IQNA

Waislamu Afrika

Maandamano ya kulaani kubomolewa misikiti zaidi ya 19 Ethiopia yapelekea wawili kuuawa

15:48 - May 29, 2023
Habari ID: 3477063
TEHRAN (IQNA)- Watu wawili wameuawa wakati askari polisi walipowashambulia Waislamu walioandamana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa kupinga kubomolewa misikiti yao zaidi ya 19 katika eneo la kandokando ya mji huo.

Makumi ya Waislamu katika mji wa Addis Ababa, Ijumaa waliingia barabarani baada ya Sala ya Ijumaa kutokea msikiti mkuu wa Anwar na kuandamana kupinga bomoabomoa ya misikiti kadhaa katika mji huo.

Waislamu hao walitoa kauli mbiu dhidi ya serikali na mradi wake mkubwa wa ujenzi wa Jiji Kubwa la Sheger ambalo litazunguka mji mkuu huo wa Ethiopia na kutaka ubomoaji wa misikiti ukomeshwe.

Kwa mujibu wa mashuhuda, askari wa vikosi vya usalama waliopelekwa eneo la msikiti huo kukabiliana na maandamano hayo walikabiliwa na upinzani wa waandamanaji, hivyo wakafyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi na kuwajeruhi watu kadhaa. Wawili kati ya majeruhi walifariki baada ya kukimbizwa hospitalini.

Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu katika mkoa wa Oromia limesema, shambulio la vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji lilikuwa la kinyama na kinyume cha sheria na kubainisha kuwa, raia hao Waislamu waliandamana kwa amani kutetea haki zao.

Mwaka jana, serikali ya Ethiopia ilizindua mpango wenye utata wa kutaifisha maeneo sita magharibi mwa mji mkuu Addis Ababa, na tangu miezi michache iliyopita, imeanza kubomoa majengo, nyumba na misikiti, ambayo inadai ilijengwa kinyume cha sheria.

Wapinzani wanalaani mradi huo wakisema ni wa kibaguzi na kuongeza kuwa ubomoaji wa nyumba na misikiti unafanywa kwa kutumia vigezo vya kikabila na kidini dhidi ya watu wasio wa kabila la Oromo na Waislamu.

Raia wengi wa Ethiopia ni Wakristo hasa wa madhehebu ya Othodoksi, lakini Waislamu walio wachache ni takriban theluthi moja ya watu wote wa nchi hiyo.

3483715

Kishikizo: ethiopia waislamu
captcha