IQNA

Kiongozi Muadhamu Aonana na Amir wa Kuwait

17:33 - June 03, 2014
Habari ID: 1414303
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jumatatu asubuhi mjini Tehran alionana na Sheikh Sabah al Ahmad al Jabir as Sabah, Amir wa Kuwait na ujumbe alioandamana nao na kusema kuwa, eneo la Ghuba ya Uajemi na usalama wake ni suala muhimu mno.

Katika kikao hicho, amesisitiza kuwa: Amani ya eneo hili itaweza kudumishwa kama utakuwepo uhusiano mzuri na salama kati ya nchi zote za eneo hili.
Ameongeza kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku zote ikawa inapigania kuwa na uhusiano salama na majirani zake wote wa eneo la Ghuba ya Uajemi na hivi sasa pia inaendeleza vilivyo siasa zake hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kukurubiana nchi za eneo hili na kuwepo uhusiano salama baina yao ni faida kwa eneo hili zima, lakini kama msingi huo hautafuatwa, basi hitilafu baina ya nchi hizo na kila nchi ya eneo hili kujitenga na mwenzake na kufanya mambo kivyake, hakuwezi kuwa na matokeo mengine ila kuwafurahisha tu maadui wa pamoja wa nchi hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja ujuba unaoongezeka kila leo wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni matunda ya kukosekana uhusiano salama baina ya nchi za eneo hili na kusisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku zote imekuwa ikiamiliana kwa kifua kipana na nchi zote za eneo hili la Ghuba ya Uajemi.
Vile vile amekutaja kustawishwa uhusiano wa Kuwait na Iraq kuwa ni kwa manufaa ya eneo hili zima na kuongeza kwa kusema: Kuhusiana na kadhia ya Syria pia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuunga mkono uamuzi wowote utakaochukuliwa na wananchi wenyewe wa Syria.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia hatari za makundi ya kitakfiri katika eneo hili na kusisitiza kwamba: Inasikitisha kuona kuwa baadhi ya nchi za eneo hili hazioni kwamba hatari ya makundi hayo ya kitakfiri itazielekea pia nchi hizo katika siku za usoni. Amesema kwa kuisisitiza kuwa, inahuzunisha kuona kwamba nchi hizo zinaendelea kuyaunga mkono makundi hayo na kutojali hatari zake.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, baadhi ya nchi za eneo hili hivi sasa zinayasaidia makundi hayo ya kitakfiri na zinaunga mkono jinai zinazofanywa na makundi hayo huko Syria na katika baadhi ya nchi nyingine, lakini zinapaswa kuelewa kuwa, katika mustakbali usio mbali, makundi hayo ya kitakfiri yatakuwa balaa kwa roho za nchi hizo hizo ambazo zinayaunga mkono hivi sasa na wakati huo tena zitalazimika kutoa gharama kubwa kupambana nayo.
Aidha ameashiria kuwepo Iran pega kwa bega na Kuwait katika matukio nyeti ya miaka ya huko nyuma na ameishukuru nchi hiyo kutokana na misimamo yake kuhusiana na matukio ya eneo hili akiongeza kuwa: Inabidi masuala ya eneo hili yatatuliwe kwa mbinu na mitazamo kama hiyo ya Kuwait.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria uhusiano wa kiuchumi na kibiashara uliopo baina ya Iran na Kuwait na kusema kuwa: Kuna uwanda mpana wa kuweza kustisha zaidi na zaidi uhusiano wa kiuchumi wa nchi hizi mbili na inabidi kufunguliwe ukurasa mpya katika uhusiano wa kiuchumi wa Iran na Kuwait.
Katika mazungumzo hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Hujjatul Islam Walmuslimin Sheikh Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Amir wa Kuwait, Bw. Sheikh Sabah al Ahmad al Jabir as Sabah ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imam Husain AS na kusema kuwa, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei ni "murshid" na muongozaji wa masuala ya eneo hili zima akisema kuwa: Kuwait iko tayari kwa ajili ya kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwamba hata katika mazungumzo yake aliyoyafanya na viongozi wa Iran katika safari yake hii ya mjini Tehran kumefikiwa makubaliano mbali mbali kuhusu kuongezwa upeo wa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya nchi hizi mbili.
Amir wa Kuwait aidha ameyaunga mkono matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na ulazima wa kuwepo umoja, mshikamano na misimamo ya pamoja baina ya nchi za eneo la Ghuba ya Uajmeni na pia kuhusiana na udharura wa kupambana na misimamo ya kufurutu ada na kuutaja uhusiano wa Kuwait na Iraq kuwa ni mzuri sana akisema kuwa, viongozi wa Iraq ni marafiki wa Kuwait na kwamba ana matumaini masuala na matatizo ya Syria yatatatuliwa kwa njia za amani kwa mujibu wa maamuzi ya wananchi wenyewe wa nchi hiyo.

1413585

Kishikizo: iran kuwait khamenei sabah
captcha