IQNA

Rais Assad wa Syria

Marekani inazuia misaada kuwafikia waathirika wa mitetemeko ya ardhi Syria

18:21 - February 09, 2023
Habari ID: 3476535
TEHRAN (IQNA)- Rais Bashar al-Assad wa Syria amefichua kuwa Marekani inatoa mashinikizo kwa nchi zinazotaka kuwasaidia waathirika wa mitetemeko ya ardhi nchini Syria. Assad ameyasema hayo katika mkutano na ujumbe wa mawaziri kadhaa wa Lebanon.

Tetemeko la kwanza la  ardhi la ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Rishta lilitikisa kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria Jumatatu asubuhi ya tarehe 6 Februari. Kitovu chake kilikuwa ni katika mji wa Gaziantep wa Uturuki ambapo mamia ya majengo yameporomoka.Masaa machache baadaye kulijiri mtetemeko mwingine wa ardhi uliokuwa na ukubwa 7.6 kwenye kipimo cha rishta.
Rais wa Syria amekutana na kufanya mazungumzo mjini Damascus na ujumbe wa mawaziri wa Lebanon unaoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Abdallah Bouhabib.
Katika mazungumzo hayo, Assad ametoa shukrani kwa Lebanon na nchi zote ambazo ziko pamoja na Syria katika kipindi hiki kigumu na akasema nchi nyingi zinashinikizwa na Marekani zisiisaidie Syria.
Rais wa Syria amesisitiza pia umuhimu wa ushirikiano kati ya Beirut na Damascus katika nyanja zote kwa kuzingatia uwezo wa nchi hizo mbili na maslahi ya pamoja yanayozikurubisha.

Ujumbe wa mawaziri wa Lebanon umeeleza kuwa serkali na wananchi wote wa Lebanon wako pamoja na watu wa Syria na kusisitiza kwamba Walebanon wanashirikiana na wananchi na serikali ya Syria katika majonzi na masaibu yaliyowapata na wanaitakidi kuwa ni wajibu wao kuwa pamoja na ndugu zao wa Syria katika hali hii ngumu inayowakabili.

Katika mkutano huo, mawaziri wa Lebanon walijadili hatua na maamuzi yaliyopitishwa na kutangaza kuwa, Lebanon imefungua viwanja vya ndege na bandari zake ili kutuma misaada Syria kutokea pande zote.
Ikiwa yameshapita masaa 72 tangu kutokea kwa janga hilo, wataalamu wa maafa wameonesha wasiwasi wao wa kuweza kuokoa maisha zaidi. Mamlaka zimefahamisha kuwa watu 12,873 wamekufa nchini Uturuki na takriban 3,162 katika nchi jirani ya Syria.
3482415
Kishikizo: syria mitetemeko uturuki
captcha