Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini (mwenyezi Mungu
amrehemu) ndiye aliyeipa siku hiyo ya Ijumaa ya mwisho ya mwezi Ramadhani jina
la Siku ya Kimataifa ya Quds kwa shabaha ya kuakisi dhulma ya kihistoria
inayofanywa na madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu, dhidi ya
watu wanaoendelewa kudhulumiwa na kukandamizwa wa Palestina na ardhi yao takatifu.
Suala la kukombolewa Palestina kutoka kwenye makucha ya Wazayuni maghasibu
lilikuwa miongoni mwa malengo na kaulimbiu kuu za Imam Ruhullah Khomeini tangu
alipoanza harakati zake hapo mwaka 1960. Wakati huo Imam alikutaja kuasisiwa
dola haramu la Israel katika ardhi ya Palestina kuwa ni kitendo cha kishetani
na kuutaja utawala huo kuwa ni tezi ya saratani ambalo inapaswa kuondolewa na
kukatwa kwa njia yoyote ile inayowezekana.
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wakati ulimwengu wa Kiislamu ulipokuwa
bado katika mshtuko wa kutiwa saini makubaliano ya fedheha ya Camp David kati
ya aliyekuwa rais wa Misri, Anwar Sadat na waziri mkuu wa wakati huo wa utawala
haramu wa Israel Menachem Begin chini ya usimamizi wa rais Jimmy Carter wa
Marekani, hatua ya Imam Khomeini ya kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi
mtukufu wa Ramadhani kuwa ni siku ya maandamano ya kuhamasisha ukombozi wa Quds
tukufu, kwa mara nyingine tena ilihuisha matumaini katika nyoyo za Waislamu.
Miezi sita tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, yaani
tarehe sita Agosti mwaka 1979 sawa na tarehe 13 Ramadhani mwaka 1399 Hijria
sambamba na kuanza duru mpya ya jinai na ukatili wa Israel huko Lebanon, Imam
Khomeini alitoa taarifa akiitangaza Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi wa Ramadhani
kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Quds na akawata Waislamu kote duniani kuonesha
mshikamano wao katika siku hiyo. Katika sehemu moja ya ujumbe wake siku hiyo
Imam Khomeini alisema: "Kwa miaka mingi sasa nimekuwa nikiwatahadharisha
Waislamu kuhusu hatari ya utawala ghasibu wa Israel ambao sasa na katika siku
hizi umezidisha mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya ndugu zetu wa Palestina
hususa huko kusini mwa Lebanon kwa shabaha ya kuangamiza kabisa wanamapambano
wa Kipalestina... Nawataka Waislamu kote duniani na serikali za nchi za
Waislamu kushikamana kwa ajili ya kukata mkono wa ghasibu huyo na wasaidizi
wake. Vilevile nawaomba Waislamu wote duniani kuichagua Ijumaa ya mwisho ya
mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Quds ambayo inaweza kuainisha hatima ya
Wapalestina na watangaze mshikamano wa kimataifa wa Kiislamu katika kutetea
haki za kisheria za Waislamu wenzao wa Palestina…" mwisho wa kunukuu.
Hatua hiyo ya busara ya Imam Khomeini katika kipindi hicho ilivunja njama za
Wazayuni wakiungwa mkono na madola ya Magharibi na viongozi wa nchi kadhaa za
Kiarabu kama Anwar Sadat na Mfalme Hussein wa Jordan za kutaka kuutambua rasmi
utawala haramu wa Israel.
Kwa upande mwingine mataifa mbalimbali ya Waislamu yalikaribisha hatua hiyo ya
Imam Khomeini ya kutangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani kuwa Siku ya
Kimataifa ya Quds. Waislamu katika mabara yote ya dunia katika kipindi chote
cha miaka 37 iliyopita tangu kutangazwa siku hii, wamekuwa wakishiriki kwa
wingi katika maandamano ya siku hiyo na kuhuisha pamoja na kuunga mkono malengo
ya Wapalestina ya kukomboa Quds tukufu kutoka kwenye makucha ya Wazayuni.
Kwa sasa huko katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu utawala wa Kizayuni wa
Israel umechukua hatua kali za kiusalama dhidi ya Wapalestina wanaojitayarisha
kuadhimisha siku hiyo Ijumaa hii kwa kuwazuia hata kuingia katika Msikiti wa al
Aqsa. Katika miaka iliyopita maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds huko
Palestina inayokaliwa kwa mabavu yamekuwa yakiandamana na umwagaji damu na
makumi ya Wapalestina huuawa kila mwaka katika siku hiyo kwa kupigwa risasi na
askari wa Israel na wengine kujeruhiwa. Hata hivyo na licha ya ukatili huo,
maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds yamekuwa yakifanyika kwa adhama na kwa
idadi kubwa zaidi kuliko mwaka wa kabla yake. <<<< >>>>
Moja kati ya maadhimisho makubwa zaidi dunia ya Siku ya Kimataifa ya Quds
hufanyika nchini Iran. Wananchi katika miji na vijiji vyote vya Iran
huadhimisha siku hiyo kwa maandamano na mikusanyiko wakionesha mshikamano wao
na wenzao wa Palestina wanaoendelea kukandamizwa na kusisitiza umuhimu wa
kukombolewa Quds tukufu. Wairan hawakuacha kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya
Quds hata katika kipindi cha mashambulizi ya kinyama ya makombora na ndege za
kivita za utawala wa Saddam Hussein. Kushiriki kwa wingi mamilioni ya Wairani
katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds ni ishara ya kuendelea kuhuishwa
malengo na thamani za Wapalestina za kutaka kukombolewa Quds na nchi yao.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mstari wa mbele daima kuwatetea na
kuwasaidia kisiasa, kifedha, kijeshi na kiroho Wapalestina hata katika siku na
kipindi kigumu cha mashambulizi ya Wazayuni wa Israel, wakati nchi za Kiarabu
zilipowaacha na kuwapuuza Waislamu wenzao wa Palestina hususan wakazi wa Ukanda
wa Gaza. Inatupasa pia kuelewa kwamba, kambi ya muqawama na mapambano dhidi ya
maghasibu Wazayuni huko Lebanon na Palestina ilianzishwa kwa msaada wa Jamhuri
ya Kiislamu ya Iran. Vilevile ushindi wa mara kwa mara wa wanamapambano wa
Lebanon na Palestina mkabala wa Wazayuni huko Lebanon na Gaza ni matunda ya
misaada hiyo ya Iran.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haijawahi kuwa na mtazamo wa kimadhehebu au
kimakundi katika kuyaunga mkono makundi na harakati za mapambao ya Kiislamu.
Kwa mfano tu Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas inapewa
umuhimu na kusaidiwa ipasavyo na Jamhuri ya Kiislamu sawa kabisa na ilivyo kwa
harakati ya Hizbullah ya Lebanon. Iran haikubadili kamwe mtazamo na mwenendo
wake huo wa kuzisaidia harakati za ukombozi wa Palestina licha ya baadhi ya
maafisa wa harakati Hamas kubadili mwelekeo wao na kujitenga kiasi na Jamhuri
ya Kiislamu.
Utawala bandia wa Israel na waungaji mkono wake wa Kimagharibi hususan Marekani
wanaelewa kwamba, nukta ya udhaifu wa utawala huo ni kambi ya muqawama na harakati
za mapambano ya ukombozi wa Kiislamu katika nchi za Syria na Lebanon. Kwa
msingi huo walifikia uamuzi kwamba, wanaweza kutimiza malengo yao ya muda mrefu
ya kuhalalisha uwepo wa dola bandia la Israel kwa kuanzisha migawanyiko na
mpasuko katika kambi hiyo. Wazayuni na washirika wao wamefanya jitihada kubwa
katika uwanja huo na kwanza walitumia uwezo wao wote wa kijeshi kuvamia eneo la
kusini mwa Lebanon hapo mwaka 2006 kwa shabaha ya kuisambaratisha harakati ya
Hizbullah. Hata hivyo mapambano ya kishujaa ya Hizbullah katika vita vya siku
33 na ushindi mkubwa wa wapiganaji wa harakati hiyo viliambatana na kushindwa
kihistoria kwa utawala bandia wa Israel. Wakati huo huo ushindi wa wapiganaji
wa Hamas mbele ya uvamizi wa Israel katika eneo la Gaza hususan uwezo wa
makombora ya harakati hiyo wa kupiga maeneo ya Tel Aviv, vimeonesha tena ni kwa
kiwango gani Israel inakabiliwa na changamoto kubwa. Ni kutokana na kushindwa
na changamoto hizo ndipo kukaanzishwa mradi wa kuzusha ghasia na vita vya ndani
nchini Syria kwa kutumia kisingizio cha kuimarisha demokrasia na kuiondoa
madarakani serikali halali ya nchi hiyo. Watekelezaji wakuu wa mradi huo ni
Saudi Arabia, Uturuki na Qatar wakisaidiwa na Israel na nchi kadhaa za
Magharibi hususasn Marekani. Mradi huo ulianzishwa kwa shabaha ya
kusambaratisha kambi ya muqawama na mapambano ya ukombozi dhidi ya Israel na
kuliondoa kabisa suala la kukaliwa kwa mabavu Palestina katika ajenda kuu ya
ulimwengu wa Kiislamu. Katika fremu hiyo yalianzishwa na kuimarishwa makundi ya
kigaidi na kitakfiri kama Daesh na Jabhatu Nusra katika nchi za Syria na Iraq
ambayo sasa yamekuwa tishio kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu. Mgogoro huo
umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa
wakimbizi.
Sera na siasa hizo za utawala bandia wa Israel na washirika wake za
kuzishughulisha nchi za Kiislamu na kuzusha migogoro ya ndani zimewafanya
walimwengu wasahau au kuyapa umuhimu ndogo maudhui ya Palestina na masaibu
wanayoendelea kukutana nayo watu wa Palestina. Siku ya Kimataifa ya Quds ni
cheche na chachu inayowaamsha Waislamu na wapenda haki kote ulimwenguni na
kuwataka waelewe kwamba, chanzo cha migogoro na matatizo mengi ya ulimwengu wa
Kiislamu na Mashariki ya Kati ni utawala bandia na haramu wa Israel. Kwa msingi
huo nchi za Waislamu hazitapata ustawi, amani na maendeleo maadamu utawala bandia
wa Israel ungalipo na unaendelea kuungwa mkono kwa hali na mali na washirika
wake wa Magharibi na vibaraka wao kama Saudi Arabia, Uturuki n.k.