IQNA

Al Azhar ya Misri yalaani mauaji ya kigaidi huko Garissa Kenya

18:25 - April 06, 2015
Habari ID: 3099045
Jumuiya na taasisi mbalimbali za kimataifa na kiraia zimeendelea kulaani mauaji yaliyofanywa Alkhamisi iliyopita na kundi la kigaidi la al Shabab dhidi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya.

Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al Azhar nchini Misri kimelaani vikali mauaji yaliyofanywa na kundi  hilo la kigaidi ambayo yamechukua roho za watu wasio na hatia huko mashariki mwa Kenya.

Taarifa iliyotolewa na taasisi hiyo ya Kiislamu imesema kuwa Al Azhar inalaani vikali ugaidi wa kundi la al Shabab la Somalia na mauaji ya watu 150 yaliyofanywa na kundi hilo katika Chuo Kikuu cha Garissa.

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya umesema kuwa unaunga mkono mapambano ya watu wa Kenya dhidi ya ugaidi.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Bi Federica Mogherini amelaani mashambulizi yaliyofanywa na kundi la al Shabab dhidi ya Chuo Kikuu cha Garissa na kusema kuwa kwa mara nyingine tena Wakenya wamekuwa wahanga wa misimamo mikali na makundi ya kikatili.

Mogherini amelaani vikali shambulizi hilo na kusema Umoja wa Ulaya unaunga mkono mapambano ya Wakenya dhidi ya ugaidi.

Alkhamisi iliyopita wanachama wa kundi la kigaidi la al Shabab walivamia mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Garissa huko mashariki mwa Kenya na kuua watu 148 wengi wao wakiwa wanafunzi.

Mauaji hayo yamelaaniwa vikali na jumuiya na taasisi za kimataifa. Viongozi wa Kiislamu nchini Kenya wamelaani shambulizi la kigaidi dhidi ya wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Garissa na kusema kuwa kitendo hicho hakina mfungamano wowote na dini tukufu ya Uislamu.../mh

3090535

Kishikizo: kenya azhar garissa gaidi
captcha