IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kikosi cha Quds ni sababu muhimu zaidi inayozuia diplomasia legevu Asia Magharibi

1:21 - May 03, 2021
Habari ID: 3473871
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) ni sababu muhimu zaidi na athirifu ya kuzuia diplomasia legevu na isiyo na irada katika eneo la Asia Magharibi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesema hayo Jumapili mjini Tehran katika hotuba yake kwa mnasaba wa Siku ya Wafanyakazi Duniani na Siku ya Mwalimu ambapo sambamba na kukosoa matamshi yanayotolewa na viongozi rasmi wa nchi ambayo yanatumiwa vibaya na maadui amesisitiza kwamba,  Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) ni sababu kubwa kabisa athirifu ya kuzuia diplomasia legevu na isiyo na irada katika eneo la Asia Magharibi.

Ayatullah Khamenei amekosoa faili la sauti ambalo liko mikononi mwa vyombo vya maadui na wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu na kueleza kwamba, kwa miaka mingi sasa Wamarekani wamekasirishwa na ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema pia katika hotuba yake hiyo kwamba, ni kwa sababu hiyo ndio maana Wamarekani hawakuwa wakimpenda shahidi Qassim Suleimani na ndio maana wakamuua shahidi.

Ayatulllah Khamenei ameongeza kuwa, hatupaswi kusema mambo ambayo yatakuwa na maana ya kama vile tunakariri matamshi ya maadui.

Kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, madola ya Magharibi yamekuwa yaking'ang'ania na kutaka sera za kigeni za Jamhuri ya kiislamu ya Iran ziwe chini ya bendera yao, hili ndilo wanalotaka, kwa sababu kwa miaka mingi hali ilikuwa hivyo (kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu).

Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa mipango yote ya nchi iwe ni ya kijeshi, kisayansi, kiutdamaduni na kidiplomasia ndio ikijumuishwa hujenga sera ya nchi. Kwa msingi huo ni kosa kupuuza mpango mmoja na kosa hilo halipaswi kufanywa na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu.

Aidha hakuna sehemu yoyote duniani ambayo utapata sera za kigeni zinaanishwa na wizara ya mambo ya nje bali kile ambacho hufanyika ni kuwa wakuu wa ngazi za juu huainisha mielekezo ya sera za kigeni ambayo hutekelezwa na wizara ya mambo ya nje.

Ameongeza kuwa, katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sera za kigeni huainishwa na Baraza Kuu la Usalama wa taifa katika viako ambavyo huhudhuriwa na wakuu wa nchi na kile ambacho wizara ya mambo ya nje hufanya ni kutafuta mbinu za kutekeleza sera hizo.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, kauli hiyo ya Kiongozi Muadhamu imekuja baada ya klipu ya sauti kuvuja ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif anasikika akilalamika kuwa eti diplomasia ya Iran imetolewa muhanga kwa ajili ya harakati za kikosi cha Quds cha IRGC.

3968811

 

captcha