IQNA

Hali ya Waislamu duniani

Waislamu Kanada walalamikia marufuku ya kusali iliyowekwa katika shule za serikali

10:16 - May 22, 2023
Habari ID: 3477029
Waislamu nchini Kanada wamelalamikia marufuku ya kusali iliyowekwa katika shule za serikali jimboni Quebec.
Kwa mujibu wa amri ya Waziri wa Elimu wa jimbo la Quebec nchini Kanada, ni marufuku kwa vijana wa Kiislamu kutekeleza faradhi yao ya Sala katika shule za serikali za jimbo hilo.
Waislamu wa Kanada wamewasilisha malalamiko yao dhidi ya uamuzi huo na kusisitiza kwamba kupiga marufuku watu kusali katika skuli za serikali za Quebec kunapingana na Katiba ya nchi hiyo.
Jumuiya za Kiislamu nchini Kanada zimeitaka mahakama itangaze kwamba uamuzi uliochukuliwa na maafisa wa jimbo la Quebec umekiuka katiba ya nchi.
Taasisi sita, ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Kiislamu ya Kanada na Taasisi ya Waislamu wa Kanada, pamoja na asasi zingine nne za jimbo hilo, zimewasilisha kesi ya kutaka Mahakama ya Juu ya Quebec itangaze kuwa amri iliyotangazwa na jimbo hilo haitekelezeki au iifute.
Asasi hizo zimesisitiza kuwa agizo hilo ni la kibaguzi na linakiuka Mkataba wa Haki na Uhuru wa Kanada.
Amri hiyo wa Waziri wa Elimu wa Quebec ya kupiga marufuku watu kusali maskulini ilitangazwa Aprili 19, baada ya kupokea ripoti kwamba maafisa wa skuli zisizopungua mbili nchini Kanada wanawaruhusu wanafunzi kukusanyika katika uwanja wa skuli kwa ajili ya kusali.
4141907
captcha