IQNA

Qur'ani Tukufu Inasemaje /46

Wale wanaopokea baraka za Mwenyezi Mungu na amani

17:38 - March 07, 2023
Habari ID: 3476672
TEHRAN (IQNA) - Baadhi ya wanadamu hupokea Salawat za Mwenyezi Mungu za baraka na amani. Wafasiri wa Qur'ani Tukufu wanasema kwamba Salawat ya Mwenyezi Mungu si maneno tu bali ni baraka, nuru na amani ambayo mtu huisikia kutoka ndani.

Aya ya 157 ya Sura Al-Baqarah inazungumzia ukweli mzuri kuhusu maisha ya watu wenye subira wanaopewa Salawat za Mwenyezi Mungu: “Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao Mlezi na rehema. Nao ndio wenye kuongoka."

Salawat ina maana gani hasa? Neno Salat kwa Kiarabu linamaanisha umakini na uthabiti. Kwa mujibu wa Tafsiri ya Al-Mizan ya Qur'ani Tukufu, Salawat maana yake ni rehema inapohusishwa na Mwenyezi Mungu, toba inapohusishwa na malaika, na sala inapohusishwa na watu.

Ayatullah Abdullah Javadi Amoli (aliyezaliwa 1933), anasema Salawat ya Mwenyezi Mungu haiko katika maneno bali iko katika vitendo vya Mwenyezi Mungu. Inaleta nuru, mwangaza na utakasifu katika moyo wa mtu. Kwa msingi wa hilo, anajitahidi kumtii Mwenyezi Mungu, anachukia dhambi, anaogopa moto wa mateso, anatamani sana kufika peponi, na anajitoa kabisa kwa wale wanaompenda Mungu.

Salawat ya Mwenyezi Mungu pia inadhihirisha sifa ya Mungu ya Hannan, ambayo ina maana ya huruma na fadhili. Kuna wema na huruma katika maana ya Salawat. Kwa hiyo Salawat maana yake ni Mwenyezi Mungu kuwapa baraka na nuru wale wanaosubiri.

Wafasiri wa Quran wanasema Salawat inaweza kuwa katika viwango tofauti. Ayatullah Javadi Amoli anasema kwamba kutokana na Salawat tukufu, Mtukufu Mtume (SAW) alifikia hadhi kwamba yeye mwenyewe akawa chanzo cha Salawat kwa wengine.

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 43 ya Surat Al-Ahzab: “Yeye na Malaika wake ndio wanakurehemuni ili kukutoeni gizani mwende kwenye nuru. Naye ni Mwenye kuwarehemu Waumini.”

captcha