IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Ayatullah Khamenei: Katika Uislamu, njia ya shughuli zozote za kijamii ziko wazi kwa wanawake

18:59 - December 27, 2023
Habari ID: 3478103
IQNA- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kislamu mapema leo amehutubia maelfu ya wanawake na wasichana ambako amebainisha mtazamo wa kimantiki wa Uislamu kuhusu nafasi ya wanawake katika familia na shughuli kijamii, siasa na uongozi katika ngazi mbalimbali.

Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, katika Uislamu, njia ya shughuli zozote za kijamii ziko wazi kwa wanawake, sawa na ilivyo kwa wanaume, kwa sharti kwamba mambo mawili muhimu yazingatiwe, yaani suala la familia na kuchunga hatari ya mvuto wa kijinsia.

Akihutubia kikao hicho kilichofanyika kabla ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa binti kipenzi wa Mtume Muhammad (SAW), Bibi Fatima  Zahra (SA), Ayatullah Ali Khamenei ameutaja utukufu wa bibi bora zaidi ya wote duniani, (Bibi Fatima al Zahra), kuwa ni jambo lisiloweza kufikirika na kuongeza kuwa: Kwa mujibu wa Hadithi sahihi, Mwenyezi Mungu hukasirika kwa hasira ya Bibi Fatima (SA) na anaridhika kwa ridhaa yake, na hakuna fadhila na ubora mkubwa zaidi na ulio juu na huu unaoweza kufikirika kwa mwanadamu; kwa hiyo, yeyote anayetaka kupata radhi za Mwenyezi Mungu anapaswa kufuata mawaidha, masomo na mwelekeo wa mtukufu huyo katika masuala ya familia, katika nafasi ya binti, mama, mke, na katika nyanja ya jamii na siasa.  

Ayatullah Khamenei ameutaja utambulisho wa mwanamke, thamani zake, haki zake, wajibu, uhuru na mipaka yake kuwa ni suala lenye muhimu mkubwa na akasema kwamba, kuna mitazamo miwili jumla ionayokabiliana ya Kimagharibi na ya Kiislamu duniani kuhusu suala hili muhimu sana.

Akiashiria sera ya mfumo wa ustaarabu na utamaduni wa nchi za Magharibi ya kuhepa mijadala inayohusu masuala ya wanawake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kwa kuwa hawana mantiki yoyote kuhusu wanawake, Wamagharibi, mkabala wa kila swali na maudhui, wanajaribu kubainisha hoja zao kwa mabishano na uhuni, kununua shakshia mashuhuri wa kisiasa na wasio wa kisiasa na kwa kutumia nyenzo za sanaa na fasihi, mtandao, na kudhibiti vituo vya kimataifa vinavyohusiana na wanawake.

Ayatullah Khamenei ameashiria takwimu rasmi za kutisha za ufuska na ufisadi wa kimaadili katika nchi za Magharibi na kusema: Kwa nini kila suala linaloharibu familia linakuzwa na kufanywa mashuhuri zaidi katika nchi za Magharibi, na kwa upande mwingine hakuna lawama wala hatua kali zinazochukuliwa dhidi ya watu wanaowanyanyasa wanawake wenye vazi za hijabu?

Ameutaja mwenendo wa Uislamu katika suala la wanawake kuwa wa busara na wa kimantiki, kinyume kabisa na mtazamo wa Magharibi, na kuongeza kuwa: Suala la wanawake ni moja ya nukta zenye nguvu za Uislamu, na isifikiriwe kuwa tunapaswa kukalishwa kiti moto katika suala la wanawake.

Ayatullah Ali Khamenei ameyataja maendeleo na ustawi wa wanawake katika nyanja mbalimbali za sayansi, fasihi, michezo na sanaa katika kipindi cha Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni mara kumi zaidi ya kabla ya ushindi wa Mapinduzi na kusema: "Licha ya kuwa bado hatujaweza kuifanya nchi kuwa ya Kiislamu kikamilifu, lakini tumepata mafanikio haya; na iwapo Uislamu utatekelezwa kikamilifu, mafanikio haya yatakuwa mara dufu."

Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia uchaguzi muhimu wa tarehe Mosi Machi mwakani, na kusema ushiriki wa wanawake katika uwanja huo ni dharura sana katika jamii na familia.

3486589

 

Habari zinazohusiana
captcha