IQNA

Kuundwa kamati ya kuchunguza jinai za Wazayuni huko Gaza

9:57 - November 13, 2014
Habari ID: 1472788
Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa, kumeundwa kamati ya uchunguzi kuhusiana na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel katika ukanda wa Gaza.

Wakati wa vita vya siku 51 huko Gaza, takribani Wapalestina elfu mbili waliuawa na wengine elfu kumi na moja kujeruhiwa. Nukta ya kutaamali katika vita vya Gaza ni hii kwamba, katika vita hivyo, raia ndio waliokuwa walengwa wakuu wa mashambulio ya kinyama ya Israel. Fauka ya hayo, mauaji yote hayo yalifanyika huku nchi za Kiarabu zikiwa zimekaa kimya.  Nchi za Kiarabu ambazo zinaitambua Palestina kuwa ni sehemu ya ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu, zilikuwa watazamaji tu katika vita hivyo. Si hayo tu, hata Umoja wa Mataifa nao haukuchukua hatua yoyote ya maana kuzuia mashambulio ya kinyama ya utawala haramu wa Israel. Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na wananchi wa Palestina waliingia katika medani ya vita katika mazingira haya. Makombora ya muqawama wa Palestina yaliyokuwa yakivurumishwa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu yaliwanyima usingizi na hata utulivu wa kiroho walowezi wa Kiyahudi. Hata viongozi wa Israel nao waliingiwa na wahka na wasi wasi mkubwa kutokana na makombora hayo ya Wapalestina. Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, licha ya kuwa vita hivyo havikuwa na mlingano, lakini muqawama wa Palestina uliibuka na ushindi. Baadhi ya duru za kisiasa zinaamini kwamba, hatua ya Umoja wa Mataifa ya kuchunguza jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza kupitia kamati maalumu, inaweza kuhesabiwa kuwa changamoto kubwa kwa viongozi watenda jinai wa Tel Aviv. Kwa sasa Israel ndio utawala unaochukiwa zaidi katika Mashariki ya Kati huku ukosoaji dhidi ya utawala huo kimataifa ukiwa unaongezeka kila leo. Katika kipindi cha zaidi ya miongo sita tangu kuasisiwa utawala wa bandia wa Israel katika Mashariki ya Kati, hakuna jinai ambayo haijafanywa na utawala huo katili dhidi ya wananchi wa Palestina. Kuharibu ardhi za kilimo, kubomoa nyumba za Wapalestina na kuwauwa shakhsia wa Kipalestina ni upande mmoja tu wa siasa za Israel zilizojengeka juu ya misingi ya utumiaji mabavu, ukandamizaji na mauaji dhidi ya Wapalestina. Kuwaondoa kabisa Wapalestina katika maeneo unayoyakalia kwa mabavu ni miongoni mwa hatua ambazo zimekuwa zikifuatiliwa na utawala wa Kizayuni katika miongo yote hii. Katika vita vya siku 51 vilivyoanzishwa na Israel huko Gaza, nyumba elfu kumi na mia sita zilibomolewa, hospitali 23 ziliharibiwa kabisa, zaidi ya shule mia na themanini na misikiti mia moja na thelathini na mbili nayo iliharibiwa kabisa. Jinai za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza zilikuwa kubwa mno kiasi kwamba, hata baadhi ya waungaji mkono wake walishindwa kunyamaza kimya na wakajitokeza na kuukosoa utawala huo. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hatua ya Umoja wa Mataifa ya kutaka kuchunguza jinai za Israel kupitia timu maalumu ni jambo linaloonesha unyeti uliopo hivi sasa kuhusiana na hujuma za Wazayuni huko Palestina. Hapana shaka kuwa, kama mashinikizo ya kimataifa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel yatashadidishwa, jambo hilo linaweza kuwa wenzo bora kabisa wa kukabiliana na utawala huo ghasibu unaotenda jinai kila uchao huko Palestina.../mh

1472397

Habari zinazohusiana
captcha