IQNA

Mahakama Nigeria yaakhirisha tena kesi ya Sheikh Zakzaky

16:45 - February 25, 2020
Habari ID: 3472503
TEHRAN (IQNA) - Mahakama ya Nigeria imeakhirisha tena kusikiliza kesi ya Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN), Sheikh Ibrahim Zakzaky hadi mwezi Aprili.

Maafisa wa mahakama nchini Nigeria walitangaza jana kuwa kesi ya Sheikh Zakzaky imeakhirishwa tena na imepangwa kusikilizwa tarehe 23 na 24 Aprili mwaka huu.

Kwa uamuzi huo uliotolewa na mahakama, kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, ambaye yeye mwenyewe pamoja na mkewe hali zao za afya ni mbaya sana, wataendelea kushikiliwa kwenye jela ya jimbo la Kaduna kwa muda wa miezi miwili mingine.

Akizungumza na mwandishi wa IQNA, Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu (IHRC) Bw. Masoud Shajareh ametoa mwito tena wa kuwataka viongozi wa serikali ya Abuja wamwachie huru Sheikh Zakzaky na mkewe. Aidha amesema hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky na mke wake, Zeenah, inazidi kuzorota na wanahitaji msaada wa dharura wa kiafya. Ameoneza kuwa wakuu wa jela ya Kaduna wamekataa kutoa msaada unaohitajika wa kitiba kwa wawili hao.

Masoud Shajareh amesisitiza kuwa, kesi ya kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ni ya kisiasa; na kwa mujibu wa sheria za Nigeria na hata za kimataifa, Sheikh Zakzaky na mkewe inapasa waachiliwe huru kwa kutolewa jela haraka iwezekanavyo.

Makumi ya wanachama wa IMN pamoja na kiongozi huyo wa harakati hiyo wamewekwa kizuizini tangu walipotiwa nguvuni mwaka 2015 baada ya jeshi la Nigeria kushambulia Husainia ya mji wa Zaria jimboni Kaduna; na tangu wakati huo hadi sasa wanaendelea kusota jela pasi na kuthibitishwa makosa na mashtaka yanayowakabili.

Licha ya Mahakama Kuu ya Nigeria kuwahi mara moja kutoa hukumu iliyosisitiza kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe hawana hatia yoyote na ikaamuru waachiliwe huru, lakini wawili hao wangali wameendelea kuwekwa jela na hivi sasa hali zao za afya ni mbaya sana.

3470743

captcha