IQNA

Vyombo vya Habari vya Saudia na Kiwahabi vinapotosha ukweli kuhusu Mina

10:22 - October 05, 2015
Habari ID: 3381643
Tarehe 24 Septemba katika siku kuu ya Idul Adha wakati zilipoenea habari za kukanyagana na kuzimia baadhi ya Mahujaji huko Mina, hakuna aliyedhani au kuamini kuwa tukio hilo lingegeuka na kuwa maafa makubwa na ya kuogofya ambayo yameshuhudiwa.

Kadiri siku zinavosonga mbele ndivo tunavyozidi kupata maelezo zaidi kuhusu maafa ya kutisha na ya kusikitisha huko Mina. Vyombo mbali mbali vya habari vimetangaza kuwa hadi sasa idadi ya waliopoteza maisha Mina inakadiriwa kuwa elfu tano. Ingawa tukio la kuanguka kreni au winchi na kuuawa mahujaji zaidi ya 100 ni jambo ambalo lilibainisha wazi usimamizi mbovu wa ukoo wa Aal Saudi katika Ibada ya Hija mwaka huu, lakini kujiri tukio la Mina limeibua upeo mpana zaidi wa uzembe wa hali ya juu na kutokuwepo usimamizi unaofaa katika ibada hiyo muhimu. Waislamu kote duniani wameumizwa sana na maafa ya Mina na waliowengi wamebainisha kutoridhishwa kwao na utawala wa Ukoo wa Aal Saud. Wakuu wa Riyadh wamejaribu kufungamanisha maafa ya Hija na masuala ya kisiasa Mashariki ya Kati na hivyo wanatumia vyombo vya habari kuficha na kufunika ukweli kuhusu maafa ya Mina. Katika hatua yao ya awali, Wasaudi na Mawahabbi waliibua mitandao mipya ya kijamii kwa lengo la kuwatuhumu Mahujaji Wairani kuwa eto ndio chanzo kikuu cha maafa hayo kabla ya hapo waliwatuhumu pia Mahujaji wa Kiafrika. Mbinu hiyo ya Mawahabi na Saudi Arabia haikuwashangaza watabiri wengi wa mambo kwani sawa na huko nyuma, kila wakati wakuu wa Saudia wanapojipata njia panda, huituhumu Iran kuwa inahusika na masaibu yao!
Kwa mfano kulianzishwa hashtag # nyingi katika mitandao ya kijamii kwa lengo la kuwatuhumu Wairani kuwa walivuruga nidhamu katika Mina. Wasaudi waliunda hashtag za Kiarabu kama vile #Iran inawaua Mahujaji na # Iran inaua ambapo lengo la upotoshaji huo lilikuwa ni kiulaumu Iran kama mhusika wa maafa ya Mina.
Gazeti la Saudi Arabia la al Sharq al Awsat linalochapishwa London lilidai kuwa maafa ya Mina yalitokana na ukosefu wa utaratibu miongoni mwa Mahujaji Wairani. Gazeti hilo lililokaribu na kasri ya watawala wa Saudia na ambalo ni mashuhuri kwa uhasama wake dhidi ya Iran, katika hatua  ya ajabu lilidadi kuwa eti afisa mmoja Muirani alikiri kuwa Mahujaji Wairani walitumia njia isiyofaa huko Mina na kusababisha maafa katika eneo hilo. Hii ni katika hali ambayo habari hiyo ilikuwa ni urongo mtupu. Lakini upotoshaji huo haukuishia hapo.Televisheni ya Al Arabiya ambayo ina ufungamano wa karibu na ukoo wa Aal Saud katika ripoti kuhusu Wairani waliotoweka Mina ilidai kuwa, mahujaji waliotajwa hawakuwahi kuingia Saudia. Vyombo vya habari vya Saudia aidha vilidai kuwa karibu mahujaji 30 Wairani walitiwa mbaroni kutokana na maafa ya Mina na baada ya muda usio mrefu habari hii nayo ilithibitika kuwa ni urongo mtupu na hata wakuu wa Iran walikanusha habari kama hizo. Televisheni hiyo ya Al Arabiya mnamo Septemba 26 ilitangaza kuwa, duru rasmi za Saudia zimetangaza kuhusu kuendelea uchunguzi kuhusu sababu ya msongamano wa Mahujaji huko Mina. Televisheni hii ya Saudia katika uongo wake mpya, ilimnukulu mtu aliyedaiwa kuwa afisa katika msafara wa Mahujaji wa Wairani akisema kuwa Wairani walienda kinyume ya njia iliyoanishwa wakitekeleza faradhi ya Ramy al-Jamarat  na hivyo kusababisha maafa katika eneo hili.
Katika upande mwingine gazeti la Wall Street Journal la Marekani lilichukua muelekeo mwingine. Katika ripoti yake, gazeti hilo lilisema hakuna uongozi unaostahiki katika wizara ya Hija ya Saudia ambayo ni mwandalizi mkuu wa ibada ya Hija. Gazeti hilo lilifichua kuwa baadhi ya maafisa waandamizi wa wizara hiyo walijiuzulu kutokana na hitilafu zilizokuwepo. Kwa mujibu wa gazeti hilo, maafisa waliojiuzulu walikuwa na uzoefu wa makumi ya miaka na walkuwa na majukumu ya kusimamia harakati za mahujaji kutoka Mina hadi Ramy al-Jamarat.
Mwandishi wa zamani wa gazeti la Wall Street Journal, Bi. Asra Quratulain Nomani, ambaye aliwahi kuhiji aliandika hivi kufuatia maafa ya Mina: "Nina  yakini kuwa hivi sasa ni wakati bora zaidi kwa Waislamu kuisusia serikali ya Saudi Arabia ambayo imejitwika jukumu la msimamizi wa Haramein au maeneo mawili matakatifu ya Makka na Madina na kwa msingi huo watawala hao wa Saudia wamejiweka katika hadhi  ya aina fulani ya kinga ya kimaadili." Mwandishi huyo Mmarekani Mwislamu mwenye asili ya India aliandelea kuandika hivi kuhusu kususiwa na kushinikizwa utawala wa Aal Saud: "Nafuatilia nukta kadhaa kuhusu maafa ya Mina ambapo wakuu wa Saudia wameonekana kuwa ni wenye kiburi na moyo mgumu huku wakiwalaumu Mahujaji  na hasa kutoka nchi za Afrika kuwa ndio waliohusika na maafa hayo."
Bi. Nomani katika safari yake ya hija anasema alishuhudia kwa karibu usimamizi mbovu wa wakuu wa Saudia katika masuala ya Hija na kuandika hivi: "Nchi hii ambayo inapokea pato la mabilioni ya dola kutoka kwa Mahujaji, inakiuka vibaya sana haki za binadamu. Hii ni nchi ambayo imepelekea kuibuka maafa ya kusikitisha katika siku za Hija. Hii ni nchi ambayo imefasiri vibaya Uislamu na kueneza kote duniani Uislamu wa utumiaji mabavu (kama wanavofanya magaidi wa ISIS). Hivi sasa baada ya maafa ya Mina serikali ya Saudia inajaribu kuibua kimya katika vyombo vya habari ili kunusuru itibari yake iliyobakia."
Televisheni ya CNN ya Marekani, ambayo inafuata kibubusa sera za Saudi Arabia, ilidai kuwa mahujaji waligongana wakati wakitoka sehemu mbili mkabala jambo ambalo liliibua maafa ya Mina na kwamba eti wengi walikuwa na haraka ya kuelekea Rami al Jamarat asubuhi mapema. Aidha CNN iliendelea kudai kuwa eti msongamano huo ulisababishwa na joto kali. Kanali hiyo ya Marekani haikutoa maelezo yoyote kuhusu taswira zilizoonyesha kutojali maafisa wa Saudia na namna walivyobakia kuwa watazamaji huku mahujaji wakipoteza maisha.
Kashfa ya baadhi ya vyombo vya habari kushirikiana na utawala wa Aal Saud kuficha ukweli kuhusu maafa ya Mina haiishii katika tukio hilo tu. Huko nyuma kuliwahi kufichuka nyaraka za namna utawala wa Saudia ulivyotumia kiasi kikubwa cha fedha kuvinyamazisha vyombo vya habari vya kimataifa au kuvilazimu vipayuke sera za watawala wa ufalme huo. Tovuti ya Wikileaks mwezi Juni ilifichua nyaraka zilizoonyesha kuwa utawala wa Saudia umetumia kiasi kikubwa cha fedha kuvihonga vyombo vya habari katika nchi nyingi za Kiarabu. Tovuti hiyo pia ilifichua namna Saudia ilivyokata misaada yake kwa baadhi ya vyombo vya habari ambayvo vilionekana kutotii matakwa yake. Mfano moja ni televisheni ya LBC ya Lebanon iliyokumbwa na hali kama hivyo mwaka 2012. Balozi wa Saudia Beirut alipendekeza kuondolewa televisheni hiyo katika satalaiti ya Arabsat kutokana na kuwa ilikataa kutii sera za ukoo wa Aal Saudi. Aidha nyaraka hizo zilionyesha namna ilivyopendekezwa mhariri mkuu wa gazeti mashuhuri la Lebanon la Al Safir aalikwe Saudia ili gazeti hilo liabdilishe sera zake zipendelee Riyadh.
Mohammad al Qasimi mwandishi masuhuri wa Morocco katika makala yake ya uchambuzi ameandika hivi: "Televisheni za nchi za Kiarabu zimegawanyika katika kambi mbili. Ya kwanza ni kambi ya televisheni zinazotangaza maswala yanayowahusu wananchi na kuunga mkono wanaodhulumiwa. Kambi ya pili ni ile inayoakisi na kufuata sera za Marekani na nchi za Ulaya kwa lengo la kudhoofisha mamapmbano na harakati za kupigania ukombozi Palestina, Lebanon na Iraq. Misdaki na mfano wa wazi wzi wa mgawanyiko huu ni katika televisheni za Kiarabu za Al Alam na Al Arabiya. Kwa hakika ni aibu kubwa kuwa Televisheni ya Al Arabiya ina jina kama hilo lakini inajidhalilisha na kunyamazia kimya mambo mengi. Televisheni hii katika kutekekeleza majukumu yake ya kuaibisha, inapotosha fikra za umma hatua kwa hatua sambamba na kuharibu taswira ya viongozi maarufu wa ulimwengu wa Kiislamu."
Nassir Angawi   mwandishi Msaudi katika makala aliyoiandika katika tovuti ya "Markaz Haramein" mwaka 2009 alisema moja ya sababu ya uhasma wa Iran na Saudia ni kuhusu vyombo vya habari. Aliandika hivi: 'Kuhusu uhusiano na Iran, Saudi Arabia haitaki kuwa na uhusiano mzuri na badala yake inataka mkabala na uhasama na Iran. Kila wakati tunaposhuhudia kupungua uhasama ni kwa sababu ya hatua chanya zilizochukuliwa na Iran. Saudia inasisitiza kuwepo misimamo mikali ya nchi za Kiarabu dhidi ya Iran. Vyombo vya habari vya Saudia vinaongoza katika hujuma ya kihabari dhidi ya Iran." Mwandishi hiyo anabainisha sababu ya uhasama wa Saudia dhidi ya Iran kwa kusema: "Saudia imepoteza ushawishi wake katika eneo. Wasaudi hawawezi kushindana kwa njia salama na ya kawaida na kwa msingi huo wanaanzisha vita  katika vyombo vya habari kufidia hasara walizopata.
Ni jambo la kusikitisha kuwa katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, zaidi ya Mahujaji 7,00 wamepoteza maisha Makka katika matukio ambayo yangeweza kuepukika. Ili kukwepa lawama, watawala wa Saudia wamekuwa wakitumia propaganda za vyombo vya habari kuwalaumu mahujaji kuwa ndio chanzo kikuu cha maafa. Kukaririwa mara kadhaa maafa katika ibada ya Hija ni dalili ya wazi kuwa utawala wa Aal Saud hauwezi na wala haustahiki kupewa jukumu zito la kusimamia maeneo mawili matakatifu ya Kiislamu ya Makka na Madina. Pengine njia pekee ya kuuokoa umma wa Kislamu kutokana na mgogoro wa usimamizi mbovu wa Haramein ni kuundwa baraza la nchi za Kiislamu ili kusimamia maeneo hayo matakatifu ambayo ni ya Waislamu wote na hivyo ni haki yao kuyasimamia.

3370675

captcha