IQNA

Waislamu Ethiopia

Watu watatu wauawa katika maandamano ya Waislamu wanalalmikia kubomolewa misikiti Ethiopia

13:05 - June 03, 2023
Habari ID: 3477088
TEHRAN (IQNA)- Mvutano unaendelea nchini Ethiopia kuhusu mpango tata wa kubomoa misikiti nchini humo, huku watu watatu wakiuawa katika mapigano ya hivi punde siku ya Ijumaa.

Waliuawa wakati polisi walipopambana na waumini nje ya msikiti mkubwa zaidi wa Addis Ababa, vikosi vya usalama vya Ethiopia vilisema.

Maeneo kadhaa ya ibada ya Waislamu yameharibiwa mjini Addis Ababa katika miezi ya hivi karibuni, uharibifu huo ni sehemu ya mradi wenye utata wa mipango miji ambao umezua hasira miongoni mwa waumini.

Ijumaa iliyopita, mapigano yalizuka nje ya Msikiti wa Grand Anwar, na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine dazeni kujeruhiwa, polisi ilisema na kwamba waliwakamata watu 114. Wajumbe wa Republican Guard, kitengo chenye jukumu la kulinda taasisi na maafisa wa serikali, pia walikuwepo.

Baadhi ya watu waliokuwemo katika umati huo waliwarushia mawe polisi, na polisi waliwajibu kwa mabomu ya kutoa machozi.

Haijajulikana kama polisi walitumia risasi, makombora ya plastiki au au walipiga risasi tupu. Milio ya risasi iliendelea kusikika kwa takriban saa mbili kabla ya hali ya utulivu kurejea, huku polisi wakiwa wamezingira barabara zilizopo jirani na msikiti huo.

Amir, muumini na kijana aliyekuwepo katika msikiti huo wakati wa sala ya Ijumaa alisema: "Tulifahamu kiasi kitakachotokea baada ya swala." "Mamia ya kaka na dada zetu walikamatwa wiki iliyopita... watu wana hasira misikiti yetu inaharibiwa."

Mradi wa mipango miji, unaojulikana kama Sheger City, unahusisha muunganisho wa manispaa kadhaa katika eneo la Oromia nje kidogo ya mji mkuu wa nchi hiyo.

Pia Mradi huo umesababisha ubomoaji wa nyumba na maeneo ya biashara, na wanaharakati wa haki za watu wa eneo hilo wameuita mradi huo kuwa ni "kinyume cha sheria ".

Wakati huo huo, Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Ethiopia limeeleza kutoridhishwa kwake na taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na ofisi ya mawasiliano ya serikali ya mkoa wa Oromia, ikitaja kushindwa kuwakilisha kwa usahihi hisia na mahitaji ya jamii pana ya Waislamu nchini Ethiopia.

Baraza Kuu lilisema katika taarifa yake siku ya Alhamisi, kwamba kamati ya watu tisa, ambayo iliundwa kufuatia kikao cha dharura cha baraza hilo Mei 28, kwa sasa inajadiliana na viongozi wa ngazi za juu kutoka serikali ya shirikisho, kwa lengo la kutatua suala hilo. ya kubomoa misikiti.

Likitoa wito kwa jamii ya Kiislamu kusubiri kwa subira matokeo ya majadiliano yanayoendelea, baraza hilo lilitahadharisha dhidi ya uwezekano wa kutumiwa hali hiyo na makundi fulani yenye ajenda za kisiasa, na kuwataka kujiepusha na vitendo vyovyote haramu.

3483808

captcha