IQNA

Rais wa Iran katika shehre za kufunga Mashindano ya Qur'ani

Iran inaweza kuwa Mji Mkuu wa Kukuza Utamaduni wa Qur'ani Tukufu

10:45 - February 23, 2023
Habari ID: 3476610
TEHRAN (IQNA) - Rais wa Iran Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu Iran amesema Iran inaweza kuwa mji mkuu wa kukuza utamaduni wa Qur'ani Tukufu duniani.

Ameyasema hayo jana Jumatano jioni katika hotuba yake ya kufunga Mashindano ya 39 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu, ambapo washindi walitangazwa na kutunukiwa tuzo.

Hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Tehran, ilihudhuriwa pia na maafisa wengine wakuu, akiwemo Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu Mohammad Mehdi Esmaeili, na Waziri wa Elimu Yousef Nouri.

Sherehe hiyo ilianza kwa usomaji wa aya za Qur'ani Tukufu na Amir Hossein Rahmati, qari wa Kiirani aliyeshika nafasi ya kwanza katika kategoria ya kisomo.

Kisha, Hujjatul Islam Seyed Mehdi Khamoushi, Mkuu wa Shirika la Masuala ya Wakfu na Misaada, akawasilisha ripoti kuhusu shughuli za Qur'ani Tukufu za jumuiya hiyo, ikiwa ni pamoja na kuandaa mashindano ya Qur'ani ya kitaifa na kimataifa.

Amebainisha kuwa duru hii ya mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ilifanyika katika hatua mbili, ambapo duru ya kwanza ilifanyika kwa njia ya intaneti na kushirikisha wagombea 150 kutoka nchi 80.

Kutoka miongoni mwao, maqari 52 na wahifadhi kutoka nchi 33 walifika kwenye fainali iliyoanza mjini Tehran siku ya Jumamosi, aliongeza.

Baadaye, taarifa iliyotolewa na jopo la waamuzi wa shindano hilo ilisomwa na Abbas Salimi, ambaye aliongoza jopo katika sehemu ya wanaume.

Taarifa hiyo imelipongeza mashindano hayo yaliyofanyika kwa kauli mbiu ya “Kitabu Kimoja Umma Mmoja” na kusisitiza kuwa yanadhihirisha umoja na mshikamano wa Waislamu.

Aidha taarifa hiyo imelaani vitendo vya hivi karibuni vya kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu duniani, na kuwataka watu wote kusoma Qur'ani na kutafakari mafundisho yake matukufu.

Katika hotuba yake Rais Ebrahim Raisi aliyasifu mashindano hayo kama tukio kuu la Qur'ani katika ulimwengu wa Kiislamu.

Amesema Shirika la Masuala ya Wakfu na Misaada lina tajiriba nzuri katika kuandaa mashindano hayo na liko tayari kuzishirikisha na nchi nyingine.

Raisi ameongeza kuwa, mashindano hayo yanapaswa kuibua uvumbuzi na maendeleo katika kustawisha Qur'ani Tukufu. Rais wa Iran aidha alisistiza kuhusu umoja wa Waislamu duniani kote ili kuweza kukabiliana na njama za maadui.

Baadaye katika hafla hiyo, washindi wa kategoria tofauti walitajwa na kupokea tuzo zao.

Kwa upande wa wanawake, Fahimeh Asgharzadeh kutoka Iran, Layla Afara kutoka Lebanon na Ameneh Shirzad kutoka Afghanistan waliibuka wa kwanza hadi wa tatu katika kitengo cha Tartil.

Katika kuhifadhi Qur'ani nzima, wa kwanza alikuwa Amina Ibrahim kutoka Ghana akifuatiwa naHajar Mehralian kutoka Iran na Nasrin Khaledi kutoka Algeria.

Katika sehemu ya wanaume Tartil, Mohammad Javad Javeri kutoka Iran alinyakua tuzo ya juu, wakati Mohammad Yar kutoka Kyrgyzstan na Ismail Hamdan kutoka Lebanon aliibuka wa pili na wa tatu.

Msomaji bora wa mashindano hayo alikuwa Amir Hossein Rahmati kutoka Iran. Mshindi wa pili katika qiraa alikuwa Seyed Amir Hashemi kutoka Afghanistan na mshindi wa tatu alikuwa Abdullah Fikri kutoka Indonesia.

Na katika kategoria ya mwisho, yaani kuhifadhi Qur'ani Tukufu, tuzo kuu ilienda kwa Sina Tabakhi kutoka Iran huku Abdul Alim Abdul Rahim kutoka Kenya akishika nafasi ya pili na Sheikh Mahmoud Hassan kutoka Bangladesh alifanikiwa kupata nafasi  ya tatu katika kategoria hii.

4123916

captcha