IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu / 71

Misingi mitatu ya wito wa Nabii Nuh kwa Imani ya Mungu Mmoja

10:56 - April 15, 2023
Habari ID: 3476871
TEHRAN (IQNA) – Hadhrat Nuh alikuwa miongoni mwa Ulul'azm Anbiya (manabii wakuu). Kulingana na riwaya, alimwomba Mwenyezi Mungu ampe wakati wa kuwaongoza watu wake na alipewa takribani miaka 1,000.

Katika kuwalingania watu wake kwenye njia iliyo sawa, Nuhu (AS) alizingatia baadhi ya kanuni ambazo zimetajwa katika Surah Nuh.

Nuh ni jina la Surah ya 71 ya Qur'ani Tukufu. Ina Aya 28 na iko katika Juzuu ya 29. Ni Makki na ni sura ya 71 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Nuh (AS) ni miongoni mwa Mitume maalum wa Mwenyezi Mungu na Sura imepewa jina lake kwa sababu inaangazia hadithi yake. Sura hiyo ni taswira ya mapambano ya mara kwa mara kati ya wafuasi wa ukweli na wale wanaofuata batili. Pia inahusu programu ambazo wafuasi wa ukweli wanapaswa kutekeleza kwenye njia yao.

Kuna marejeo ya kisa cha Nuhu (AS) na hatima ya watu wake katika Sura mbalimbali za Qur'ani Tukufu. Kinachokuja katika Surah Nuh ni kuhusu sehemu maalum ya maisha yake ambayo haijatajwa mahali pengine katika Kitabu Kitukufu. Sura hii inazungumzia mwito wa mara kwa mara wa Nabii Nuh wa Tauhidi na jinsi alivyowatendea watu wake wakaidi ambao hawakuwa tayari kuikubali imani na kuwa waumini.

Hadithi ya Nabii Nuh (AS) na watu wake iliyotajwa katika Sura Nuh ni mfano wa Mitume wa Mwenyezi Mungu kuwalingania watu kwenye tauhidi, misimamo ya wakanushaji na mapambano baina ya haki na batili. Ndiyo maana imeitwa Surah Nuh.

Aya ya 3 ya Sura, “Ya kwamba mumuabudu Mwenyezi Mungu, na mumche Yeye, na munitii,” inaweka wazi kanuni tatu za mwaliko wa Nuhu kwa watu wake. Sehemu ya kwanza, “mumuabudu Mwenyezi Mungu”, inafunua jinsi watu wa Nuhu walivyofikiri juu ya Mungu walipokuwa wakiabudu sanamu badala ya kumwabudu Mungu. Kwa hivyo kanuni ya kwanza ya mwaliko wa Nuhu ni wito kwenye tauhidi. Kanuni ya pili, ambayo msingi wake ni maneno “mumche Yeye”, inasisitiza kuepuka dhambi na kutenda mema. Na sehemu ya tatu, " na munitii ", inasisitiza kwamba watu lazima wamtii Nuhu. Pia inathibitisha utume wake na ukweli kwamba watu wanapaswa kuchukua mafundisho ya dini kutoka kwake.

Sura inataja mapendekezo na nasaha za Nuhu, inasisitiza haja ya kumcha Mwenyezi Mungu na kumtii Yeye na Mitume Wake, inataja baraka za Mwenyezi Mungu, inabainisha alama na matokeo ya tauhidi, inafafanua zaidi juu ya kanuni za kiitikadi, Fiqhi, maadili na kijamii, na inaashiria dua zenye mafunzo za Nabii Nuh.

captcha