IQNA

Kiongozi Muadhamu ahudhuria maombolezo ya Bibi Fatima Zahra (SA)

14:08 - December 17, 2023
Habari ID: 3478047
IQNA- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameshiriki kikao cha maombolezo ya kukumbuka siku aliyokufa shahidi Bibi Fatimatu-Zahra (SA), binti kipenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW na mke wa Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib (AS), Imamu na Kiongozi wa Waislamu baada ya Mtume (SAW).

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amehudhuria marasimu hayo ya kimaanawi hapa mjini Tehran jana usiku, akiwa pamoja na viongozi wengine kadhaa, akiwemo Rais Ebrahim Raisi wa Iran na Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge), Mohammad Baqer Qalibaf.

Umati mkubwa wa wananchi Waislamu wa Iran jana usiku ulihudhuria vikao na marasimu ya maombolezo ya kukumbuka siku aliyokufa shahidi Bibi Fatima (SA) katika kona mbalimbali za nchi, na hususan katika Haram ya Imam Ridha (AS), Imam wa nane wa Waislamu wa Kishia iliyoko katika mji wa Mashhad, kusini mashariki mwa Iran na katika Haram ya mtukufu Bibi Maasumah (SA) iliyoko mjini Qum kusini mwa Tehran kuomboleza kufa shahidi kidhulma kwa binti kipenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW.

Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita alikufa shahidi Bibi Fatima al-Batul, binti mtukufu wa Mtume wetu Muhammad (SAW) na mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (AS). Alizaliwa miaka mitano baada ya kubaathiwa Nabii Muhammad (SAW) na mtukufu huyo akampa jina la Fatima.

Chini ya malezi ya baba yake, Bibi Fatima (SA) alifikia daraja la juu katika maarifa, elimu na uchamungu. Katika maisha yake, Bibi huyo mtukufu alifahamika sana kwa ukarimu, kujitolea, subira, uchamungu na kuwasaidia masikini na watu wasiojiweza.

Mtukufu huyo alijulikana kwa lakabu na majina kadhaa ya sifa teule kama Zahra, Siddiqah, Taahirah, Mubaarakah, Batul, Raadhiyah na Mardhiyyah.

 

4188337

Habari zinazohusiana
captcha