IQNA

Ugaidi

Makumi waauawa hujuma kanisani Nigeria, Rais Buhari alaani ukatili huo

11:31 - June 06, 2022
Habari ID: 3475341
TEHRAN (IQNA) Watu zaidi ya 50 wakiwemo wanawake na watoto, wameuawa baada ya genge lenye silaha kushambulia kanisa moja ya kikatoliki kaskazini magharibi mwa Nigeria wakati wa ibada ya Jumapili.


Duru nchini Nigeria zinadokeza kuwa watu hao wenye silaha walifyatulia risasi waumini na kulipua mabomu kwenye kanisa la St. Francis katika mji wa Owo jimboni Ondo. Washambuliaji hawakutambulika na nia yao haikufahamika mara moja.
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amelaani tukio hilo na kulitaja kuwa  ni "muaaji ya kikatili ya waumini." Amesema Nigeria katu haitasalimu amri mbele ya watu watenda maovu na kwamba hatimaye taifa la Nigeria litapata ushindi. Buhari ameamuru mashirika ya kiserikali kuchukua hatua na kuwasaidia waliojeruhiwa.
Naye Adelegbe Timileyin mbunge wa eneo la Owo katika bunge la Nigeria, amewaambia waandishi habari kwamba kasisi aliyekuwa anaongoza ibada ametekwa nyara na miongoni mwa waliofariki walikuwemo watoto wengi.
Maafisa wa usalama hawajatoa idadi ya waliofariki, lakini Timileyin anasema anadhani hadi watu 50 wameuliwa, ingawa anasema kwamba huenda idadi itakuwa kubwa zaidi.
Gavana wa jimbo la Ondo Arakunrin Oluwarotimi Akeredolu ambaye ametembelea eneo la tukio amelitaja kuwa 'mauaji makubwa ya umati' ambayo hayapaswi kukaririwa tena.

Papa Francis aliyearifiwa kuhusu shambulio hilo alitoa taarifa akisema "ninawaombea waathirika na nchi nzima, kutokana na msiba huu uliotokea wakati wa kusherehekea Pentekoste."
Nigeria imekuwa ikikumbwa na matatizo ya usalama kwa muda mrefu ambapo na magaidi na magenge ya wahalifu hutekeleza mauaji kiholela.
4062133

captcha