IQNA

Mtazamo

Kuinyima UNRWA misaada ni mbinu mpya ya Israel, Magharibi kutekeleza mauaji ya kimbari Gaza

14:01 - February 01, 2024
Habari ID: 3478288
IQNA- Ikiwa imepita miezi minne ya mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza, utawala huo umeshindwa kufikia lengo la kuangamiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, na pia haujaweza kuvunja azma na irada ya wakazi wa eneo hilo. Hivyo ili kujaribu kufidia kufeli huko, Wazayuni wakishirikiana na baadhi ya waitifaki wao wa Magharibi, sasa wanalenga kusambaratisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA.

Siku moja baada ya Wazayuni kudai kwamba wafanyakazi kadhaa wa UNRWA walihusika katika matukio ya Oktoba 7, Marekani, Uingereza, Ujerumani na nchi nyingine kadhaa za Magharibi mara moja zilitangaza kusimamisha misaada yao ya kifedha kwa shirika hilo. Kusitisha msaada kwa UNRWA kuna maana ya kusitisha utoaji wa msaada wa chakula na huduma za afya kwa malaki ya wakimbizi wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza wakati huu wa hali ngumu ambapo utawala wa haramu wa Israel umezidisha mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa eneo hilo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina "UNRWA", ambalo historia yake inaanzia mwaka 1949, ambalo kwa sasa lina wafanyakazi wapatao elfu 30, hutoa huduma kwa zaidi ya Wapalestina milioni 5 ndani na nje ya ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, hususan eneo lenye vita la Gaza. 
Ijumaa iliyopita, utawala wa Kizayuni wa Israel ulidai kuwa wafanyakazi kadhaa wa UNRWA walishiriki katika Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023.

Wakati madai hayo yakiwa bado hayajathibitishwa, nchi 6  za Magharibi, zikiwemo Marekani, Canada, Australia, Finland, Uingereza na Italia, zilichukua hatua ya kukurupuka na kutangaza kwamba, kutokana na ukiukwaji unaofanywa na UNRWA, zinasitisha misaada kwa taasisi hiyo.

Siku moja baada ya kauli hii na katika mwendelezo wa misimamo iliyoratibiwa ya nchi za Magharibi dhidi ya UNRWA, Ujerumani, Scotland na Ufaransa nazo ziliunga mkono hatua hiyo ya kusimamisha mara moja misaada yao kwa UNRWA, na sasa ni washirika katika mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Ni wazi kuwa Wazayuni wameanzisha kampeni dhidi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, kwa uratibu wa vyombo vya habari na vya kidiplomasia vya Magharibi.

Sababu za hatua dhidi ya UNRWA

Swali la linaloulizwa ni kuwa, kwa nini Wazayuni wanafuata mchakato wa kusimamisha shughuli za mashirika ya misaada ya kibinadamu huko Gaza wakati na kipindi hiki? Kuna sababu fiche ambazo zimepelekea kuanzishwa propaganda dhidi ya UNRWA katika vyombo vya habari vya Magharibi.

Baadhi ya wachunguzi wa mambo wanaamini kuwa, Israel imeamua kuibua tuhuma zisizo na msingi dhidi ya wafanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), sambamba na kuzidisha mashinikizo kwa Wapalestina wanaoishi Gaza na harakati ya Hamas, ili kwa njia hiyo kufidia kipigo cha kidiplomasia katika kesi ya malalamiko ya Afrika Kusini dhidi ya utawala huo mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki, (ICJ) huko The Hague.

Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, kufuatia hatua iliyochukuliwa na serikali ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, Wazayuni wamekuwa wakilaaniwa kila upande katika uga wa kimataifa. Ni wazi kuwa uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki dhidi ya Israel umetoa kipigo kikubwa kwa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake. Kufuatia hujumu ya ICJ, waliowengi duniani hawana shaka kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

 Kwa hakika Israel kwa ushirikiano na uratibu wa waungaji mkono wake katika nchi za Magharibi, inajaribu kuibua mtiririko wa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya UNRWA ili kuharibu hadhi ya taasisi nyingine zilizo chini ya Umoja wa Mataifa ikiwemo Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ.

Kushindwa kijeshi

Uamuzi wa waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni wa kusimamisha misaada kwa UNRWA katika hali ambayo mamia ya maelfu ya Wapalestina hususan wakazi wa Gaza, wako chini ya mashambulizi makali zaidi ya anga na nchi kavu ya utawala huo ghasibu, unaonyesha kushindwa juhudi za kijeshi za utawala huo na kuimarika irada ya wananchi na wapigania uhuru wa Palestina.

Ni wazi kuwa, Israel, kwa hima ya madola ya Magharibi hasa Marekani, imeamua kuendeleza sera yake ya mauaji ya kimbari huko Gaza, mara hii kwa kutumia silaha ya njaa na kuzuia huduma za afya na matibabu.

Ahabu ya pamoja

Baadhi ya nchi za Magharibi, zimeunga mkono ombi la utawala wa Kizayuni la kusitisha misaada kwa UNRWA kwa kisingizio cha kuhusika kwa baadhi ya wafanyakazi wake katika  operesheni ya tarehe 7 Oktoba, katika hali ambayo katika cha miezi mitatu iliyopita, utawala katili wa Israel umeua wafanyakazi 150 wa UNRWA huko Gaza. Ni nadra sana idadi kama hiyo ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kuuawa katika kipindi kifupi lakini nchi za Magharibi zimenyamazia kimya jinai hiyo.

Hata kama madai kuhusu vitendo vya wafanyakazi wachache wa UNRWA yatakuwa ya kweli, juhudi za makumi ya maelfu ya wafanyakazi wengine wa UNRWA na huduma yao kwa mamia ya maelfu ya watu hazipaswi kupuuzwa na kukabiliwa na 'adhabu ya pamoja'.

Kwa maneno hayo tunaweza kuhitimisha kuwa, uamuzi huu wa nchi zinazouunga mkono utawala wa Kizayuni una maana ya kuwaadhibu mamilioni ya Wapalestina hususan wakati huu wa maafa ya kibinadamu huko Gaza. Hatua hiyo ya nchi za Magharibi dhidi ya UNRWA ina maana ya kushiriki moja kwa moja katika mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

3487044

Habari zinazohusiana
captcha