IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Usalama ni kati ya nguzo muhimu za ustawi na maendeleo ya Iran ya Kiislamu

19:09 - October 04, 2016
Habari ID: 3470599
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesema usalama ni moja ya nguzo kuu za ustawi na maendeleo ya Iran ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo katika mkutano na makamanda na wakuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amesema, usalama maana yake ni "utulivu wa akili wa mtu binafsi na utulivu wa watu wote kijamii" na akaongeza kuwa, unapokosekana usalama, hata kama watu katika jamii watakuwa na nia na uwezo wa kufanya mambo, uwezekano wa kutekeleza harakati mbalimbali za kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na za utoaji huduma hutoweka.

Ayatullah Khamenei amesisitizia nafasi muhimu ya Jeshi la Polisi katika kuleta amani na usalama na akabainisha kuwa kiwango cha uwezo na utayari wa Jeshi la Polisi pamoja na azma na imani ya wafanyakazi wake vinapaswa kuzidishwa siku hadi siku.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, amani huwa sababu ya kuongezeka imani za waumini na akafafanua kuwa: "Miongoni mwa nguzo muhimu zaidi za usalama wa Iran ni Jeshi la Polisi; tab'an nguzo hii adhimu ya amani imeundwa na rasilimaliwatu ambao wengi wao ni wafanisi, wenye kuheshimika na wenye kujituma; na kwa hivyo azma, imani, motisha na moyo wa kazi wa askari hao vinapasa viendelee kuimarishwa muda wote."

Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran ameashiria pia mabadiliko ya kasi yanayojiri katika sekta mbalimbali yakiwemo maendeleo ya sayansi na teknolojia na kusisitizia ulazima wa "kuongeza kiwango cha utayari na uwezo unaokwenda na wakati", "kuelewa na kutekeleza majukumu kikamilifu" na "kuwabainishia kwa makini wananchi katika vyombo vya habari kazi na huduma zinazotolewa" kwa ajili ya kudhamini na kustawisha amani na usalama nchini.

3535467

captcha