IQNA

Waziri Mkuu wa India amzawadia Kiongozi Muadhamu nakala ya kale ya Qur'ani

13:09 - May 24, 2016
Habari ID: 3470333
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amemzawadia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei nakala ya kale ya Qur'ani inayonasibishwa na Imam Ali Ali AS.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, akiwa mjini Tehran siku ya Jumatatu 23, Mei, Narendra Modi alikutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kumtunuku nakala nadra ya karne ya 7 Miladia ya Qur'ani Tukufu iliyoandikwa kwa maandishi ya Kufi na inayonasibishwa na Imam Ali AS.

Nakala hiyo ni ya thamani kubwa sana na ilikuwa imehifadhiwa katika maktaba ya Rampur Raza katika jimbo la Uttar Pardesh.

Maandishi ya Kikufi yalianza kutumika karne ya 7 Milladia, huko Kufa nchini Iraq na ni maandishi mashuhuri ya kikaligrafia katika lugha ya Kiarabu.

Waziri Mkuu wa India pia alimzawadia Rais Hassan Rouhani wa Iran nakala ya mashairi ya kale ya Mirza Ghalib kwa lugha ya Kifarsi. Mjumuiko huo wa mashairi ulichapishw akwa mara ya kwanza mwaka 1863, kwa jina la Kulliyat-e-Farsi-e-Ghalib, na una beti 11,000 zilizoandikwa na Ghalib.

Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi aliwasili mjini Tehran Jumapili jioni akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni wa nchi yake, na leo asubuhi amepokewa rasmi na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wakati wa safari hiyo Mkataba wa kimataifa wa kuanzishwa ushoroba wa uchukuzi na usafiri wa Chabahar umetiwa saini kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, India na Afghanistan.

3500551

captcha