IQNA

Marekani yamkamata mtangazaji Mwislamu wa Press TV, avuliwa hijabu, alishwa nguruwe

11:31 - January 17, 2019
Habari ID: 3471809
TEHRAN (IQNA)-Maafisa wa usalama wa Marekani wamemkamata mtangazaji mashuhuri wa Televisheni ya Press TV Bi. Marzieh Hashemi ambapo wamemvua hijabu yake na kumlisha nyama ya nguruwe.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani kitendo cha serikali ya Marekani cha kumuweka kizuizi mtangazaji huo maarufu wa televisheni ya Press TV na ametaka kuachiliwa huru mara moja mtangazaji huyo tena bila ya masharti yoyote. Press TV ni kanali inayosimamiwa na Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Utangazaji la Iran, IRIB, na ina makao yake mjini Tehran.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, hatua ya maafisa wa serikali ya Maarekani ya kumuweka kizuizini mwanamke huyo Mwislamu Mmarekani ni uvunjaji wa wazi kabisa wa haki za binadamu na inazidi kuthibitisha kuwa serikali ya Marekana haiheshimu msingi wowote wa uhuru wa kujieleza na haiwezi kabisa kuvumilia kukosolewa.

Kwa mujibu wa kanali ya habari ya Press TV, Bi Hashemi, Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika, aliyekuwa akiitwa Melanie Franklin na baadaye akasilimu baada ya kudhihirikiwa na nuru ya uongofu ya Uislamu, alitiwa nguvuni Jumapili St. Louis, Missouri na kupelekwa mjini Washington DC ambako amewekwa kizuizini tokea Jumapili bila ya kuelezwa amekamatwa kwa kosa gani.

Wakati huo huo, Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, IRIB, kimetoa taarifa na kutaka kuachiliwa huru mara moja na bila ya masharti Bi.Hashemi.

Taarifa ya siku ya Jumatano, Kitengo cha Kimataifa cha IRIB, imelalamikia vikali hatua ya polisi ya Marekani kumkamata Bi. Hashemi siku chache zilizopita bila kumfahamisha sababu ya kukamatwa mbali na kumuweka chini ya mashinikizo makali ya kiroho na kimwili.

Taarifa hiyo imesema: "Marzieh Hashemi, kama mwandishi habari wa kimataifa na kama Mwanamke Mwislamu mwenye asili ya Afrika, alienda Marekani kukutana na familia yake na kumtembelea kaka yake anayeugua saratani lakini amekamatwa bila sababu yoyote."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Punde baada ya Marzieh Hashemi kukamatwa, wakuu wa gereza walimtia pingu na kumfunga kwa nyororo na pamoja na kuwa walifahamu kwamba yeye ni Mwislamu, walimvua Hijabu na kumnyima chakula halali."

Taarifa ya Kitengo cha Kimataifa cha IRIB imesisitiza kuwa: "Kwa kuzingatia udahifu wa kimwili alio nao Bi. Hashemi na hitajio lake la chakula maalumu, anapaswa kuruhusiwa kumuona daktari haraka iwezekanavyo."

Mkuu wa Kitengo cha Kimataifa cha IRIB Dkt. Peyman Jebeli amesema,  "Hakuna sababu yoyote ya  kukamatwa Marzieh Hashemi nchini Marekani. Kosa lake kubwa ni kuwa yeye ni mwanamke Mwislamu Mmarekani na tokea mwaka 2003 amekuwa akifanya kazi na Press TV."

Ameashiria namna wakuu wa Marekani wanavyomdhalilisha Marzieh Hashemi akiwa korokoroni ikiwa ni pamoja na kumvua hijabu yake na kumlazimisha ale nyama ya nguruwe ambayo ni haramu kwa Waislamu na kusema, kitendo hicho ni ukiukwaji wa wazi wa matukufu na thamani za Kiislamu. Aidha amesema mbali na kumnyima chakula cha halali, wakuu wa Marekani pia wamekataa kumpa Bi. Hashemi nguo zinazofaa katika msimu huu wa baridi kali nchini humo.

3467710

captcha