IQNA

Hania: Quds inashuhudia vita vya irada baina ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni

21:13 - April 23, 2021
Habari ID: 3473843
TEHRAN (IQNA)- Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, Quds (Jerusalem) haitasalimu amri katika vita vya utambulisho mbele ya utawala haramu wa Israel na siasa zake za ubaguzi.

Ismail Hania amesema hayo, baada ya hujuma na mashambulio ya wavamizi dhidi ya Quds inayokaliwa kwa mabavu yaliyopelekea kujeruhiwa Wapalestina kadhaa na kubainisha bayana kwamba, kile ambacho kinatokea hivi sasa huko Quds ni vita vya irada baina ya taifa lililo katika uvamizi na utawala vamizi.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameeleza kuwa, taifa la Palestina haliko peke yake huko Quds na kwamba, watu wote watatetea na kulinda ardhi na matukufu ya Kiislamu ambayo yamo mbioni kuangamizwa na utawala ghasibu wa Israel.

Usiku wa jana (Alkhamisi) wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walifanya hujuma na mashambulio huko Quds inayokaliwa kwa mabavu ambapo zaidi ya Wapalestina 100 wamejeruhiwa katika tukio hilo.

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na uvamizi wake dhidi ya maeneo ya Wapalestina ukifanya njama za kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.

Msikiti wa al-Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu umekuwa ukiandamwa na njama mtawalia za utawala vamizi wa Israel, hatua ambazo zinakwenda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi na maeneo ya Wapalestina.

3966603

captcha