IQNA

Mauaji

Kenya kuchunguza mauaji ya umati kanisani, taasisi za kidini kuchunguzwa

22:51 - May 05, 2023
Habari ID: 3476958
TEHRAN (IQNA)- Rais William Ruto wa Kenya ameunda tume ya kuchunguza mauaji katika kanisa moja katika kaunti ya Kilifi eneo la pwani nchini humo na halikadhalika ameunda jopo kazi la kuchunguza taasisi za kidini nchini humo.

Ruto amemtwika jukumu Jaji Jessie Lessit  kuongoza kamishna wa tume itakayochunguza mauaji tata katika msitu wa Shakahola ambao uko katika shamba linalomilikiwa na kasisi aliyehusishwa na mauaji hayo. Wakili Kioko Kilukumi ataongoza wakili mkuu na kusaidiwa na Vivian Nyambeki na Bahati Mwamuye.

Tume hiyo itachunguza vifo vya zaidi ya watu 100 wanaoaminika kuwa ni wafuasi wa pote moja la Kikristo lenye misimamo mikali  ambalo kiongozi wao aliwaamuru wakae na njaa, msemaji wa rais Ruto alisema.

Kulingana na notisi kwenye gazeti la serikali, tume hiyo itatayarisha ripoti chini ya miezi sita na kutoa mapendekezo yao kwa Rais Ruto. Tume hiyo  ina jukumu la kubainisha chanzo cha vifo vilivyotokea na pia kuchunguza ni nini kilichosababisha idara za usalama, usimamizi, na sheria kufeli kuchukua hatua hadi mkasa kufanyika.

Serikali ya Kenya inasema waliofariki walikuwa wanachama wa kanisa la Good News International linaloongozwa mhubiri tata wa Kikrsito Paul Mackenzie, ambaye  wafuasi wake wanasema alitabiri mwisho wa dunia ungekuwa tarehe 15 Aprili na hivyo kuwaagiza wafuasi wake kujiua ili wawe wa kwanza kwenda mbinguni.

Idadi ya vifo imefikia 111, lakini inaweza kuongezeka zaidi kwani maafisa wa usalama wanaendelea kutafuta makaburi ya umati katika eneo la kanisa hilo.

Mackenzie, ambaye anashikiliwa na  polisi, hajazungumza chochote hadharani juu ya tuhuma zinazomkabili na wala hajatakiwa kujibu shitaka lolote la jinai. Wakili wake George Kariuki aliambia wanahabari Jumanne kwamba mteja wake anaweza kukabiliwa na "mashtaka ya ugaidi".

Mackenzie alifikishwa mahakamani katika mji wa Mombasa siku ya Ijumaa, ambapo waendesha mashtaka walimtaka hakimu amzuilie kwa siku 90 zaidi huku uchunguzi wao ukiendelea.

Akiitangaza tume hiyo, Msemaji wa rais Hussein Mohamed, alisema Ruto pia ameteua kikosi kazi kutathmini kanuni zinazosimamia taasisi za kidini nchini Kenya.

4137806

captcha