IQNA

Chuo Kikuu Ujerumani chatenga bajeti ya Euro Milioni 2.7 za mradi wa Qur'ani

9:24 - December 27, 2018
Habari ID: 3471788
TEHRAN (IQNA)- Akademia ya Uislamu katika Sayansi na Jamii ya Chuo Kikuu cha Goethe nchini Ujerumani imetenga bajeti ya Euro milioni 2.7 katika mradi wa kufanya utafiti kuhusu Qur'ani Tukufu.

Taarifa inasema bajeti hiyo imetengewa makundi mawili ya utafiti kwa lengo la kubuni mfumo wa kidijitali wa kuhifadhi maelezo na uchambuzi wa Qurani Tukufu na 'Sheria za Qurani'.

Chuo Kikuu hicho kimesema mradi huo wa kijamii umeainishwa na kuidhinishwa na Wizara ya Elimu na Utafiti ya Ujerumani, kwa kushirikiana na Wakfu wa Mercator.

Mbali na Chuo Kikuu cha Goethe, Vyuo Vikuu vyengine vya Ujerumani vinavyoshirikishwa kwenye mradi huo ni pamoja na Frankfurt am Main, Gisen na Hamburg.

Tafiti nyingi zimefanywa kuhusu Qurani Tukufu na aghalabu zimehifadhiwa kwa njia ya maandishi, lakini mradi huu wa Akademia ya Uislamu katika Sayansi na Jamii ya Chuo Kikuu cha Goethe nchini Ujerumani unapania kuhifadhi tafiti hizo kupitia mfumo wa dijitali.

Kwa utaratibu huu, taarifa zozote mpya kuhusu historia na chimbuko la Uislamu na pia maelezo kuhusu Qurani Tukufu zitawekwa mtandaoni kwa ajili ya kuwanufaisha watu wote.

Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Horst Seehofer alisema Waislamu ni sehemu ya jamii ya Ujerumani. Aliyasema hayo mwezi Novemba mjini Berlin wakati akizungumza katika Kongamano la Nne la Uislamu nchini Ujerumani (DIK).

Ujerumani ni nchi yenye watu milioni 81 na ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu Ulaya maghairbi baaada ya Ufaransa. Waislamu Ujerumani wanakadiriwa kuwa milioni 4.7 ambapo milioni 3 miongoni mwao wana asili ya Uturuki.

3775320

captcha