IQNA

Matukio ya Palestina

Ripoti: Yamkini nusu ya wakazi wa Gaza wakafa njaa

19:21 - December 15, 2023
Habari ID: 3478039
IQNA- Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa, asilimia 50 ya wakazi wa eneo la Palestina la Ukanda wa Gaza linalokaliwa kwa mabavu wapo hatari ya kupoteza maisha kutokana na makali ya njaa.

Carl Skau, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Dunia (WFP) amesema hayo katika makao makuu ya umoja huo mjini New York na kuongeza kuwa, "Ukweli unaotisha ni kwamba, watu tisa kati ya kila watu kumi (Gaza) hawali vizuri, hawali kila siku na wala hawajui mlo wao ujao utatoka wapi."

Ameongeza kuwa, WFP ilifanikiwa kusambaza chakula cha msaada katika Ukanda wa Gaza wakati wa usitishaji vita kwa muda wa siku saba, lakini imeshindwa kuendelea na mpango huo baada ya kuanza upya vita katika eneo hilo.

Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amesisitizia udharura wa kusimamishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza haraka iwezekanavyo, sambamba na kufikishwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo la Palestina lililo chini ya mzingiro.

Skau amebainisha kuwa, iwapo mazingira yataruhusu, shirika hilo la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Dunia (WFP) litasambaza misaada hiyo kwa Wapalestina wengine milioni moja wa Gaza ndani ya wiki chache.

Mwito huo wa kusimamishwa mapigano Gaza umetolewa katika hali ambayo, Marekani mara kadhaa imelipigia kura ya veto azimio la kusitisha vita Gaza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; kitendo ambacho kimeendelea kulaaniwa kimataifa.

Zaidi ya Wapalestina wasiopungua 19,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wameuawa shahidi wakati wa vita vya mauaji ya halaiki ambavyo Israel ilivianzisha tarehe 7 Oktoba, kufuatia operesheni iliyofanywa na makundi ya muqawama ya Gaza iliyopewa jina la Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa.

Mustakabali wa Israel

Osama Hamdan, Mwakilishi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS mjini Beirut ameihutubu Marekani ya kwamba, "msifuatilie utakavyokuwa mustakabali wa Gaza baada ya vita, bali fikirieni mustakabali wa Israel".

Kwa mujibu wa televisheni ya Al Jazeera ya Qatar, Hamdan ameeleza kuwa, Brigedi za Al-Qassam zimetimiza ahadi ziliyotoa ya kuigeuza Gaza kuwa makaburi ya wanajeshi wa utawala ghasibu wa Kizayuni, na akaongeza kuwa Netanyahu na jeshi la Israel hawana muda mrefu kabla ya kutangaza kuwa wameshindwa.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas amebainisha kuwa, "ni baada tu ya kusitishwa kikamilifu vita dhidi ya Gaza na kukubaliwa masharti ya Muqawama kuhusu mateka, ndipo tutafanya mazungumzo".

Osama Hamdan amesisitiza kwamba Hamas inakaribisha hatua na juhudi zozote za kusimamisha vita na kuachiliwa huru mateka wa Kipalestina na akaongeza kuwa, utawala ghasibu wa Kizayuni na serikali ya Biden ndio wanaobeba dhima ya kuendelea mauaji ya halaiki ya watu wa Gaza kutokana na ukaidi wao.

Kiongozi huyo wa Hamas ameongeza kuwa, hatua ya Marekani ya kuwawekea vikwazo viongozi wa harakati hiyo inaendana na ushirikiano uliopo baina yake na utawala haramu wa Israel.

Aidha amesisitiza kwa kusema: "msimamo wetu kama ilivyo siku zote ni kutotambua utawala huo ghasibu kuwa na haki ya sehemu yoyote ya ardhi hii".

Hamdan ameongeza kuwa, maneno ya Biden kuhusu kutokuwa na lengo maalumu mashambulizi ya Israel ni kukiri Marekani kwamba kinachoendelea Gaza ni uhalifu wa kivita.

4188012/

Habari zinazohusiana
captcha