la makumbusho la kuonyesha historia ya Qur'ani Tukufu, kwa kuzingatia juhudi za kielimu na kisanii katika kuhifadhi, kunakili, na michango ya wanazuoni wa Kuwait katika kuieneza.

Pia amesema jumba hilo la makumbusho linatoa programu za elimu kwa ajili ya kujifunza na kusoma Qur'ani kwa makundi ya rika tofauti, pamoja na matukio ya kitamaduni, mihadhara na semina za kukuza maarifa na turathi za Kiislamu.

Aidha, jumba hilo la makumbusho linaunga mkono utafiti wa kitaaluma katika masomo ya Qur'ani na uhifadhi wa mambo ya kale, hulinda miswada na maandishi ya zamani, na kuchapisha nyenzo zinazohusiana na Qur'ani na turathi za Kiislamu.

Jumba la makumbusho lina kumbi tano kuu, zikiwemo za kielimu, za sauti-kuona, mapokezi, utawala, na ukumbi maalum kwa makusanyo ya thamani.

Habari zinazohusiana
captcha