IQNA

Undumakuwili katika kadhia ya Shahidi Shireen Abu Akleh

17:53 - May 15, 2022
Habari ID: 3475254
TEHRAN (IQNA)- Ushahidi wote unaonyesha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umemuua kwa makusudi mwandishi wa habari wa kike na Mkristo wa televisheni ya Al-Jazeera ya Qatar Shireen Abu Akleh kwa mujibu mpango maalumu uliokuwe umeratibiwa tangu hapo awali.

Risasi ya mlenga shabaha wa Israel iliyofyatuliwa kutoka kwa gari la jeshi la Israel aina ya Jeep ilimpiga kichwani mwandishi huyo wa habari katika sehemu ambayo haikuwa na fulana ya kuzuia risasi, na kwa msingi huo si jambo lililofanyika kwa sadfa na bahati mbaya bila ya kupangwa na kuratibiwa hapo awali, na kuchaguliwa mlenga shabaha mahiri kwa ajili ya jinai hiyo. Israeli ilikuwa na hasira kubwa na Shireen Abu Akleh ambaye tangu mwaka 1997 amekuwa akiwajulisha walimwengu kuhusu siasa za ukandamizaji na kupenda kujitanua za utawala wa Kizayuni na kuzuia upotoshaji wa utawala huo.

Baada ya Israel kufeli na kushindwa kuzuia operesheni za Wapalestina katika ardhi ya Palestina iliyovamiwa na kaliwa kwa mabavu mwaka 1948 yaani Israel, hususan huko Tel Aviv, imekuwa ikifanya mikakati ya kulipiza kisasi. Awali ilitaka kufanya mauaji ya kigaidi dhidi ya Yahya al Sinwar, mkuu wa harakati ya Hamas huko katika Ukanda wa Gaza ambaye katika Siku ya Kimataifa ya Quds alipongeza operesheni za kujitolea mhanga za Wapalestina dhidi ya Israel. Lakini kutokana na kuogopa jibu kali la harakati aa mapambano ya ukombozi hususan Hamas, Israel iliamua kusitisha mpango huo wa mauaji ya kigaidi na badala yake sasa umemlenga mwandishi wa habari aliyekuwa akifichua mipango na jinai za utawala huo kwa walimwengu, Shireen Abu Akleh. 

Mazishi yaliyoakisiwa duniani kote

Hata hivyo, mahudhurio makubwa ya Wapalestina katika mazishi Abu Akleh ambayo yamewakumbusha walimwengu mazishi ya kiongozi wa zamani wa PLO, Yasser Arafat, ambaye pia alikuwa muhanga wa njama za Israel, yamepiga kengele ya tahadhari kwa Waisraeli. Vyombo vya habari duniani kote, hata vya Wamagharibi havikuwa na budi ila kuakisi mazishi ya mwanahabari huyo.

Hivyo basi, kuanzia sasa tunaweza kukisia kwamba Wapalestina wanajiandaa kulipiza kisasi kwa Waisraeli baada ya jinai hiyo ya kikatili. Wakati huo huo, mauaji ya Shireen Abu Akleh yamekuwa sababu mpya ya kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa wa Wapalestina.

Nje ya Palestina pia mashinikizo ya kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yameongezeka, na licha ya upinzani na pingamizi za Marekani na Uingereza, juhudi zinaendelea kwa ajili ya kufungua kesi mpya dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. 

Undumakuwili wa Wamagharibi katika kulaani

Pamoja na hayo yote inatupasa kukiri kwamba, licha ya wimbi la kulaani na ukosoaji wa duru za kimataifa na za Magharibi dhidi ya mauaji ya mwandishi huyo wa habari wa Al-Jazeera, hatupaswi kupuuza ukweli kwamba, misimamo hii haikuwa sawa na ukubwa wa jinai na mauaji ya kutisha ya mwandishi huyo wa kike wa habari aliyekuwa akitekeleza majukumu yake.

Ni wazi kwamba kama mauaji kama hayo yangetokea katika vita vya Ukraine, na mwandishi wa habari wa Magharibi au wa Kiukreni akalengwa na kupigwa risasi kichwani na askari wa Russia, yangepigwa makelele mengi na kuzushwa mijadala juu ya haja ya kuchukuliwa hatua za kisheria; na kadhia hiyo ingekuwa habari nambari moja kwa wiki kadhaa na kupewa kipaumbele katika vyombo vya habari vya Magharibi sambamba na kuwashwa mishumaa ya kuwalilia. Vilevile tungeshuhudia hatua mbalimbali huko Magharibi na Ulaya, ikiwa ni pamoja na kunyamaza kimya dakika chache katika mikutano rasmi kwa heshima ya mhasiriwa, kwa kisingizio cha kuunga mkono uhuru wa kujieleza na demokrasia!

Masikini Shireen Abu Akleh, hakufanyiwa lolote kati ya mambo hayo; na zaidi ni kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel haukuwaruhusu Wapalestina kumpa heshima stahiki za mwisho na kumzika ipasavyo mwandishi huyo wa habari.

Hata hivyo, mwili Shireen Abu Akleh umepumzishwa eneo lile lile la Mashariki mwa Quds (Jerusalem), ambako ndiko ilikoanzia intifadha ya hivi karibuni ya Wapalestina kwa ajili ya kuitetea Quds tukufu, yaani kitongoji cha Sheikh Jarrah, na hatimaye ikapelekea kuanza Operesheni ya Upanga wa Quds.

Kwa hiyo, ingawa mauaji ya kigaidi ya Israel yamezima sauti Shireen Abu Akleh, lakini hapana shaka kuwa kaburi lake litakuwa kituo kingine cha mapambano ya ukombozi huko Quds, na njia yake itaendelea kuenziwa na wapigania uhuru wa Palestina.

/4057140/

captcha