IQNA

Uchaguzi wa Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu asisitiza kujitokeza kwa wingi wananchi wa Iran katika uchaguzi

18:14 - February 28, 2024
Habari ID: 3478428
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema: Maadui wa Iran ya Kiislamu wana hofu ya kushiriki kwa wingi kwa wananchi katika uchaguzi hapa nchini.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo ​​Jumatano katika kikao na maelfu ya wananchi wanaojiandaa kupiga kura kwa mara ya kwanza na kundi la familia za mashahidi. Ameutaja ushiriki mkubwa na wenye hamasa wa taifa katika uchaguzi ujao wa Bunge, kuwa ni dhihirisho la nguvu ya kitaifa, dhamana ya usalama wa taifa na jambo linalowakatisha tamaa maadui wa Iran na kusema: Marekani, sera za nchi nyingi za Ulaya, Wazayuni waovu, mabepari na makampuni makubwa yanayofuatilia kwa makini masuala ya Iran kutokana na sababu mbalimbali, wanaogopa zaidi ushiriki mkubwa wa watu katika chaguzi na nguvu ya watu wa Iran kuliko kitu kingine chochote.

Ayatullah Khamenei ameyataja mafanikio muhimu ya uchaguzi madhubuti na wenye hamasa kubwa kuwa ni kuchaguliwa watu imara na kuundwa Bunge lenye nguvu; na matokeo yake ni kutatua matatizo yaliyopo na kupatikana maendeleo ya nchi. Ameongeza kuwa: Bunge lenye nguvu litaweza kufanya mambo makubwa na kupiga hatua za maendeleo.

Uchaguzi wa duru ya 12 ya Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu ya Iran yaani Bunge na wa duru ya 6 wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Iran utafanyika Ijumaa, Machi 1 kote nchini. 

Takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran zinaonyesha kuwa karibu wagombea 15,000 wameidhinishwa kushiriki katika uchaguzi wa bunge mwaka huu, ikiwa ni rekodi tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu miaka 45 iliyopita. Mamia ya wagombea pia wanawania viti 88 katika Baraza la Wataalamu. Wajumbe wa baraza hilo huhudumu kwa miaka minane.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la Gaza kuwa suala la msingi la Ulimwengu wa Kiislamu na kusema: Suala la Gaza limeutambulisha Uislamu duniani na kudhihirisha kuwa, Uislamu ndio unaowapa watu wa Gaza nguvu na kuwawezesha kusimama imara, kupambana na kutosalimu amri mbele ya mashambulizi ya mabomu na majanga yote yanayofanywa na Wazayuni.

Ayatullah Ali Khamenei amesema: Suala la Gaza limeonyesha ukweli wa utamaduni na ustaarabu wa Kimagharibi kwa walimwengu na kudhihirisha wazi kwamba, wanasiasa waliozaliwa katika utamaduni huo hawako tayari hata kukiri kitendo cha Wazayuni cha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina; na licha ya baadhi ya madai yao, kivitendo, wanazuia juhudi za kusiiisha mauaji hayo ya kimbari kwa kutumia kura ya veto kupinga maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kitendo cha kujichoma moto afisa wa Jeshi la Anga la Marekani kwa ajili ya kupinga jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza ni ishara ya kukithiri kashfa na fedheha za siasa zilizodhidi ya binadamu za Marekani na utamaduni mbovu na dhalimu wa nchi za Magharibi. Amongeza kuwa, hata mtu huyu aliyelelewa katika utamaduni wa Kimagharibi, ameelewa na kuona vyema kina cha fedheha ya utamaduni huo.

3487370

Habari zinazohusiana
captcha