IQNA

Hauli ya Imam Khomeini

Kongamano la Imam Khomeini lafanyika kwa njia ya intaneti Afrika Mashariki

8:29 - June 05, 2023
Habari ID: 3477100
Kongamano kwa mnasaba wa kukumbuka mwaka wa 34 wa kuaga dunia Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu Amrehemu) limefanyika kwa njia ya mtandao na kuwaleta pamoja wasomi na wanafikra wa Afrika Mashariki.

Kikao hicho ambacho kimefanyika Jumapili kwa njia ya intaneti kimeandaliwa na Kitengo cha Utamaduni cha Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Kenya kwa ushirikiano na vitengo vya utamaduni katika balozi za Iran nchini Uganda na Tanzania.

Akizungumza katika kikao hicho, Profesa. Adam Sebyala, wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al-Mustafa, Uganda aliashiria  mtazamo wa Imam Khomeini kuhusu haki ya kijamii na usawa.

Aidha aliangazia juhudi za Imam Khomeini za kupambana na umaskini, ufisadi, na ukosefu wa haki, huku akigusia hali ya haki katika jamii ya sasa.

Alibainisha kuwa Imam Khomeini alijenga shakhsia yenye nguvu sana na akaongoza kivitendo kwani alikuwa wa kwanza kutekeleza  sera kwa kujinyima  huduma za serikali alizopewa

Profesa Sebyala amesema Imam Khomeini aliurudisha ulimwengu kwenye zama bora za  Mtume Muhammad (SAW) kimaadili na kijamii ndani ya mipaka ya utamaduni wa Kiislamu.

Naye Dkt. Hassan Kinyua wa Kenya ambaye ni  mwandishi, mwanasheria na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi (UON), alizungumza kuhusu msukumo wa Imam Khomeini kuhusu umoja wa Waislamu na mazungumzo baina ya  dini mbalimbali.

Amesema Imam Khomeini alijitahidi sana kuziba mapengo kati ya madhehebu na dini mbalimbali, huku akikuza uelewano na kuishi pamoja kwa amani.

Kwa upande wake, Stambuli Abdul Nassir, mwanahistoria maarufu kutoka Mombasa, Kenya alizungumza kuhusu Imam Khomeini na ushawishi wake wa kimataifa.

Mohamed Ridha Mortazavinia, mwanazuoni wa Kiislamu mwenye makao yake Tanzania alizungumza kuhusu mapambano na ukombozi kwa mtazamo wa Imam Khomeini.

Alisema kuwa mapambano na kusimama kidete dhidi ya ukoloni mamboleo ndio njia pekee ambao ya kuleta mabadiliko nchi za Afrika. Alisema Imam Khomeini alitufundisha kumwamini na kumtegemea Mwenyezi Mungu ikiwa tunataka mabadiliko yoyote katika maisha na jamii zetu.

Kwa upande wake Sheikh Ali Mwega, msomi wa Kiislamu kutoka Nakuru, Kenya alijadili mtazamo wa Imam Khomeini kuhusu masuala ya kiroho na Imani. Pia alichunguza jinsi hali yake ya kiroho ilivyoongoza matendo na maamuzi yake, na jinsi inavyoendelea kuwatia moyo watu kuimarisha uhusiano wao na imani yao.

Akihutubia kikao hicho Seyed Hassan Albeity, mwanaharakati wa Kiislamu na mwanasiasa maarufu kutoka Lamu, Kenya alizungumza kuhusu athari za kimataifa za Imam Khomeini na Mapinduzi ya Kiislamu aliyoyaongoza.

Amebainisha kuwa Imam Khomeini alitumia mbinu mpya ya Kiislamu ya mapinduzi ambayo ilikuwa ya kipekee sana ikilinganishwa na mapinduzi mengine ambapo watu wanatumia unyanyasaji wa bunduki na ushawishi wa kifedha ili kuchukua madaraka.

Aliwakumbusha washiriki kwamba Imam Khomeini allisisitiza kuhusu umuhimu wa kupata mafunzo ya Mwezi Mtukufu Ramadhan na matukio ya Karbala ili kuendeleza mapambano na kukabiliana na vikwazo vya kiuchumi vya maadui.

4145443

Kishikizo: imam khomeini
captcha