IQNA

Kulekea katika Umoja wa Waislamu kwa mujibu wa sira ya Bwana Mtume SAW

11:31 - January 08, 2015
Habari ID: 2684362
Hivi sasa tumo katika Wiki ya Umoja kati ya Waislamu ambayo ilitangazwa na hayati Imam Khomeini kutokana na hitilafu za mapokezi kuhusu siku aliyozaliwa Mtume Muhammad SAW. Wiki hiyo inaanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal.

Makusudio ya umoja wa umma wa Kiislamu ni haya kwamba, Waislamu kila mmoja akiwa na madhehebu yake wajumuike pamoja katika mambo ya kidini yanayowakutanisha pamoja kama Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Qur’ani Tukufu, Mtume SAW, sunna na sira ya Mtume SAW, mkabala na hatari zinazoikabili misingi na nguzo za Uislamu na jamii ya Waislamu kwa ujumla. Kwa muktadha huo, Waislamu wanapaswa kushikamana, kuunganisha nyoyo zao na kujiweka mbali na tofauti za kimadhehebu, kisiasa, kikaumu na kilugha ambazo hazina matunda yoyote ghairi ya kudhoofisha umma wa Kiislamu. Ni jambo lisilo na shaka kuwa, sira ya Mtume SAW inaweza kuwa mbainishaji na mfasiri wa misingi na vigezo vya kuleta umoja katika hali ya sasa inayotawala katika ulimwengu wa Kiislamu.

Sira hii inawezekana kuichunguza katika engo mbalimbali. Mtume SAW alikuwa akiutambua umoja wa umma wa Kiislamu kama mkakati wa kimsingi wa nguvu ya ya Waisamu katika zama zote na alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kufikiwa hilo, kiasi kwamba, nguvu na izza ya jamii changa ya Kiislamu katika kipindi cha risala na Wahyi, natija yake ilikuwa ni miongozo na juhudi za kuleta umoja za Mtukufu huyo. Kupitia sira ya kisiasa, kijamii na kiutamaduni ya Bwana Mtume SAW tutafahamu kwamba, suala la umoja sio muhimu kwa Waislamu tu bali ni jambo lenye umuhimu wa aina yake hata kwa jamii zisizo za Kiislamu; chambilecho Waswahili, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Kwa hakika hayo ni mambo ambayo Bwana Mtume SAW alikuwa akiyapa kipaumbele katika jamii. Imam Ali AS anasema katika Nahaj al-Balagha kwamba: “Mtume SAWaliondoa mapengo ya kijamii kwa umoja, akaleta marekebisho na akaunganisha nyufa zilizokuwako katika jamii.”

Mtume Muhammad SAW akiwa na lengo la kuleta umoja na mshikamno wa umma wa Kiislamu, alitumia mikakati ya kiitikadi, kimaadili, kisiasa na kiutamaduni. Kupambana na fikra chafu za shirki na zisizokuwa za kitawhidi na kisha badala yake kuleta fikra za kitawhidi, kulipelekea kupatikana uwanja na mazingira ya umoja wa kiitikadi kwa namna fulani. Hatua ya Bwana Mtume SAWya kuegemea katika Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, hususan kuiunganisha risala na ujumbe wake na misingi ya dini ya Nabii Ibhrahim AS ilikuwa njia bora na mwafaka kabisa ya kustafidi na mazingira ya kijamii ya zama zile kwa ajili ya kuleta umoja wa kifikra.

Moja ya mbinu zilizotumiwa na Mtume Muhammad SAW kwa ajili ya kulinda umoja na mshikamano wa Waislamu ni kulinda usawa na uadilifu. Mtukufu huyo aliondoa kabisa sera za ukabila na ubaguzi wa aina zote.

Ujumbe wa Tawhidi na imani ya Mungu Mmoja wa Mtume SAW na wito wa kuwepo usawa na uadilifu ulifuta kikamilifu ada za kijahilia na ubaguzi wa kidhalimu, na kutayarisha uwanja mzuri wa kujiunga watu wa kabila, kaumu na mataifa tofauti katika dini ya Uislamu. Katika jamii ya kijahilia ya zama zile, kulikuwa na kundi miongoni mwa Warabu ambalo lilikuwa lingali likiamini dini aliyokuja nayo Nabii Ibrahim AS yaani ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Chini ya kalima ya Tawhidi, Bwana Mtume SAW aliliweka katika mipango yake ya mwanzo suala la kupambana na nembo za dhulma, ufisadi na uonevu ulimwenguni.

Jambo jingine lililokuwa na nafasi na taathira muhimu katika kuunganisha na kuuleta pamoja umoja wa Kiislamu na jamii ya Kiislamu katika zama za Bwana Mtume SAW ni mwenendo mzuri na tabia njema ya Mtume wa Allah. Wanahistoria wamekiri ukweli huu kwamba, kile ambacho kilimfanya Mtume SAW atawale katika nyoyo za watu ni mwenendo wake mwema hasa namna alivyokuwa akiamilia vizuri na watu. Tabia njema, moyo mpana wa ustahamilivu, huruma kwa masikini na wastadhaafu na kujiweka mbali na kujiona, kujikweza, kutaka jaa na uongozi ni thamani aali za kiakhlaqi na kimaadili ambazo zilimfanya awe mahbubu na mpendwa wa watu wote.

Kwa hakika uwepo wa Mtume ulikuwa ukihesabiwa kuwa kitovu na kituo cha kuwakutanisha na kuwaleta pamoja Waislamu. Katu Mtume SAW hakuwahi kutumia daraja na cheo chake cha Utume kwa ajili ya kuwaogofya na kuwatisha watu. Bali alikuwa kiongozi mpole, mwenye kuguswa mno na mambo ya watu, msamehevu na aliyaweka mambo haya katika faharasa ya mwenendo wake na watu. Mfano hai na wa wazi wa Mtume kusamehe ni msahama wake alioutoa kwa watu wote wa Makka.

Baada ya mji wa Makka kukombolewa yaani Fat’hi Makka, wakazi wa mji huo ambao walimtendea dhulma Mtume na masahaba zake walisamahewa wote. Hii ni katika hali ambayo, Mtume na wafuasi wake walikuwa katika kilele cha nguvu na wangeweza kuitumia fursa hiyo kulipiza kisasi. Mtume SAW alihutubia siku ya Fat’hi Makka na kusema:

“Mwislamu ni ndugu wa Muislamu, hamdhulumu, haachi kumsaidia, wala hamdanganyi na wala hamdharau. Ni jukumu la Waislamu kushikamana na kufanya juhudi kwa ajili ya kuwasaidia wasiojiweza na kuwa na kuhurumiana wao kwa wao.”

Wapenzi wasikilizaji, tabia njema yenye kuvutia ya Bwana Mtume SAW daima ilikuwa moja ya sababu muhimu za kuondoa hitilafu na mkakati wenye thamani, mhimili wa huba na umoja wa nyoyo. Inasikitisha hii leo, akthari ya nchi za Kiislamu hazina viongozi waadilifu, wenye uchungu na nchi yao na wa kuaminika, jambo ambalo limepelekea kuweko pengo baina ya umma wa Kiislamu na watawala. Jambo hili limezifanya jamii za Kiislamu kukabiliwa na changamoto na matatizo mengi kutoka ndani na hivyo kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na adui yao mmoja wa nje. Mazingira haya yameandaa uwanja wa kuingia baina ya Waislamu makundi na harakati za kuwafarakanisha Waislamu. Mtume SAW akitumia nafasi yake na kwa kuwa na tadibiri na muono wa mbali alifanikiwa kung’oa mizizi mikubwa ya hitilafu katika jamii ya wakati huo. Moja ya matatizo makubwa ya jamii ya Madina wakati huo lilikuwa ni suala la ukabila. Makabila hayo yalikuwa na hitilafu baina yao.

Kuingia Madina Bwana Mtume SAW kulikwenda sambamba na kutiliana saini mikataba na makundi mbalimbali. Mikataba hiyo inaweza kuwa mikakati ya wazi kabisa kwa ajili ya umoja wa Kiislamu katika jamii ya wakati huo.  Baada ya kuingia Yathrib, yaani Madina, Mtume Mtukufu alitayarisha mazingira ya kujenga umoja na mshikamano katika jamii mpya ya Kiislamu. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na mtukufu huyo ni kutayarisha mkataba wa kwanza kabisa katika Uislamu katika miezi ya mwanzoni mwa kuwepo kwake Yathrib (Madina). Mkataba huo uliandaa uwanja wa kuweko umoja wa kisiasa na kiutawala. Aidha hatua yake ya kuunga  udugu baina ya Muhajirina (Waislamu waliohama kutoka Makka) na Ansar (wenyeji wa Madina) wa kusaidiana katika njia ya haki nayo ilikuwa na umuhimu wa aina yake. Kwa hatua hiyo Mtume SAW alijenga umoja na mshikamano wa pande zote kati ya Muhajirina na Ansar.  Hatua hizo za Mtume SAW ni misdaqi na dhihirisho la aya ya 10 katika Surat al-Hujuraat inayosema: Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.

2670900

captcha