IQNA

Shakhsia katika Qur'ani Tukufu/24

Musa; Nabii aliyeinukua katika nyumba ya adui

19:02 - December 31, 2022
Habari ID: 3476333
TEHRAN (IQNA) – Musa-Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake- (AS)-, nabii mkuu wa Bani Isra’il ambaye aliinukua katika nyumba ya Firauni, aliwaokoa watu kutokana na dhulma ya Firauni.

Musa (AS) anasemekana kuwa alikuwa wa ukoo wa Lawi, mwana wa Yaqub (AS). Jina la baba yake limetajwa kuwa ni Amram katika Taurati na Waislamu wanamfahamu kama Imran.

Musa (AS) alizaliwa yapata miaka 250 baada ya kifo cha Ibrahimu (AS). Kuzaliwa kwake kulikuja wakati ambao Firauni alikuwa ameamuru kuuawa kwa watoto wote wa kiume wa Bani Israil na kuwekwa kizuizini kwa wasichana wote. Baadhi ya wanahistoria wanasema Firauni alitoa amri hiyo akihofia kwamba Bani Isra'il wanaweza kupata nguvu na kuunda umoja na maadui zake wakati baadhi ya wengine wanasema alifanya hivyo baada ya kuota ndoto kuhusu mvulana kutoka Bani Isra'il akiharibu utawala wake.

Kwa mujibu wa aya za Qur'ani Tukufu, baada ya Musa kuzaliwa, mama yake (Yokebed) alipewa wahyi kumnyonyesha na kisha kumtupa majini.

“Tulimfunulia mama yake Musa kwa kumwambia: Mnyonyeshe. Na utakapo mkhofia basi mtie mtoni, na usikhofu wala usihuzunike. Hakika Sisi tutamrudisha kwako na tutamfanya miongoni mwa Mitume.  Basi wakamwokota watu wa Firauni, aje kuwa adui kwao na huzuni. Hakika Firauni na Hamana na majeshi yao walikuwa wenye makosa.  Na mkewe Firauni alisema: Atakuwa kiburudisho cha macho kwangu na kwako. Msimuuwe! Huenda akatufaa, au tumpange kuwa mwenetu. Wala wao hawakutambua.  Na moyo wa mama yake Musa ukawa mtupu. Alikuwa karibu kumdhihirisha, ingeli kuwa hatukumtia nguvu moyo wake ili awe miongoni mwa Waumini.  Naye akamwambia dada yake Musa: Mfuatie. Basi naye akawa anamuangalia kwa mbali bila ya wao kujua.  Na tukamjaalia awakatae wanyonyeshaji wote tangu mwanzo, mpaka dada yake akasema: Je! Nikuonyesheni watu wa nyumba watakao mlea kwa ajili yenu, nao pia watakuwa wema kwake? Basi tukamrudisha kwa mama yake ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike. Na ajue ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, lakini wengi wao hawajui. (Surah Al-Qasas, Aya ya 7-13)

Basi mama yake Musa akamnyonyesha mtoto wake. Musa alikulia katika nyumba ya Firauni mpaka alipokuwa kijana. Musa, tofauti na Firauni, alikuwa mwamini Mungu mmoja na hakuweza kuvumilia uonevu na ukandamizaji.

Siku moja, alipomwona mtu wa Misri akimshambulia mtu kutoka Bani Israil, Musa alimlinda mtu huyo aliyeonewa na kumpiga yule Mmisri kifuani. Mtu huyo alikufa na Musa akatoroka Misri. Alikwenda Madyan, ambako alikutana na wasichana waliokuwa wakitafuta kondoo. Musa (AS) aliwasaidia katika kuwanywesha kondoo na akafuatana nao hadi nyumbani kwao.

Hao walikuwa mabinti wa Shuaib (AS). Walimsihi baba yao kumwajiri Musa (AS) naye akakubali. Kisha Shuaib (AS) akamuoza Musa binti yake. Inasemekana Musa alifanya kazi kwa Shuaib kwa miaka kumi, akijifunza Hikma (hekima) na elimu kutoka kwake.

captcha