IQNA

Maonyesho ya Qur'ani

Maonyesho ya Qu'rani yanakuza mwingiliano wa Qur'ani miongoni mwa mataifa ya Kiislamu

15:07 - March 26, 2024
Habari ID: 3478583
IQNA - Maonyesho ya 31 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ni fursa ya kujenga maingiliano na ushirikiano kati ya mataifa ya Kiislamu katika nyanja tofauti zikiwemo sanaa, tafsiri na usomaji, afisa mmoja alisema.

Hujjatul Islam Seyyed Mustafa Hosseini Neishaburi, mkurugenzi wa kitengo cha kimataifa cha maonyesho hayo alitoa kauli hizo alipokuwa akizungumza na IQNA siku ya Jumatatu.

Akiashiria ushiriki wa wasanii na wanafikra kutoka nchi 26 tofauti katika maonyesho ya mwaka huu, alisema, "Ushiriki wao una faida kwa pande zote. Inaruhusu nchi nyingine kuthamini uwezo wa kisanii wa Iran katika kufikisha ujumbe wa Uislamu, huku Iran ikipata ufahamu kuhusu uwezo wa kisanii wa nchi nyingine za Kiislamu katika uwanja wa sanaa ya Qur'ani na kidini."

"Hii inakuza maingiliano mazuri kati ya Iran na nchi nyingine za Kiislamu," alisisitiza.

Katika maeneo ya uchapishaji, tafsiri, kaligrafia, na sanaa zinazohusiana, nchi zinazoshiriki hujifunza kutoka kwa ujuzi wa kila mmoja, kuunda harambee, alisema.

Zaidi ya hayo, Iran imeanzisha hati za maelewano na nchi mbalimbali kwa ajili ya ushirikiano, alisema, akibainisha kwamba kwa mfano, Iran inaweza kujifunza kutokana na uzoefu wa Pakistan katika kutoa mafunzo kwa wahifadhi Qur'ani na vile vile Iran na Saudi Arabia zimepata tajriba yenye mafanikio katika nyanja ya tafsiri program za kompyuta za Qur’ani, na pia Misri imedhihirisha uwezo mwingi katika uga wa usomaji Qur’ani huku Uturuki ikiwa imebobea katika fani ya kaligrafia na uandishi wa Qur’ani, na Iran imeonyesha ustadi mkubwa wa kupamba misahafu kwa dhahabu.

“Maonyesho haya, kwa hiyo, yanatoa fursa ya harambee na ushirikiano kati ya nchi mbalimbali na wasanii wao, na ushirikiano huu unaweza kuendelea zaidi ya maonyesho,” alisema.

'Muqawama katika Quran'

Afisa huyo aidha ameashiria hatua zilizochukuliwa mwaka huu za kuongeza ufahamu kuhusu suala la Palestina na hali mbaya ya watu huko Gaza ambapo mashambulizi ya Israel tangu Oktoba yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 32,200 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

"Ili kuangazia suala la Palestina na kutumia uwezo wa maonyesho, tumeandaa hafla inayoitwa 'Muqawama (mapambano ya Kiislamu) katika Quran'," alisema.

"Kama sehemu ya tukio hili, waandishi wa kaligrafia kwenye maonyesho wanashirikiana na wageni wanaopenda kuandika aya za muqawama katika Qur'ani Tukufu kila usiku," alisema, akibainisha, "Hii ni kwa sababu dhana ya muqawama sio dhana ya kisiasa na kijeshi tu, lakini pia ni itikadi ya Qur'ani. Yeyote anayeshikamana na dini na Qur'ani haiwezi kupuuza aya hizi za muqawama.”

Zaidi ya hayo, mikutano kuhusu Palestina inafanyika kila usiku, ikihudhuriwa na watu mashuhuri wa ndani na kimataifa, aliongeza.

Maonyesho ya 31 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Tehran yalizinduliwa Jumatano Machi 20 katika ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini (RA) na yanaendelea kwa muda wa wiki mbili.

Maonyesho ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tehran kila mwaka huandaliwa na Wizara ya Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Maonyesho hayo yanalenga kukuza ufahamu Qur'ani na kuendeleza shughuli za Qur'ani.

Huonyesha mafanikio ya hivi punde zaidi ya Qur'ani nchini Iran na pia bidhaa mbalimbali zinazotolewa kwa ajili ya kutangaza Kitabu hicho Kitakatifu.

3487721

Habari zinazohusiana
captcha