IQNA

Ni kwa nini utawala wa Israel umeshadidisha hujuma katika Quds Tukufu?

21:20 - April 26, 2021
Habari ID: 3473852
TEHRAN (IQNA)- Kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani kumekwenda sambamba na kuanza duru mpya ya mivutano baina ya Wapalestina na Wazayuni huko Quds inayokaliwa kwa mabavu ambapo Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imetoa mwito wa kufanyika Intifadha ya Quds.

Tangu ulipoanza mwezi mtukufu wa Ramadhani hadi sasa kumeshuhudiwa mapigano huko Quds baina ya Wapalestina na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Hadi sasa Wapalestina wasiopungua 200 wametiwa mbaroni. Mapigano ya Ijumaa iliyopita huko Quds yalipelekea zaidi ya Wapalestina 100 kujeruhiwa. Aidha katika mapigano ya siku ya Jumamosi takribani walowezi wa Kizayuni 20 na wanajeshi wa Kizayuni walijeruhiwa.

Shirika la Hillali Nyekundu la Palestina lilitangaza Jumapili ya jana kwamba, Wapalestina 12 wamejeruhiwa katika shambulio la jeshi la Israel katika viunga vya kitongoji cha kale cha Quds inayokaliwa kwa mabavu. Fauka ya hayo, siku za hivi karibuni zimeshuhudia zaidi ya maroketi 40 yakivurumishwa kutoka Ukanda wa Gaza kuelekea upande wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Benny Gantz, Waziri wa Vita wa utawala ghasibu wa Israel alitoa tishio siku ya Jumamosi baada ya kikao cha usalama cha utawala huo kilichoitishwa kutathmini hali ya mzozo na mvutano na Gaza kwamba, atashadidisha mapigano.

Hivi sasa swali la kimsingi linaloulizwa ni hili kwamba, sababu ya kuanza duru hii ya mivutano ni nini hasa?

Tunaweza kusema kuwa, sababu muhimu zaidi ya kuanza duru hii mpya ya mzozo inarejea katika kadhia ya Quds na msikiti wa al-Aqswa. Kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani kulikwenda sambamba na kuongezeka idadi kubwa ya Wapalestina Waislamu waliokuwa na nia ya kufanya itikafu katika msikiti wa al-Aqswa. Hata hivyo Wapalestina hao walikabiliwa na vizingiti vya jeshi la Israel lililokuwa likiwazuia kwenda katika msikiti huo.

Mbali na sababu nyingine ulizokuwa nazo utawala ghasibu wa Israel kwa ajili ya kuwakandamiza Wapalestina na kuzusha machafuko huko Quds na katika Msikiti wa al-Aqswa, filihali utawala huo unadai umiliki wa mji huo. Madai hayo ya Israel chimbuko na taathira yake ni uamuzi wa Disemba 2017 wa aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump wa kuitangaza Baytul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel na kuhamishia ubalozi wake katika mji huo kutoka Tel-Aviv.

Ukweli wa mambo ni kuwa vurugu na machafuko ya sasa huko Quds ni mapigano kuhusiana na umiliki wa mji huo muhimu na wa kistratejia. Khalid al-Qaddumi, mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) hapa mjini Tehran anasema: Kile ambacho kinatokea sasa huko Quds, ni vita vya kutaka kuthibitisha umiliki na mamlaka hususan ya msikiti wa al-Aqswa na maeneo yake ya kando kando ambayo Wazayuni wanayatambua kama Hodhi Takatifu.

Sababu ya pili ya vuguru na machafuko ya sasa huko Quds inarejea katika kadhia ya uchaguzi. Wapalestina wanatarajiwa kufanya uchaguzi wa Bunge tarehe 22 ya mwezi ujao wa Mei. Wapalestina wanasisitiza kuwa, uchaguzi huo ufanyike pia huko Quuds. Hata hivyo Israel inakataa kufanyika uchaguzi wa Bunge huko Quds ikidai kwamba, ina mamlakka ya mji huo. Wapalestina wanaamini kuwa, uchaguzi wa Bunge ambao haujumuishi eneo la Quds sio tu kwamba, hauna itibari na thamani, bali itakuwa ni kukubali kwamba, mji huo ni milki ya utawala huo vamizi.

Katika upande mwingine, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala dhalimu wa Israel ambaye amepewa tena jukumu la kuunda serikali mpya ambapo kuna uwezekano wa kufanyika uchaguzi wa tano wa Bunge ana mahesabu maalum na kadhia ya Quds na Wazayuni wenye kufurutu ada kwa ajili ya kufikia malengo yake ya kisiasa. Kwa msingi huo, kutofanyika uchaguzi wa Bunge la Palestina huko Quds yatakuwa mafanikio muhimu kwa Netanyahu.

Khalid al-Qaddumi, mwakilishi wa Hamas mjini Tehran anasema: Tanuri la moto wa uchaguzi ambapo utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya chaguzi nne za Bunge katika kipindi cha chini ya miaka miwili na kufanya juhudi serikali ya Kizayuni hususan Netanyahu kwa ajili ya kupata kura nyingi zaidi za Wazayuni wenye kufurutu ada kwa kuwarahisishia mambo na kuwapatia upendeleo maalum kama kuwaruhusu kufanya hujuma dhidi ya msikiti wa al-Aqswa na kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina huko Quds, ni sababu nyingine ya matukio ya sasa huko Quds.

Kushadidi vurugu na machafuko hayo, kumeifanya Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina itoe mwito wa kuanzishwa Intifadha ya Ramadhani na kuwataka Wapalestina kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika Itifadha hii Tukufu ya Ramadhani.

3474557

Kishikizo: palestina quds
captcha