Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa:"Majenerali walioongoka na waliojitolea wa Kiislamu, Meja Jenerali Mohammed Reza Zahedi na mpiganaji mwenzake Mohammed Hadi Haj Rahimi wameuawa shahidi katika jinai ya utawala ghasibu na unaochukiwa wa Kizayuni."
Ayatullah Khamenei amesema: "Amani na rehema za Mwenyezi Mungu na mawalii wake ziwe juu yao na mashahidi wengine wa tukio hili, na laana ziwashukie viongozi wa utawala dhalimu na vamizi wa Israel. Mashahidi walipokea ishara ya kukubaliwa mapambano yao ya muda mrefu kutoka kwa Mwenyezi Mwenye Rehema, na sasa wako pamoja na mawalii na watu wema kwa baraka na neema za Mwenyezi Mungu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Wapiganaji shujaa wa Kiislamu wataadhibu utawala khabithi wa Israel unaotekeleza mauaji ya kimbari na wataufanya ujutie jinai hiyo na jinai zingine kama hiyo."
Jana Jumatatu jioni, ndege za kivita za utawala haramu wa Israel zililenga ubalozi mdogo wa Iran katika Mtaa wa Al-Mezeh huko Damascus.
Jana jioni (Aprili Mosi 2024), utawala wa Kizayuni ulishambulia ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus na kuua shahidi washauri wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu akiwemo Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) nchini Syria na Lebanon, Brigedia Jenerali Mohammad Reza Zahedi na naibu wake, Mohammad Hadi Haj Rahimi na watu wengine watano.
Tamko la Rais Raisi
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia jinai na ugaidi uliofanywa jana Jumatatu na utawala wa Kizayuni wa kushambulia ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus Syria na kusema kuwa, Wazayuni wanapaswa kutambua kwamba ugaidi wao wa kinyama kama huo hauwezi kuwafanikishia malengo yao maovu.
Rais Ebrahim Raisi akilaani ugaidi na jinai hiyo ya utawala wa Kizayuni ambayo imekanyaga sheria zote za kimataifa za wajibu wa kuheshimiwa maeneo ya kidiplomasia na kusisitiiza kuwa, maafisa hao wa Iran wamefanikiwa kupata daraja ya juu ya kuuawa shahidi katika njia ya Quds na kulinda Haram za Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, utawala ghasibu wa Kizayuni umefanya shambulio hilo la kipunguani na kiwendawazimu baada ya kuchezea vipigo mtawalia katika medani za mapambano baina yake na kambi ya muqawama.
Kwa mara nyingine amesisitiza kwa kusema: Wazayuni waelewe kwamba vitendo vyao hivyo vya kinyama kamwe havitawasaidia kufanikisha malengo yao haramu na maovu, bali siku baada ya siku tutaendelea kushuhudia jinsi kambi ya muqawama inavyozidi kuwa imara na hasira za mataifa ya dunia zinavyozidi kuongezeka dhidi ya utawala katili na pandikizi wa Israel.
/3487778