IQNA

Wapalestina wausafisha Msikiti wa Al-Aqsa kabla ya Ramadhani

0:15 - March 28, 2022
Habari ID: 3475082
TEHRAN (IQNA) – Maelfu ya Wapalestina walisaidia katika kusafisha Msikiti wa Al-Aqsa huko katika mji wa Quds (Jerusalem) ambao uko katika sehemu ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kukoloniwa na utawala haramu wa Israel.

Shughuli za usafishaji ni sehemu ya juhudi za kuandaa msikiti kwa ajili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Harakati ya Kiislamu katika Ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Jumuiya ya Kuilinda Al-Aqsa Awqaf (wakfu) na Mitakatifu iliandaa shughuli hizo.

Zaidi ya wanaume, wanawake na watoto wa Kipalestina 10,000 kutoka maeneo mbali mbali walishiriki katika shughuli hizo.

Pamoja na kusafisha nyua na sehemu nyingine za msikiti, shughuli hizo zilijumuisha ukarabati wa sehemu za majengo katika vitongoji vya Mji Mkongwe.

Wapalestina wanasubiri kwa shauku mwezi mtukufu ili kuhudhuria sala na ibada maalum katika msikiti huo.

Ramadhani, mwezi wa tisa wa kalenda ya Kiislamu, huzingatiwa na Waislamu duniani kote kama mwezi wa kufunga, sala, tafakari, hisani na mijimuiko ya waumini. Mwaka huu Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unatazamiwa kuanza Aprili 3.

4045223

captcha