IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi

Imam Ruhullah Khomeini (RA) ni miongoni mwa viongozi vinara wa historia

13:31 - June 04, 2023
Habari ID: 3477093
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, amemtaja hayati Imam Ruhullah Khomeini (RA) kuwa ni miongoni mwa viongozi vinara wa historia.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo mapema leo ​​(Jumapili) akihutubia taifa wakati wa kumbukumbu ya mwaka wa 34 wa kifo cha Imam Khomeini (RA) katika Kaburi lake kwenye viunga vya mji wa Tehran. Amesema: Yumkini kukafanyika upotoshaji katika kipindi fulani kuhusu Imam Khomeini, lakini jua hilo halitabaki nyuma ya mawingu. 

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Imam Khomeini alifanya mageuzi matatu makubwa na yasiyo na kifani katika ngazi ya nchi, katika ngazi ya Umma wa Kiislamu na katika ngazi ya dunia, ambayo huenda yasitokee tena katika siku zijazo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Imam Khomeini (RA) alivunja muundo wa kisiasa wa kifalme na badala yake akaanzisha demokrasia na kuongeza: Imam Khomeini aliondoa mfumo usio wa Kiislamu kwenye uwanja, akabadilisha udikteta na kuweka uhuru mahala pake, akajenga hali ya kujiamini mahali pa kutokuwa na utambulisho, na akabadilisha hali ya kuwa tegemezi kwa wageni na kuifanya hali ya 'sisi tunaweza'. 

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, kizazi kipya kina haja ya kumtambua vyema imam Ruhullah Khomeini. 

Ayatullah Khamenei amesema kuwa Imam Khomeini (RA) alihuisha uzingatiaji wa masuala ya kiroho hata katika nchi zisizo za Kiislamu na akasema: Hali ya masuala ya kiroho duniani ilikuwa ikikanyagwa na baadhi ya madola, na harakati ya Imam Khomeini ilihuisha masuala hayo duniani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua kuwa, mageuzi haya ya Imam yamekabiliwa na upinzani wa madola ya kibeberu ambayo yanafanya kila linalowezekana kukabiliana na ufufuaji wa masuala ya kiroho.

Ameashiria vita vya kambi ya ubeberu dhidi ya Jamhuri ya Kislamu na kusema: "Kinachoweza kusimama mbele ya harakati yetu kama bonde hatari ni kusahau na kughafilikka na safu za adui."

Ayatullah Khamenei amesema kwamba maadui wameshindwa katika majaribio yao mengi dhidi ya Iran na akaongeza: Jaribio la hivi karibuni la adui lilikuwa ghasia za miezi kadhaa iliyopita hapa nchini, na kwamba machafuko hayo yalipangwa katika duru za kifikra za nchi za Magharibi.

Amesisitiza udharura wa kuimarishwa moyo wa imani na matumaini mema hususan kati ya tabaka la vijana na kusema: Wimbi la mashambulizi ya maadui linalenga kudhoofisha imani na matumaini katika nyoyo za watu.

Sehemu nyingine za hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kumbukumbu ya kifo cha hayati Imam Ruhullah Khomeini itakujieni katika matangazo yetu yajayo. 

captcha