IQNA

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamesimama kidete baada ya miaka 42

15:46 - February 02, 2021
Habari ID: 3473613
TEHRAN (IQNA) - Miaka 42 iliyopita taifa kubwa la Iran huku likiwa limejizatiti kwa imani thabiti na matumaini ya kuwa na mustkabali mzuri, na bila ya kutegemea dola lolote lenye nguvu duniani, lilifanikiwa kuweka nyuma kipindi kigumu na muhimu kwenye historia yake na hatimaye kufanikiwa kufikia kwa kishindo ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Tokea tarehe 12 hadi 22 Bahman mwaka 1357 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, kulijiri matukio muhimu nchini ambayo yalipelekea kung'olewa madarakani utawala fasidi wa Shah. Ni wazi kuwa matukio hayo yalisambaratisha kabisa mahesabu ya ufalme huo na waungaji mkono wake wa nje.

Kushindwa njama ya kumzuia Imam arejee nchini tarehe 12 Bahman, kuvunjwa Baraza la Ufalme na kubuniwa serikali ya mpito na Imam Khomeini (MA), kutangazwa mfungamano wa wafanyakazi wa sekta muhimu nchini kama vile sekta ya mafuta na harakati za mapinduzi ya wananchi, kupuuzwa sheria za kijeshi nchini kutokana na amri ya Imam, kumiminika mitaani wananchi na tangazo la kihistoria la kundi la kikosi cha anga la kumbai Imam tarehe 19 Bahman, ni matukio muhimu yaliyojiri nchini katika kipindi hicho na hatimaye kufanikisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Hotuba ya kihisotoria ya Imam Khomeini

Hotuba muhimu aliyoitoa Imam Khomeini (MA), Mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran tarehe 12 Bahman katika makaburi ya Beheshte Zahra (SA) mara tu baada ya kurejea nchini kutoka uhamishoni, kwa hakika ulikuwa ujumbe muhimu wa Mapinduzi. Sisitizo la Imam katika hotuba hiyo juu ya udharura wa wananchi kujiainishia  mustakbali wao wenyewe na kupewa umuhimu msingi wa kufanyika uchaguzi na kujitawala nchi katika nyanja zote ni miongoni mwa misingi muhimu ambayo iliimarisha nguzo za Mapinduzi ya Kiislamu nchini.

Ushindi wa Mapinduzi kwa hakika kulikuwa ni kuthibiti azma ya taifa kubwa la Iran kwa ajili ya kujitawala, kujipatia utukufu na heshima na hatimaye kujitoa katika minyororo na udhibiti wa madola ya kibeberu.

Chuki ya Marekani

Ni wazi kuwa chuki ya Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu inatokana na uamuzi wa busara wa wananchi shupavu wa Iran wa kuyachagua mapinduzi hayo ambayo yaliwasababishia mabeberu changamoto nyingi nchini na hivyo kuwa mfano bora wa kuigwa na mataifa mengine yaliyokuwa chini ya udhibiti na dhulma ya madola makubwa duniani.

Tokea mwanzoni mwa kubuniwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Marekani ililichukulia suala la kuangusha na kuitoa madarakani kuwa moja ya malengo yake ya kistratijia. Madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani yanatambua wazi kwamba kikwazo kikubwa zaidi kinachoyakabili katika utekelezaji wa njama zao za kutaka kuingusha serikali ya Kiislamu nchini Iran ni uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa serikali hiyo.

Katika miaka ya karibuni Marekani imetumia mbinu na nguvu zake zote kuiwekea Iran vikwazo vya kila aina ili kutoa mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya wananchi wa Iran eti kwa lengo la kuwafanya wakate tamaa na Mapinduzi ya Kiislamu na hivyo kutoa mwanya wa kuondolewa madarakani serikali yao wanayoipenda ya Kiislamu. Katika kipindi cha miaka 42 iliyopita Marekani haijawahi kulegeza hata siku moja msimamo wake wa kuiwekea Iran vikwazo vya Kiuchumi.

Taifa shupavu

Kutiliwa shaka shughuli za nyukli za Iran ambazo zinatekelezwa kwa malengo ya amani, kudai kwamba makombora ya Iran yanahatarisha usalama wa eneo, kupotoshwa kwa makusudi nia njema ya Iran kuhusu nchi za eneo, kuuliwa kigaidi makamanda shujaa wanaopambana vilivyo na magenge ya kigaidi katika eneo la Asia Magharibi wakiongozwa na Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na vilevile kuuawa kigaidi wasomi bingwa wa Iran wakiwemo wale wanaoshughulika na masuala ya nyuklia kama vile Mohsen Fakhrizadeh ni miongoni mwa hatua za uhasama ambazo zimetekelezwa na Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika miaka ya karibuni.

Licha ya hayo yote lakini taifa shupavu la Iran limesimama imara na kupitia mshikamano na umoja wake wa kitaifa, limethibitisha kivitendo kwamba hakuna dola lolote lenye nguvu duniani linaloweza kulidhuru wala kudhuru mfumo wa Mapinduzi ya Kiislamu.

3473878

captcha