IQNA

Sheikh Zakzaky na mkewe hatimaye waelekea India kupata matibabu

10:54 - August 13, 2019
Habari ID: 3472081
TEHRAN (IQNA) - Hatimaye Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria leo ameondoka Abuja na kuanza safari ya kuelekea nchini India kwa ajili ya matibabu.

Ripoti kutoka Abuja zinasema kuwa, Sheikh Zakzaky akiwa ameandamana na mkewe, jana Jumatatu waliondoka mjini humo na kuanza safari ya kuelekea nchini India kwa ajili ya matibabu.

Jumatatu iliyopita ya tarehe 6 Agosti, Mahakama Kuu ya jimbo la Kaduna ilitoa hukumu ya kuachiwa huru mwanaharakati huyo ili asafiri kuelekea nje ya nchi kwa ajili ya matibabu. Hivi karibuni serikali ya Nigeria ilitoa masharti mapya ya kwa ajili ya kutoa ruhusa hiyo.

Kamishna wa Usalama na Masuala ya Ndani wa Jimbo la Kaduna, Samuel Aruwan alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, miongoni mwa masharti yanayopaswa kuzingatiwa kwa ajili ya kuruhusu safari hiyo ni Wizara ya Mambo ya Nje kuainisha wakati wa kukutana na Sheikh Zakzaky hospitalini huko India na vilevile kuarifisha wadhamini wawili mashuhuri. 

Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe walitiwa nguvuni na askari wa jeshi la Nigeria Desemba 13, 2015 katika shambulio na uvamizi uliofanywa na askari hao dhidi ya Huseinia ya Baqiyatullah katika mji wa Zaria.

Siku hiyo askari wa jeshi la Nigeria waliwafyatulia risasi watu waliokuwa wamejumuika kwenye kituo hicho cha kidini na mbele ya nyumba ya msomi huyo na kuwaua shahidi mamia miongoni mwao wakiwemo watoto wake watatu wa  kiume.

3834406

captcha