IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

'Shughuli za nyuklia za Iran haziwezi kusimamishwa'

14:16 - April 10, 2014
Habari ID: 1392769
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema shughuli za ustawi na utafiti wa nyuklia Iran kamwe hazitasimamishwa.

Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo jana Jumatano ambayo ilisadifiana na Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia nchini Iran ameonana na mkuu na maafisa wa ngazi za juu pamoja na wataalamu bingwa, mawaria na wasomi wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran na kusema kuwa, moja ya mafanikio muhimu zaidi ya maendeleo ya nyuklia ya Iran ni kutia nguvu moyo wa kujiamini kukubwa kitaifa nchini na kuandaa mazingira ya kupatikana maendeleo ya kielimu katika sekta nyinginezo.
Vile vile ameashiria mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1 na kusisitiza kuwa: Kukubali kufanya mazungumzo hayo kulikuwa na lengo la kuvunja anga ya chuki ya kambi ya kibeberu dhidi ya Iran na inabidi mazungumzo hayo yaendelee lakini watu wote wanapaswa kutambua kuwa, pamoja na kuendelea na mazungumzo hayo, lakini shughuli za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uwanja wa kufanya utafiti na kujiletea ustawi wa nyuklia hazitosita wala kusimama kwa hali yoyote ile na hakuna mafanikio yoyote ya nyuklia yatakayosimamishwa kama ambavyo uhusiano wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA na Iran nao inabidi uwe wa kawaida tu na usiingizwe mambo ya nyongeza.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya tarehe 20 Farvardin (Aprili 9) Siku ya Taifa ya Nishati ya Nyuklia nchini Iran. Aidha ameitaja hatua ya kuingizwa siku hiyo katika kalenda rasmi ya Iran kuwa ni matunda ya juhudi na jitihada za wasomi na wataalamu wenye misimamo thabiti na amilifu katika masuala ya nyuklia.
Vile vile amewakumbuka kwa wema na kuwashukuru mashahidi na watu wote waliojitolea kwa hali na mali katika kufanikisha masuala ya nyuklia nchini Iran na kuongeza kuwa: Ijapokuwa utaalamu wa nyuklia unatumika katika kuzalisha nishati na vile vile katika masuala ya ufundi na viwanda, afya na matibabu, kilimo na usalama wa chakula na biashara, lakini faida muhimu zaidi ya utaalamu wa nyuklia nchini Iran ni kuwa utaalamu huo umeimarisha na kutia nguvu uwezo wa kujiamini kitaifa nchini Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria mbinu kubwa inayotumiwa na wakoloni, iwe ni wakoloni wa zamani au wakoloni wa hivi sasa ya kujaribu kuonesha na kuwakubalisha watu duniani waamini kuwa mustakbali wao hauwezi kubadilika na kwamba yale mataifa yaliyo dhaifu siku zote yataendelea kuwa chini ya udhibiti wa madola hayo ya kibeberu na kuongeza kuwa: Mbinu yoyote ile itakayopelekea kuvunja njama hizo, bila ya shaka yoyote itakuwa ni nguzo madhubuti na jambo la kimsingi kwa ajili ya ustawi wa kitaifa na wa kuliwezesha taifa husika kufanya harakati adhimu za kujianishia mustakbali wake.
Vile vile ameashiria njama za kambi ya kiistikbari ya kujaribu kuizuia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupiga hatua za kimaendeleo tangu katika miaka ya awali kabisa ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kujaribu kuwaonesha walimwengu kuwa Iran ni nchi iliyobaki nyuma kimaendeleo na dhaifu na kuongeza kuwa: Moja ya mipango mingine ya kambi ya kimataifa ya kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu ni njama kubwa zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na kambi hiyo za kutoa athari hasi kwa siasa kuu za Iran na kuishinda irada na nia ya viongozi wa kisiasa wa nchi yetu lakini kambi ya kibeberu imeshindwa kufanikisha njama zake hizo hadi hivi sasa na katika siku za usoni pia itashindwa tu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, hila na njama nyingine zinazofanywa na kambi ya waistikbari katika kukabiliana na Mfumo wa Kiislamu nchini Iran ni kuanzisha anga ya kimataifa ya kupinga Jamhuri ya Kiislamu kwa kueneza uvumi wa kijinga kwa walimwengu.
Amesema: Kadhia ya nyuklia, ni moja ya mifano ya wazi ya masuala ambayo mabeberu wanafanya njama ya kuyatumia kueneza uongo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ulimwenguni na kuandaa anga ya kuwatia woga walimwengu kuhusu Mfumo wa Kiislamu wa nchini Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesema: Hata hivi sasa pia ambapo kwa mujibu wa kisheria, kiakili na kisiasa watu wote duniani wamepata yakini kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina nia kabisa ya kumiliki silaha za nyuklia, lakini viongozi wa Marekani mara kwa mara utawasikia wanazusha suala hilo na kurejea madai yao yale yale ya kila siku ya kudai kwamba eti Iran ina nia ya kumiliki silaha za nyuklia wakati hata wao wenyewe wanajua vyema kuwa kutomiliki silaha za nyuklia ni siasa zisizobadilka kabisa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ameongeza kwamba: Lengo la viongozi hao (wa Marekani na mabeberu wengine) ni kwamba wanataka kutumia kisingizio hicho kuifanya anga ya kimataifa kuwa dhidi ya Iran na ni kwa sababu hiyo ndio maana ilikubaliwa kwa mujibu wa mpango mpya wa serikali ya Iran kufanyika mazungumzo ya nyuklia ili kuvunja anga hiyo ya kimataifa na kuupokonya upande wa pili udhibiti wa suala hilo na kuzidi kuwabainishia walimwengu ukweli na uhakika wa kadhia ya nyuklia ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwa kusema: Tab'an mazungumzo hayo hayana maana kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran italegeza kamba walau kidogo katika harakati yake ya kielimu kuhusu teknolojia ya nyuklia.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Maendeleo na mafanikio ya nyuklia yaliyopatikana hadi hivi sasa nchini Iran kwa hakika yanatoa bishara njema kwa taifa la Iran kwamba linaweza kupiga hatua kubwa katika njia ya kufikia vilele vya juu vya maendeleo ya kielimu na kiteknolojia, hivyo harakati hii ya kielimu ya nyuklia kamwe haitasimama na bali kamwe haitopunguza kasi yake.
Vile vile amesema, timu ya Iran inayoshiriki katika mazungumzo hiyo inapaswa kushinikiza juu ya haki na wajibu wa kuendelea utafiti na ustawi wa kinyuklia nchini Iran na kuongeza kuwa: Mafanikio yoyote yale ya nyuklia ya Iran hayawezi kamwe kusimamishwa na hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kuyafanyia muamala mafanikio hayo na hakuna mtu yeyote atakayefanya hivyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakhutubu wasomi, mawaria na wataalamu wa nyuklia wa Iran akisema: Njia mliyoianza inabidi iendelea kwa nguvu zote kwani Iran inahitajia kuwa na maendeleo ya kielimu na kiteknolojia hususan teknolojia ya nyuklia.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Iwapo harakati ya kielimu katika teknoljia ya nyuklia itaendelea kwa nguvu na kwa uzito mkubwa, basi bila ya shaka yoyote kutashuhudiwa pia kuongezeka kasi ya maendeleo ya kiteknolojia katika masuala mengineyo hivyo hakuna njia wala namna yoyote ile ya kuifanya harakati yetu ya maendeleo ya kielimu ya nyuklia kusimama au kupungua kasi yake.
Aidha amesema ni jambo linalowezekana kupigwa hatua kubwa za kimaendeleo katika teknolojia kutokana na vipaji walivyo navyo vijana wa Iran na kuongeza kuwa, katika uwanja wowote ambao utakuwa na misingi na miundombinu inayotakiwa, wataalamu na wasomi vijana wa nchi yetu wanaweza kufanya kazi kubwa ndani yake na kufanya maajabu katika nyuga hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amegusia mazungumzo ya miaka michache iliyopita baina ya Iran na nchi nyingine mbili kuhusiana na fueli nyuklia ya kinu cha utafiti wa nyuklia cha Tehran na kusema: Wakati huo kulipatikana fomyula fulani kwa ajili ya kuandaa fueli nyuklia lakini tofauti na walivyowaambia marafiki zao katika eneo hili na katika moja ya nchi za Amerika ya Latini na baadhi ya viongozi humu nchini nao wakawaamini, Wamarekani walikwamisha mchakato huo na walidhani kuwa sasa Iran wameibana kikamilifu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Mimi wakati huo na tangu mwanzoni kabisa mwa jambo hilo nilisema kuwa Marekani haina nia ya kulitatua suala hili na baadaye watu wote walishuhudia kwa macho yao namna ambavyo Wamarekani walikwamisha jambo hilo na jinsi walivyozuia utekelezaji wake baada ya kufikiwa makubaliano kupitia mazungumzo yaliyofanyika kati ya Iran na nchi hizo mbili.
Vile vile ameashiria nia na moyo wa hali ya juu walio nao wasomi na wanasayansi vijana wa nyuklia wa Iran na kusema: Katika wakati huo na wakati wasomi na wataalamu wetu walipotangaza kuwa wanao uwezo wa kujizalishia wenyewe sahani za fueli nyuklia kwa ajili ya kitu cha utafiti wa nyuklia cha Tehran, Wamagharibi hawakuamini hata kidogo bali hata walifanya istihzai lakini vijana wetu wasomi walifanikisha jambo hilo chini ya muda uliotabiriwa na kuwaweka vinywa wazi maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameyataja maendeleo ya kiulinzi na kibioteknolojia ya Iran kuwa ni moja ya mifano mingine ya uwezo na vipaji vikubwa walivyo navyo vijana wa Iran na kusisitiza kuwa: Moyo huu inabidi ulindwe na uimarishwe katika majimui ya taasisi na nishati ya atomiki na kwamba taasisi hiyo inapaswa iwe na taasubu kuhusiana na mafanikio yake ya kielimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema, viongozi nchini Iran nao wanapaswa kuwa na taasubu kuhusiana na maendeleo ya nyuklia ya nchi yao na amegusia baadhi ya masuala ya ndani ya nchi kuhusu madai na mawazo ya kuweko gharama kubwa za kadhia ya nyuklia akisema: Kuwa na mawazo kama hayo kuhusiana na kadhia ya nyuklia ni kuwa na fikra finyu zisizoangalia mbali kwani kunawafanya baadhi ya watu wadhani kuwa gharama za maendeleo ya nyuklia ya Iran ni mashinikizo na vikwazo wakati ukweli wa mambo ni kuwa hata kabla ya kujitokeza kadhia ya nyuklia vikwazo na mashinikizo dhidi ya Iran yalikuwepo na kulitumika sababu na visingizio vingine kuweka mashinikizo na vikwazo hivyo.
Ameongeza kuwa: Wakati huo ambapo suala la nyuklia halikuwepo, mahakama moja ya Magharibi ilitoa hukumu dhidi ya Rais wa Iran akiwa hayupo mahakamani ambapo tab'an hivi sasa hawathubutu tena kufanya kitu kama hicho kutokana na nguvu za kitaifa ilizo nazo Iran sasa hivi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, vikwazo na mashinikizo hayatokani na kadhia ya nyuuklia bali mabeberu wa dunia wana uadui na sifa ya kuwa huru taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu ambayo imesimama juu ya msingi wa imani na itikadi za dini tukufu ya Kiislamu na vile vile hauwezi kulegeza kamba mbele ya mabeberu hao katika misimamo yake ya kupigania mustakbali bora wa taifa hili.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea kusisitiza kwa kusema: Hivyo kujitokeza mtu na kudai kuwa vikwazo na mashinikizo ndizo gharama za maendeleo ya nyuklia ya Iran, mtu huyo hatakuwa amesema kweli kwani hata kama suala la nyuklia lisingelikuwepo, maadui wa Iran wangelitumia kisingizio kingine kuiwekea mashinikizo na vikwazo Iran kama ambavyo hata hivi sasa ambapo mazungumzo ya nyuklia yanaendelea, tayari Wamarekani wameanza kuzungumzia kadhia ya haki za binadamu.
Amesema hata kama kadhia ya haki za binadamu nayo itatauliwa, maadui hao watatafuta kisingizio kingine, hivyo njia pekee ni kwamba maendeleo yetu tuenedelee kuyapigania na kuyalinda kwa nguvu zote na tusilegeze kamba hata kidogo mbele ya mashinikizo ya maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza pia kuwa inabidi mazungumzo yaendelee na fremu yake nayo iwe ni nyuklia.
Vile vile amesema: Timu ya mazungumzo ya nchi yetu haipaswi kukubaliana na mashinikizo na utenzaji nguvu wa aina yoyote ile wa upande wa pili na kwamba uhusiano wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA na Iran nao unapaswa uwe wa kawaida tu na usiongezwe kitu chochote cha ziada.
Ayatullah Udhma Khamenei ameyataja mafanikio na maendelo ya wasomi, wanasayansi na wataalamu wa nyuklia wa Iran kuwa ni matunda ya kumwamini Mwenyezi Mungu, kutekeleza vilivyo majukumu na kuwa na imani na njia sahihi akiongeza kwamba: Tumeshuhudia kwa macho yetu muongozo wa Mwenyuezi Mungu na misaada yake mikubwa kwetu.
Vile vile amewaombea dua viongozi wa hivi sasa wa masuala ya nyuklia ili wapate nguvu za kuendelea vizuri na jitihada za kuongeza maendeleo katika kadhia ya nyuklia nchini akiwemo Dk Salehi, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran kama ambavyo amewashukuru pia viongozi waliopita wa taasisi hiyo kwa idili zao kubwa walizozifanya katika jitihada za kuliletea taifa mafanikio na maendeleo makubwa ya kinyuklia.
Kabla yua hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Dk Salehi, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran ametoa ripoti fupi kuhusiana na kazi na hatua zilizochukuliwa na taasisi hiyo pamoja na mipango yake ya baadaye kama ambayo ametaja pia baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya nyuklia nchini Iran.
Amesema, jukumu na kazi kubwa na ya kiistratijia ya taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran ni kudhamini nishati inayohitajika nchini sambamba na kutimiza mahitaji mengineyo katika sekta tofauti kama za afya na matibabu, viwanda na kilimo na kuongeza kuwa: Kukamilisha mfumo wa fueli nyuklia ni moja na nukta bora zilizofanikishwa na Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran katika miaka ya hivi karibuni.
Bw. Salehi vile vile amegusia kuzidi kupatikana maendeleo ya nyuklia ya Iran katika sekta za utafiti na mpango wa kujenga vinu vipya vya nyuklia nchini na kuongeza kwamba: Kufuatilia utekelezaji wa mpango mkubwa wa uvumbuzi, iwe ni uvumbizi wa angani au wa ardhini na kugundua vyanzo vipya vya kudhamini urani inayohitajika nchini, ni miongoni mwa kazi zinazofanywa hivi sasa na Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran.
Kujengwa maeneo mapya ya vinu vya nyuklia katika eneo la Bushehr na maendeleo ya mpango mkubwa wa kinu cha nyuklia cha eneo la Darkhovin ni suala jingine lililoashiriwa na Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran ambaye ameongeza kuwa: Leo hii sambamba na maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia nchini Iran, imeanza kazi ya kuzalisha "Isotopu Oksijeni 18" katika kinu cha utafiti wa nyklia cha Arak.

1392632

captcha