IQNA

Maadili katika Qur'ani /2

Unyenyekevu; Tabia ya Waumini

16:51 - June 02, 2023
Habari ID: 3477083
TEHRAN (IQNA) – Katika maingiliano ya binadamu, kuheshimiana ni miongoni mwa kanuni muhimu zinazosaidia kukuza urafiki na mapenzi miongoni mwao.

Moja ya kanuni muhimu inayoongoza kwenye heshima ni unyenyekevu na mtu yeyote ambaye ni mnyenyekevu atakuwa maarufu.

Unyenyekevu ni miongoni mwa sifa za waumini zilizotajwa ndani ya Qur’ani Tukufu: “Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanao tembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama.” ( Aya ya 63 ya Sura Al-Furqan).

Unyenyekevu unamaanisha kutojiona bora kuliko wengine na unajumuisha maneno na matendo yanayowaheshimu wengine.

Kama sifa nyingine za maadili na akhlaqi njema, unyenyekevu ni sifa iliyo kinyume cha kiburi na udhalilishaji.

Anayejaribu kuwapita wengine kama yeye katika kila jambo na kujiona bora kuliko wengine ni jeuri. Hili halistahiki kusifiwa.

Unyenyekevu unastahili kusifiwa unapokuwa wa wastani bil kuvuka mipaka. Faid za unyenyekevu ni pamoja na

1- Utaratibu na mpangilio wa mambo

Imepokewa kutoka kwa Imam Ali (AS) kwamba unyenyekevu unasaidia kuleta utulivu na mpangilio katika mambo ya jamii.

Jamii inahitaji ushirikiano na maelewano miongoni mwa wanajamii. Ikiwa watu watakuwa na kiburi na kuoneana majivuno, kwa kawaida utaratibu na mpangilio katika jamii utapotea na mambo hayatafanyika. Kwa hivyo unyenyekevu ni muhimu katika jamii.

2- Umaarufu

Ni wazi kwamba watu wenye kiburi huchukiwa na watu na hakuna mtu anayewapenda. Unyenyekevu, kwa upande mwingine, humfanya mtu kuwa maarufu. Huenda wengine wakafikiri unyenyekevu husababisha mtu kupoteza hadhi na heshima yake katika jamii ilhali, kinyume chake, watu wanyenyekevu wanaheshimiwa na kupendwa zaidi katika jamii.

Ndio maana Imam Ali (AS) amesema kwamba tunda la mti wa unyenyekevu ni upendo na tunda la mti wa kiburi ni laana ya watu.

 

captcha