IQNA

Palestina yaunga mkono uchunguzi wa kimataifa kuhusu mauaji ya Shireen Abu Akleh

17:12 - May 14, 2022
Habari ID: 3475247
TEHRAN (IQNA)- Mamlaka ya Ndani ya Palestina imesema inaunga mkono kuhusishwa taasisi za kimataifa katika uchunguzi kuhusu kitendo cha jinai cha askari wa Israel cha kumuua shahidi mwandishi habari Mpalestina wa Kanali ya Al Jazeera Shireen Abu Akleh.

Mapema Jumatano, mwandishi wa habari ya televisheni ya al Jazeera, Shireen Abu Akleh, 51, alipigwa risasi na kuuliwa shahidi kikatili na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakati akiwa kwenye kazi yake ya kuripoti uvamizi wa kijeshi wa jeshi la Israel katika kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Jenin.

Jinai hiyo ya Israel imibua hasira kote duniani na hasira zimeongezeka zaidi kufuatia shambulio la kikatili lililofanywa na wanajeshi wa utawala haramu wa Israel dhidi ya waombolezaji waliokuwa wakiusindikiza mwili wa Abu Akleh.

Hussein al Sheikh, afisa mwandamizi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameandika katika  ukurasa wake wa Twitter kuwa, mamlaka hiyo inaunga mkono uchunguzi wa kimataifa kuhusu mauaji ya Abu Akleh.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina nayo imetoa taarifa na kueleza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel sio tu umemuua shahidi kwa damu baridi Shireen Abu Akleh, bali umeufatilia mwili wa shahidi huyo hadi katika maziko yake. Taarifa hiyo imongeza kuwa jinai ya Israel dhidi ya Abu Akleh ni ugaidi wa kiserikali ulioratibiwa na kuongeza kuwa, "Israel inaogopa pia maiti ya mwandishi habari huyo Mpalestina ikiwa katika mikono ya watu."

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imeitaja Israel kuwa ni utawala ulioasi, ghasibu, wa kibaguzi na utawala kandamizi unaokiuka haki za binadamu na kutenda jinai kila uchao dhidi ya watu wa Palestina. Imesema, utawala wa Israel hauwezi kurekebishwa isipokuwa kwa kuwekewa vikwazo.  

3478892

captcha