IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Saudia iwajibike maafa ya Mina, siku tatu za maombolezo Iran

23:51 - September 24, 2015
Habari ID: 3367103
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametangaza siku tato za maombolezo ya kitaifa kufuatia vifo vya mamia ya mahujaji waliokuwa katika ibada ya Hija huko Mina, karibu na mji mtakatifu wa Makka.

Zaidi ya Mahujaji 1,200 walipoteza maisha na maelfu ya wengine kujeruhiwa mapema Alhamisi katika msongamano wa mahujaji wakati wa kutekeleza ibada ya Hija huko Mina karibu na Makka.Katika ujumbe alioutoa leo Alhamisi, Ayatullah Khamenei alisema: Serikali ya Saudi Arabia inawajibika kukubali jukumu lake zito katika tukio hili chungu na kuchukua hatua kwa mujibu wa kanuni za haki na insafu, sambamba na kutilia maanani uendeshaji mbaya na hatua zisizofaa zilizosababisha maafa haya. Ujumbe kamili wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni huu ufuatao:
Bismillahir Rahmanir Rahim
Sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake Yeye tutarejea.
Maafa yaliyosababisha msiba mkubwa leo huko Mina ambapo idadi kubwa ya Wageni wa Rahman na waumini waliohajiri kwenda kwa Mwenyezi Mungu kutoka nchi mbalimbali wameaga dunia, yamesababisha huzuni kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu na kuibadili sikukuu ya Idi kuwa maombolezo. Katika nchi yetu azizi pia makumi ya familia zilizokuwa zikisubiri kwa shauku kubwa ndugu zao wapendwa waliokwenda kuhiji, sasa zinaomboleza vifo vyao.
Kwa moyo uliojaa huzuni na mshikamano na waliopatwa na maafa, ninatoa mkono wa taazia kwa roho iliyotakasika ya Mtume Mtukufu (saw) na kwa Walii Mkubwa wa Mwenyezi Mungu, Imam wa Zama (roho zetu ziwe mhanga kwake) ambaye ndiye haswa mwenye msiba huu, na kwa jamaa wote wa wahanga na waombolezaji wote kote duniani, hususan nchini Iran kutokana na tukio hili la kuhuzunisha.
Ninawaombea wageni hawa wa Rahmani rehma makhsusi za Mwenyezi Mungu Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu na Mwenye kushukuru. Vilevile nawaombea shufaa ya haraka waliopatwa na madhara na majeruhi wa tukio hilo.
Ninapenda kukumbusha mambo kadhaa:
1- Maafisa wa ofisi ya mwakilishi wangu na Jumuiya ya Hija ambao kutwa nzima wamekuwa wakifanya jitihada kubwa za kutambua waliofariki dunia, kutibu majeruhi, kuwarejesha nchini na kupasha habari haraka, wanapaswa kuendelea na kazi hizo, na watu wote wenye uwezo wanawajibika kuwasaidia.
2- Maafisa hao wanapaswa pia kutoa msaada kwa mahujaji wa nchi nyingine na kutekeleza haki ya udugu wa Kiislamu.
3- Serikali ya Saudi Arabia inawajibika kukubali jukumu lake zito katika tukio hilo chungu na kutenda kwa mujibu wa haki na insafu. Uendeshaji mbaya na hatua zisizofaa zilizosababisha maafa haya pia zinapaswa kutiliwa maanani.
4- Waliofariki dunia katika tukio hili Inshaallah watakuwa kielelezo cha maneno haya yenye nuru ya Qur’ani inayosema: “Na mwenye kutoka nyumbani kwake ili kuhamia kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfika mauti basi yamethibiti malipo yake kwa Mwenyezi Mungu..”; suala hili ni pozo na tulizo kubwa kwa wafiwa. Mahujaji hao wamekimbilia kwa Mola wao baada ya kufanya twawafu, kufanya saayi (baina ya Swafa na Marwa) na baada ya masaa yenye baraka tele ya kusimama Arafa na Mash’ar wakiwa katika kutekeleza amali nyingine za Hija; na Inshaallah watapata rehma za Mwenyezi Mungu.
Ninatoa tena mkono wa pole kwa waliopatwa na msiba na ninatangaza siku tatu za maombolezo ya taifa hapa nchini.
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Sayyid Ali Khamenei
02/ Mehr/1394 (24/09/15)

.../mh

3367062

captcha