IQNA

Mtazamo wa Maadili Katika Qur'ani/ 2

Uhasidi; Uovu wa kimaadili uliosababisha mauaji ya kwanza baina ya ndugu

19:46 - March 05, 2024
Habari ID: 3478452
IQNA – Wivu au uhasidi ni tabia mbaya ambayo husababisha mtu kutaka wengine kupoteza baraka zao. Kwa hakika wivu ulikuwa sababu ya mauaji ya kwanza na pia mauaji ya kwanza baina ya ndugu wa familia moja katika historia ya wanadamu.

Kwa hiyo uhasidi ulikuwa miongoni mwa maovu ya kwanza ya kimaadili ambayo yaliwakumba watoto wa Adam (AS) duniani.

Mtu anayesumbuliwa na wivu au uhasidi hukasirika anapoona baraka za Mwenyezi Mungu zikimfikia mtu mwingine. Katika kiwango fulani cha wivu, anatamani baraka wanayopewa wengine iondolewe kutoka kwao, na kwa kiwango cha juu anajaribu kuiharibu yeye mwenyewe.

Suala la uhasidu limetajwa kwa sura tofauti katika visa vya Qur'an Tukufu, vikiwemo visa vya Habil na Kain, Nabii Yusufu (AS) na ndugu zake, na wale waliohusudu hadhi ya Mtukufu Mtume  Muhammad (SAW).

Katika Surah Al-Falaq aya ya 1-5, Qur'ani Tukufu inautaja uhasidi kama chanzo cha uovu na ufisadi duniani na inamuamuru Mtume (SAW) kujikinga kwa Mwenyezi Mungu kutokana na wale wanaohusudu:

Sema: Najikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko, Na shari ya alivyo viumba, Na shari ya giza la usiku liingiapo, Na shari ya wanao pulizia mafundoni,  Na shari ya hasidi anapo husudu.

Wivu wa kwanza unaotajwa ni ule wa Kain ambaye alimwonea wivu ndugu yake Habil. Alikuwa na wivu kwa sababu Mwenyezi Mungu alikubali dhabihu ya Habil lakini si yake. Na hii ikapelekea kumuua kaka yake. Tunasoma hivi katika Qur'ani Tukufu:  “Na wasomee khabari za wana wawili wa Adam kwa kweli. Walipo toa mhanga, ukakubaliwa wa mmoja wao, na wa mwengine haukukubaliwa. Akasema: Nitakuuwa. Akasema mwengine: Mwenyezi Mungu huwapokelea wachamngu. (Aya ya 27 ya Surah Al-Ma’idah)

Katika Aya ya 51 ya Surah An-Nisa ya Qur'ani Tukufu, tunasoma kwamba baadhi ya Mayahudi, wakijaribu kuwatuliza waabudu masanamu wa Makka, walisema kwamba kuabudu masanamu kwa Kabila la Maquraishi ni bora kuliko Waislamu wanavyomuabudu Mwenyezi Mungu.

" Huwaoni wale walio pewa sehemu ya Kitabu? Wanaamini masanamu na Shet'ani! Na wanawasema walio kufuru, kuwa hao wameongoka zaidi katika njia kuliko Walio amini."

 Katika Aya ya 54, Mwenyezi Mungu anaeleza hukumu yao kuwa haina thamani, akisema inatokana na kuwa na wivu juu ya Mtume (SAW).

“Au wanawahusudu watu kwa yale aliyo wapa Mwenyezi Mungu kwa fadhila yake? Basi tuliwapa ukoo wa Ibrahim Kitabu na hikima na tukawapa utawala mkubwa." (Aya ya 54 ya Surah An-Nisa)

Kwa mujibu wa Hadith zilizosimuliwa katika vyanzo vya Sunni na Shia, aya hii inaashiria kwamba Mtukufu Mtume (SAW) na watu wa nyumbani mwake yaani Ahul Bayt (AS) walihusidiwa sana.

Aya hii pia inataja baraka alizopewa Ibrahim (AS) na watu wake, ambazo Mayahudi wanazikubali, na kuhoji kwa nini hawazikiri baraka hizi.

Kwa mujibu wa aya hii, Kitabu, Hikima na Ufalme mkubwa alipewa Ibrahim (AS).

Wivu ni uovu unaoweka msingi wa maovu na dhambi zingine. Mtu mwenye wivu hukimbilia kusengenya, chuki na maovu mengine na hufanya kila kitu ili baraka anazopewa mtu mwingine ziondolewe kwake. Ndio maana katika Hadithi kutoka kwa Imam Ali (AS), husuda imetajwa kuwa chimbuko la maovu. Kufikiri juu ya madhara yanayoletwa na husuda au wivu, kuongeza hekima, kuimarisha imani, na kuzingatia mafundisho yaliyojaa Hekima ya Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa njia za kutibu ugonjwa sugu wa uhasidi.

3487369

 

captcha