Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu ameyasema hayo leo asubuhi (Ijumaa) alipohutubia umati mkubwa uliojaa
shauku wa matabaka mbali mbali ya watu katika Haram toharifu ya Imam Khomeini (quddisa
sirruh) iliyoko kusini mwa Tehran. Ameongeza kuwa Imam Khomeini alikuwa ni mwanachuoni muumini wa kweli,
mchaji Mungu na mwanamapinduzi, amesisitizia wajibu wa kuendelezwa njia ya Imam
mwanamapinduzi wa taifa la Iran ikiwa ndiyo njia pekee ya kuleta maendeleo na
kufanikisha malengo ya wananchi na ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Vile vile
amebainisha vielelezo vitano muhimu vya kuwa mwanapinduzi na kusema: Inabidi
kuendelea na harakati na kufanya juhudi za kuiletea maendeleo nchi kwa kutumia
uzoefu uliopatikana katika mazungumzo ya nyuklia, yaani kuthibiti udharura wa
kutokuwa na imani na Marekani.
Katika hotuba yake hiyo aliyoitoa katika maadhimisho ya kukumbuka miaka
ishirini na saba ya kufariki dunia Imam Khomeini (Rahmatullahi Alayh),
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, istilahi ya muumini mcha Mungu
mwanamapinduzi ni ibara iliyokusanya kila kitu katika sifa alizokuwa nazo Imam
Khomeini (quddisa sirruh) na kuongeza kuwa: Imam wetu mtukufu alikuwa ni
muumini wa kweli wa Mwenyezi Mungu, muumini wa kweli wa watu, muumini wa kweli
wa malengo yake na mumini wa kweli wa njia aliyotumia kwa ajili ya kufikia
malengo.
Amma kuhusiana na sifa ya ucha Mungu ya Imam (Rahmatullahi Alayh), Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Imam alikuwa mja mwema wa Mwenyezi
Mungu. Alikuwa mtu wa unyenyekevu, maridhia na mtu wa dua.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia sifa ya tatu maalumu
aliyokuwa nayo Imam (quddisa sirruh) na kusema kuwa: Imam, alikuwa ni Imam
mwanamapinduzi, na sifa hiyo ndiyo sababu kuu ya hasira za madola ya kimaada ya
dunia.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa, madola ya kibeberu yanaliogopa
mno neno Mapinduzi na kuwa Iran taifa la wanamapinduzi na kuongeza kuwa: Sababu
kuu ya mashinikizo ambayo yamekuwepo dhidi ya taifa la Iran katika kipindi cha
miaka mingi sasa kwa visingizio tofauti kama vile kadhia ya nyuklia na haki za
binadamu, inatokana na woga huo huo wa madola ya kibeberu wa kuliona taifa la
Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umejipamba kwa sifa ya uanamapinduzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia namna Iran ilivyotoka
mikononi mwa madola ya kibeberu na kubadilika kuwa mfumo wa Kiislamu ambao ni
kigezo kizuri kwa mataifa mengine duniani na kusema kuwa: Suala la kimsingi
hapa ni kwamba, Imam mwanamapinduzi, ameiokoa Iran kutoka katika vinamasi vingi
kama vinamasi vya kuwa tegemezi, ufisadi wa kisiasa, ufisadi wa kimaadili,
kudhalilishwa kimataifa, kuzorota kielimu, kiuchumi na kiteknolojia na kuwa
chini ya ubwana wa Marekani na Uingereza. Aidha amesema: Imam alileta
mabadiliko makubwa sana katika njia ya harakati ya nchi na taifa na Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, Imam Khomeini (quddisa sirruh)
alibadilisha reli ya harakati ya Iran na kuielekeza upande wa malengo makuu
yaani utawala wa dini ya Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa: Utawala wa dini ya
Mwenyezi Mungu una maana ya kuleta uadilifu wa kweli wa kijamii, kung'oa mizizi
ya umaskini na ujinga, kung'oa mizizi ya unyonge na madhara ya kijamii, kujenga
mfumo madhubuti wa thamani na matukufu ya Kiislamu, kudhamini usalama wa
kimwili, kimaadili na kimaanawi, kuleta maendeleo makubwa ya kielimu nchini,
kudhamini heshima na utambulisho wa kitaifa na vile vile nguvu za kimataifa na
kuufanya uwezo wa kila aina ilio nao Iran utumike vilivyo kwa manufaa ya nchi
na kwa sura inayotakiwa.
Aidha amesisitiza kuwa, Imam Khomeini (Rahmatullahi Alayh) kwa baraka za
Mapinduzi ya Kiislamu alifanikiwa kuilekeza Iran upande wa ufanikishaji wa
malengo hayo na kuongeza kuwa: Ijapokuwa ufanikishaji wa malengo hayo
unahitajia muda wa kutosha na jitihada kubwa, lakini ni malengo yanayoweza
kufikiwa na sharti pekee la ufanikishaji wake ni kudumu katika njia ya
Mapinduzi ya Kiislamu na kuwa wanamapinduzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameangalia kwa mamna fulani nakisi
zilizopo katika mchakato wa harakati ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema:
Baada ya kufariki tunia Imam wetu mtukufu (Quddisa Sirruh), tumeweza kupata
maendeleo katika nyakati ambazo tulifanya mambo yetu kimapinduzi, na kila pale
tulipoghafilika na kutofanya mambo yetu kimapinduzi na kijihadi, tumeshindwa na
tumebaki nyuma.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amewaambia wananchi wa mabataka tofauti kwamba:
Inawezekana kufanya mambo kimapinduzi katika njia ya kufanikisha malengo hayo
na iwapo hilo litatendeka, basi bila ya shaka yoyote maendeleo nayo
yatapatikana na inawezekana pia kufanya harakati kwa mbinu nyingine tofauti na
hiyo ya kimapinduzi, lakini wakati huo hatima itakuwa mbaya na taifa la Iran na
Uislamu utapata pigo.
Amesema, Mapinduzi ya Kiislamu ni rasilimali bora na ya kipekee kwa taifa na
nchi na kusisitiza kuwa: Kumetolewa gharama kubwa katika jitihada za
kuyafanikisha Mapinduzi ya Kiislamu na kuyafikisha kwenye natija inayotakiwa,
lakini pembeni mwa gharama hizo, kuna faida na manufaa mengi zaidi
yamepatikana.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia uimara wa Mapinduzi ya Kiislamu baada
ya kupita miaka 37 ya tangu yapate ushindi na kuongeza kuwa: Leo hii hali ya
taifa la Iran inang'ara na iko wazi zaidi ikilinganishwa na huko nyuma na hivi
sasa njia na fursa za kuepuka gharama hizo zimekuwa nyingi zaidi.
Vile vile amesisitiza kuwa: Mapinduzi ya Kiislamu yamepata ushindi kutokana na
azma, irada na imani ya kweli ya wananchi na yamebakia imara hadi leo hii kwa
nguvu hizo za wananchi na yameweza kusimama kidete mbele ya vitisho vya kijeshi
na vikwazo bila ya kutetereka bali yameendelea mbele na harakati yake kiushujaa
na kwa fakhari kubwa na katika siku za usoni pia yataendelea vivyo hivyo na
harakati yake hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria kwamba, kuwa mwanamapinduzi hakuishii tu
katika kipindi cha mapambano ya kufanya mapinduzi hayo na wakati wa Imam
(Rahmatullahi Alayh) na kusema kuwa: Mapinduzi na kutenda mambo kimapinduzi ni
jambo ambalo lipo muda wote, na mapambano ya ufanikishaji wa mapinduzi yalihusu
kipindi maalumu na kwamba watu wote watakaofanya mambo yao kwa mujibu wa
vielelezo vya kimapinduzi ni wanamapinduzi. hivyo hata vijana ambao hawakuwepo
wakati wa harakati za Mapinduzi bali hata Imam hawakumuona, nao ni
wanamapinduzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, fikra ambayo inauweka
uanampinduzi sawa na misimamo mikali na ambayo inawagawa wananchi baina ya
wenye misimamo mikali na wenye misimamo ya wastani, ni fikra potofu na kusisitiza
kuwa: Kuleta fikra kama hizo ni kuwapa zawadi mabeberu na ni kukariri maneno
yale yale ya maadui, hivyo fikra hiyo haipaswi kuruhusiwa kuingia katika
utamaduni na misamiati ya kisiasa nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kosa jingine kuhusiana na
suala la kuwa mwanamapinduzi na kutenda mambo kimapinduzi akisema: Ni kosa
kutarajia kuweko kiwango kimoja cha uanampinduzi kati ya watu wote waliomo
katika harakati na njia ya vielelezo na misimamo ya Mapinduzi, bali jambo la
msingi linalopaswa kuzingatiwa ni vielelezo vya uanamapinduzi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kuna uwezekano mtu akawa na welewa
mzuri kuhusiana na Mapinduzi ya Kiislamu na akafanya harakati zake na
kutekeleza mambo yake kimapinduzi, na inawezekana kukawa na mtu mwingine
akawashindwa kufanya mambo yake kwa uzito wa mtu huyu mwingine lakini wote hao
wawili ni wanamapinduzi na hatuwezi kusema lazima kila mtu anayechunga
vielelezo vya Mapinduzi ya Kiislamu lakini hafanyi harakati kwa uzito wa
wanamapinduzi wengine, yeye si mwanamapinduzi au yuko dhidi ya Mapinduzi;
hatuwezi kusema hivyo.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ameanza kubainisha vigezo vikuu
vya mtu kuwa mwanamapinduzi, kutaja vielelezo vikuu vitano ambavyo ni:
"kushikamana na misingi na thamani kuu za Mapinduzi ya Kiislamu,"
"kuhakikisha kuwa shabaha kuu muda wote ni malengo matukufu (ya Mapinduzi
ya Kiislamu) na kutia hima kubwa ya kufikia kwenye malengo hayo,"
"kushikamana na kupigania vilivyo uhuru wa pande zote wa Iran,"
"kuwa na hisia kali mbele ya adui na kuacha kumfuata" na "kuwa
na taqwa ya kidini na kisiasa."
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi kuhusu kielelezo cha kwanza cha kuwa
mwanamapinduzi yaani "kushikamana na matukufu na usuli za kimsingi"
na kuongeza kuwa: "kuwa na itikadi ya Uislamu sahihi mbele ya Uislamu wa
Kimarekani" ndiyo nukta kuu na muhimu zaidi ya kielelezo hicho.
Vile vile amesema: Uislamu wa Kimarekani una matawi mawili, tawi la Uislamu wa
fikra mgando, na tawi la Uislamu wa kisekulari, na kwamba ubeberu na uistikbari
unaunga mkono aina zote hizo mbili za Uislamu (bandia na usio sahihi).
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, kuwa na itikadi na imani madhubuti ya kwamba
wananchi ndio mhimili mkuu, ni msingi mwingine wa Mapinduzi ya Kiislamu na
kusisitiza kwamba: Katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, msingi mkuu ni rai,
matakwa, malengo na manufaa ya wananchi na kwamba kuwa na imani na itikadi ya
kweli kuhusu mambo hayo ni jambo la dharura la kuwa mwanamapinduzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, maendeleo, mabadiliko
na kujikamilisha ni miongoni mwa matukufu na mambo makuu ya thamani ya
Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kwamba: Mtu mwanamapinduzi anayaamini pia
matukufu hayo na muda wote huwa yuko katika mabadiliko na kupigania kuwa bora
zaidi (kuliko jana yake).
Kuwasaidia wanyonge na matabaka ya watu dhaifu pamoja na kuwatetea na kuwahami
watu wanaodhulumiwa duniani, ni matukufu mengine ambayo Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu ameyaashiria wakati akibainisha kielelezo cha kwanza cha
kuwa mwanamapinduzi yaani kushikamana na usuli za kimsingi za Mapinduzi ya
Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Kama kutakuwepo kushikamana huko ambako Qur'ani inakuita kwa
jina la istiqama, basi harakati za viongozi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu
mbele ya vimbunga vya matukio nayo itakuwa madhubuti na iliyonyooka, vinginevyo
tutakumbwa na kufanya mambo kwa misimamo ya kuchupa mipaka na tutayumba. Aidha
njia na muelekeo wa harakati yetu nao utakuwa unabadilika badilika kwa kila
tukio linalotokea.
Baada ya hapo Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha kielelezo cha pili cha kuwa
mwanamapinduzi yaani kuwa na hima kuu ya kujiletea maendeleo na kufikia kwenye
malengo makuu matukufu na kuongeza kuwa: Tusisite hata mara moja kufuatilia
malengo makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu na ya wananchi na kamwe tusitosheke na
hali tunayokuwa nayo, bali muda wote tufikirie kupiga hatua kubwa zaidi za
maendeleo.
Amesema, katika upande wa pili wa kielelezo hicho kuna uvivu, uhafidhina na
ukataji tamaa na kusisitiza kwamba: Njia ya maendeleo haina mwisho na tunapaswa
muda wote kuendelea na njia hiyo kimapinduzi.
Kielelezo cha tatu cha kuwa mwanamapinduzi kilichozungumziwa na Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba aliyoitoa mbele ya hadhara
kubwa ya watu katika hauli ya 27 cha kukumbuka alipofaniriki dunia Imam
Khomeini (Rahmatullahi Alayh) ni kushikamana na istiklali na uhuru. Kiongozi
Mudhamu amekigawa kielelezo hicho katika vipengee vitatu vya kisiasa,
kiutamaduni na kiuchumi.
Ameongeza kuwa: Maana halisi ya istiklali na uhuru wa kisiasa ni kutotekwa na
wala kuhadaiwa na mbinu mbali mbali zinaotumiwa na adui, na muda wote tuchunge
uhuru wetu wa kisiasa wa ndani ya nchi, wa kieneo na wa kimataifa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria kwa mbali mbinu na hila zinazotumiwa na
maadui hususan Marekani na kusema: Maadui hawaji na vitisho mara zote, bali
baadhi ya wakati huja na tabasamu na vicheko na hata unaweza kuwasikia wakitoa
matamshi kama ya kujipendekeza, kwa mfano watakuandikieni barua na wakwambieni,
njooni tushirikiane kutatua matatizo ya dunia; sasa katika mazingira kama hayo,
mtu anaweza kushawishika na kusema, kama ni hivyo, hilo ni jambo zuri, haya
twendeni tukashirikiane na dola fulani la kibeberu kutatua masuala ya
kimataifa; lakini mtu mwenye fikra kama hizo huwa ameghafilika kwamba, katika
batini yake, adui huwa anatafuta kitu kingine kabisa na hicho
anachokidhihirisha hadharani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mwito wa adui wa
kutaka kushirikiana na sisi kwa ajili ya kutatua masuala ya kimataifa una maana
ya kumsaidia adui katika mchezo na medani aliyoiandaa yeye kwa ajili ya kutatua
masuala maalumu anayoyataka yeye, (si kwamba ana nia njema kweli ya kutatua
matatizo hasa ya dunia).
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mfano mmoja wa wazi wa kuthibitisha suala hilo
nayo ni kadhia ya Syria na kusema: Jambo ambalo lilitufanya tukatae kushiriki
katika muungano wa Kimarekani wa eti kupambana na ugaidi katika kadhia ya Syria
na masuala mengine mfano wake ni kwamba, tulishajua mapema kwamba walikuwa wana
nia ya kutumia nguvu na ushawishi wetu na ushawishi wa nchi nyingine ili
kufanikisha malengo yao maalumu, na si kupambana na ugaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ukumbusho wa kina akisema:
Masuala kama hayo ambayo katika dhahiri yake hayakinzani hata kidogo na
istikbali na uhuru wa nchi yetu, kivitendo yana maana ya kujaza jedwali la kazi
za maadui, na kwa hakika ni kinyume kabisa na istiklali na uhuru wa taifa letu.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi kuhusu tawi la pili la kipengee cha
istiklali na uhuru kwa kutilia mkazo umuhimu usio na mbadala wa uhuru wa
kiutamaduni na kusisitiza kwamba: Kuwa mwanamapinduzi maana yake ni kutumia
mtindo wa maisha ya Kiirani Kiislamu na kujiepusha kikamilifu na kuwaiga
Wamagharibi na mabeberu.
Amesema, zana mpya zinazotumiwa na Wamagharibi katika mawasiliano ya kompyuta
na Intaneti zinatumika kama "mhandisi wa taarifa" na silaha ya
Magharibi ya kudhibiti tamaduni za mataifa mengine. Amesema: Tab'an zana hizo
zinaweza kuwa na faida, lakini inabidi maaadui wapokonywe udhibiti wa zana hizo
na ihakikishwe kuwa mawasiliano ya kompyuta na Intaneti hayawi chombo cha
kujipenyeza adui na kudhibiti utamaduni wa taifa.
Istiklali na uhuru wa kiuchumi kwa maana ya kutoruhusu kumeng'enywa na nguvu za
kimataifa ni nukta nyingine muhimu iliyobainishwa na Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu katika kutolea ufafanuzi kielelezo cha tatu cha kuwa
mwanamapinduzi yaani kushikamana na uhuru wa pande zote wa nchi.
Ameongeza kuwa: Baada ya mazungumzo ya nyuklia, Wamarekani walisema: Muamala wa
nyuklia na Iran lazima upelekee kuingizwa uchumi wa Iran katika jamii ya
kimataifa. Maana ya maneno hayo ni kuwa, Iran ikubali kumezwa na kumeng'enywe
ndani na mpango na mfumo wa mabepari ambao kimsingi ni wa Wazayuni, mfumo ambao
mabepari hao wameutunga duniani kwa ajili ya kudhibiti vyanzo vyote vya fedha
vya dunia.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Katika vikwazo vyao, Wamarekani
walikuwa na nia ya kuufanya kilema uchumi wa Iran, hivi sasa ambapo mazungumzo
yamemalizika na kufikiwa natija, wanataka uchumi wa Iran umeng'enywe na uchumi
wa dunia ambao tayari umeshamezwa na Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kwa kusisitiza kwamba, uchumi wa kimuqawama
ndiyo njia pekee ya kuiwezesha Iran kuwa na uhuru wa kiuchumi na kuongeza kuwa:
Kwa bahati nzuri serikali - kulingana na ripoti ilizotoa - katika mwaka huu wa
Uchumi wa Kimuqawama, Hatua na Vitendo imeanza kuchukua hatua na kama
itaendelea kwa nguvu hizi hizi, bila ya shaka yoyote wananchi wataona matunda
yake mazuri.
Ameongeza kuwa: Katika maamuzi yote makubwa na katika kazi zote ikiwemo
mikataba na nchi nyinginezo, lazima uchumi wa kimuqawama uwe ndio kigezo na
kielelezo kikuu.
Ayatullah Udhma Khamenei amewakosoa watu ambao wanaona kuwa ustawi wa kiuchumi
unaweza kupatikana tu kupitia uwekezaji wa kigeni na kusema: Kuvutia uwekezaji
wa kigeni ni jambo zuri na la lazima, lakini lililo muhimu zaidi ya hilo ni
kuufanya amilifu uwezo mwingi wa kila namna wa ndani ya nchi na kwamba si
sahihi kukiegemeza kila kitu kwenye suala la kuvutia uwekezaji wa kigeni.
Vile vile ametumia mtazamo huo huo kuhusiana na teknolojia mpya na za kisasa
akisisitiza kwa kusema: Kama nchi za kigeni zitatoa teknolojia hizo, si jambo
baya, lakini kama hazikutoa, vijana wetu ambao wameifanya Iran azizi kuwa moja
ya nchi kumi bora katika upande wa teknolojia za Nano, nyuklia na teknolojia
nyinginezo, bila ya shaka yoyote wanao uwezo wa kuidhaminia nchi yao teknolojia
yoyote ile inayohitajika, kama kutakuwa na mipangilio mizuri.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kielelezo
cha nne cha kuwa mwanamapinduzi yaani kuwa na hisia kali mbele ya adui.
Amesisitiza kuwa: Inabidi kuifuatilia kwa kina na kuichunguza kwa undani kila
harakati ya adui na iwe ni kama vile tuko katika medani ya vita ili tuweze
kujua malengo yake na kukabiliana kwa hisia zinazotakiwa na sumu inayoweza
kuwemo ndani ya harakati za adui na kujiwekea kinga madhubuti.
Aidha Ayatullah Udhma Khamenei amewakosoa watu ambao wanafumba macho yao mbele
ya uadui wa kila aina, wa wazi na wa mara kwa mara wa Marekani, na badala yake
wanaona kuwa ni kufanya njama dhidi yao kumzungumzia adui na kusema: Kuukana
uadui mkubwa, wa kuendelea na wa wazi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu
na dhidi ya taifa la Iran ni njama ambayo inafanyika kwa makusudi kwa lengo la
kupungua hisia kali kuhusiana na shetani huyo mkubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, uadui na uhasama wa
Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ndiyo dhati ya Marekani na kuongeza
kwamba: Mfumo wa kibeberu unadhihirisha tabia yake kupitia vita, kuunga mkono
ugaidi, kuwakandamiza wapigania uhuru pamoja na kuwadhulumu, kuwanyanyasa na
kuwakandamiza Wapalestina wanyonge na kwamba mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran hauwezi kunyamaza kimya na kutoguswa na unyanyasaji na ukandamizaji huo.
Kiongozi Muadhamu amekitaja kitendo cha Marekani cha kuisaidia moja kwa moja
nchi inayowashambulia kwa kila aina ya silaha wananchi wanyonge wa Yemen kuwa
ni kushiriki katika mashambulizi na mauaji ya watu wasio na hatia na kusisitiza
kwamba: Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, haiwezekani kunyamazia kimya jinai
kama hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa muhtasari wa namna fulani wa hotuba yake hadi
kufikia hapo akisema kwa kusisitiza kwamba: Mtu yeyote au mrengo wowote
unaofanya kazi kwa ajili ya Uislamu na kwa jina la Uislamu, kama utaitegemea
Marekani, basi mtu na mrengo huo ujue kuwa unafanya kosa kubwa na utapata pigo
la kosa lake hilo.
Amekumbusha pia kuwa: Katika miaka hii hii ya karibuni pia, baadhi ya mirengo
ya Kiislamu katika eneo hili iliamua kushirikiana na Wamarekani kwa madai ya
kutumia akili ya kisiasa na kubadilisha mbinu, lakini hivi sasa mirengo hiyo
inaona madhara ya kumuamini shetani mkubwa.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesema, Waingereza ni maafiriti na makhabithi
zaidi kwa taifa Iran ikilinganishwa na maadui wengine na kuongeza kwamba:
Hakuna hata wakati mmoja ambapo Waingereza wameacha uafiriti na ukhabithi wao
dhidi ya taifa la Iran.
Ameongeza kwamba: Ni katika kuendelea uadui huo wa kila namna ndio maana
taasisi ya kipropaganda ya serikali ya Uingereza katika hauli na kumbukumbu za
mwaka wa kufariki dunia Imam wetu mtukufu ikashadidisha propaganda mbaya dhidi
ya Imam wa taifa la Iran kwa kushirikiana na Wamarekani na kwa kutumia nyaraka
bandia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, utawala fasidi wa
Kizayuni ni miongoni mwa maadui wengine wa taifa la Iran sambamba na Marekani
na Uingereza na kusisitiza kuwa: Inabidi tuwe na hisia kali katika kukabiliana
na maadui na wakati maadui wanapotoa mapendekezo yoyote yale kama vile nakala
za kisiasa na kiuchumi, inabidi tuchukue tahadhari kubwa kwani kama tutakuwa na
hisia kali, jambo hilo litafuatiwa na kutomfuata adui na hiyo ndiyo hiyo
"Jihadi Kubwa."
Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha kielelezo cha mwisho cha kuwa
mwanamapinduzi yaani kuwa na taqwa ya kidini na kisiasa na kusema: Kuwa na
taqwa ya kidini kuna maana ya kufaya jitihada kubwa za kuhakikisha kuwa malengo
yote yaliyoainishwa na yanayotakiwa na Uislamu kwa ajili ya jamii yanafikiwa.
Vile vile amekumbusha kuwa: Katika suala hili hatupaswi kutosheka tu na
mahesabu ya kiakili, kwani kufuatilia kivitendo malengo hayo ni wajibu wa
kidini na kila mtu anayeutoa Uislamu kutoka katika maeneo ya kijamii na
kisiasa, huwa hakuielewa dini tukufu ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi yua Kiislamu Ameongeza kwamba: Kama itapatikana
taqwa ya kidini; taqwa ya kisiasa nayo itapatikana na itaweza kumlinda mtu
kutokana na kuteleza kisiasa na na kumwepusha na kuyumba katika utekelezaji wa
majukumu yake.
Sehemu ya mwisho ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mbele
ya hadhara yenye shauku kubwa ya wananchi wa matabaka mbali mbali
waliokusanyika kutangaza baia na utiifu wao kwa malengo matukufu ya Imam
Khomeini (quddisa sirruh) imehusiana na nasaha kadhaa mnuhimu ambapo nasaha
yake ya kwanza ilikuwa ni kumzingatia Imam Khomeni (Rahmatullahi Alayhi) kuwa
ni ruwaza na kigezo kamili.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuhusu suala hilo kwamba: Katika muongozo na
ramani ya njia tuliyoichora leo hapa, Imam yuko juu ya kila kielelezo
tulichokielezea na inabidi azingatiwe na apewe umuhmu mkubwa na kumfana kuwa ni
kigezo kilicho kamili katika vielelezo vyote hivyo.
Amesema, kutaamali na kuzama muda wote katika kuzingatia sahifa ya Imam
Khomeini na usia wake, na kuwa na ukuruba na mapenzi na maneo na misimamo yake
ndiyo njia ya kumfanya kigezo cha kweli mwanachuoni huyo azizi aliyetangulia
mbele ya Haki na amewausia watu wote na hususan vijana kulipa umuhimu mkubwa
suala hilo.
Nasaha ya pili iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni
kutosahau uzoefu uliopatikana katika mazungumzo ya nyuklia.
Amesisitiza kwamba: Uzoefu huo unatufunza kwamba, hata kama tutaamua kulegeza
misimamo mbele ya Marekani, kamwe Mmarekani hawezi kuachana na njama zake
haribifu dhidi yetu.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia mazungumzo baina ya Iran na kundi la 5+1
na pia mazungumzo pembeni na moja kwa moja baina ya Iran na Marekani kuhusu
kadhia ya nyuklia na kusema: Kwa jitihada za ndugu zetu amilifu, mazungumzo
hayo yameweza kufikia kwenye nukta za pamoja lakini Marekani hadi hivi sasa
inakataa kutekeleza ahadi zake na inaonesha si dola lenye mwamana kwa jinsi
linavyokhalifu ahadi zake.
Ameongeza kuwa: Watu wengi walikuwa wanajua Marekani itafanya hivyo hata kabla
ya mazungumzo ya nyuklia na walitabiri mapema jambo hilo, lakini baadhi ya watu
walikuwa hawalijui hilo, hivyo sasa wanapaswa kuutambua vyema uhakika huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kama itatokezea -
jambo ambalo ni muhali kutokea - tukawa na mazungumzo na Marekani katika suala
lolote vile kama vile haki za binadamu, makombora, ugaidi, Lebanon, Palestina
na jambo lolote lile na tukaamua kulegeza kamba katika misingi na misimamo
yetu, tutambue vyema kuwa Mmarekani kamwe hawezi kulegeza kamba na baada ya
vicheko na tabasamu na maneno haya na yale, Marekani itaendelea kupigania
malengo yake bila ya kujali ahadi zake.
Nasaha za tatu zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni
suala la umoja na mshikamano baina ya serikali na wananchi.
Ameongeza kuwa: Kila mtu katika nyakati tofauti anaweza akawa anavutiwa na
serikali iliyoko madarakani au havutiwi nayo na tab'an jambo hilo halina tatizo
lolote, lakini umoja na mshikamano baina ya wananchi na serikali haupaswi
kuvurugwa kwa hali yoyote ile.
Ayatullah Udhma Khamenei Ameongeza kuwa: Tab'an kuikosoa na kuitaka serikali
ifanye mambo wanayotaka watu ni jambo ambalo halina tatizo na wala suala hilo
halikinzani na umoja na mshikamano, lakini kama ambavyo nimekuwa nikitoa nasaha
hizi kwa kila serikai inayoingia madarakani, hapa narejea tena kusema kwamba
tunapaswa kuwa macho, kusije kukazuka uhasama na chuki bali watu wote wanapaswa
wafanye kazi bega kwa bega katika kukabiliana na vitisho na uadui wa maadui.
Amesisitizia pia haja ya kuweko umoja na mshikamano baina ya Mihimili Mitatu
Mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) na kuongeza kwamba: Umoja
haukinzani hata kidogo na kutekeleza kila mmoja majukumu yake kwa mujibu wa sheria,
lakini hisia binafsi za kimirengo zisiruhusiwe kutia doa mshikamano na kufanya
kazi kwa pamoja mihimili hiyo mitat mikuu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Inabidi kila mtu ajiepushe kutamka
maneno ambayo yataleta mirengo miwili, kambi mbili na chuki na uhasama kati ya
wananchi ili adui aione Iran nzima ni moja iliyoshikamana barabara.
Nasaha za nne zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni
kuyaangalia mapambano na Marekani kuwa ni kama medani ya vita.
Amekumbusha kuwa, tab'an Marekani ndiyo iliyoko katikati ya medani hiyo lakini
uwanja wa mapambano umepanuka na kufika maeneo tofauti na baadhi ya wakati hata
ndani ya Iran. Hivyo inabidi kuwa macho na kukabiliana vilivyo na harakati zote
za matawi ya siri na ya dhahiri ya medani hiyo.
Kuhakikisha mipaka na maadui ni mipana na ni yenye rangi iliyokoza, ni nasaha
za tano zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika
maadhimisho ya miaka ishirini na saba ya kufariki dunia Imam Khomeini (quddisa
sirruh).
Amesisitiza kwamba: Baadhi ya mirengo ya ndani ya Iran inaonekana imeghafilika
na udharura wa jambo hilo na inashindwa kulinda mipaka yao na maadui na kwamba
masafa yao na maadui hao ni dhaifu na yenye rangi hafifu. Amesisitiza kwa
kusema: Kila mmoja anapaswa kuwa macho na kuhakikisha kuwa mistari ya mipaka
yake na maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu na maadui wa Imam na wa taifa la Iran
haiwi na rangi hafifu.
Nasaha za mwisho zilizotolewa na Ayatullah Udhma Khamenei katika maadhimisho
hayo zimehusiana na wananchi na viongozi nchini. Amesema: Kuweni na imani
kamili na nusra ya Mwenyezi Mungu na kuweni na yakini kwamba mustakbali bora ni
wa taifa na wa vijana wa Iran hata kama maadui watachukia.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam
Walmuslimin Hassan Khomeini, mfawidhi wa Haram ya Imam Khomeini (quddisa
sirruh) ametoa hotuba fupi na kusema kwamba Mapinduzi ya Kiislamu ni Mapinduzi
ya Mwenyezi Mungu na ya wananchi. Amesema: Kuwa na uongofu wa Mwenyezi Mungu,
heshima, mapenzi na huruma, umoja, nusra ya Mwenyezi Mungu na nguvu za wananchi
ni katika sifa maalumu za kipekee za harakati adhimu na ya kihistoria ya Imam
Khomeini na kwamba harakati hii imeendelea hadi leo hii kwa namna bora kabisa
kutokana na jitihada kubwa zilizofanyika baada ya kufariki dunia Imam Khomeini
kwa kuchaguliwa mtu anayefaa kabisa kushika nafasi yake.