IQNA

Dunia yalaani sheria mpya ya kibaguzi ya utawala haramu wa Israel

19:08 - July 20, 2018
Habari ID: 3471601
TEHRAN (IQNA)- Utawala wa Kizayuni wa Israel umelaaniwa vikali kwa kupitisha sheria mpya ya kibaguzi ambayo inatambua Mayahudi kama bora kuliko Waarabu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Sheria inayojulikana kama 'Nchi ya Taifa la Mayahudi' imepasishwa Alhamisi katika 'Knesset" bunge la utawala haramu wa Israel.

Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu kupitishwa kwa sheria hiyo ya ubaguzi wa rangi na kusema kuwa inapingana moja kwa moja na maazimio ya Umoja wa Mataifa. Licha ya kuwepo malalamiko mengi ya Mayahudi lakini bunge la utawala haramu lilipitisha mswada wa sheria hiyo. Kwa mujibu wa sheria hiyo, ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo (Israel) zinachukuliwa kuwa ni za Mayahudi pekee na kwamba Wapalestina wanaoishi katika ardhi hizo watanyimwa haki zote za kiraia na za kibinadamu. Vilevile lugha ya Kiibrania ndiyo itakayokuwa lugha rasmi katika ardhi hizo. Sheria hiyo licha ya kuutambua mji mtakatifu wa Quds kuwa eti ni mji mkuu wa utawala huo ghasibu, inatambua ujenzi na kupanuliwa kwa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi kuwa thamani ya kitaifa na kutaka hatua za haraka zichukuliwe kwa lengo la kuimarisha vitongoji vilivyopo sasa na kujengwa vingine vipya.

Wazayuni wapuuza malalamiko

Sheria hiyo ya kibaguzi imepitishwa katika hali ambayo kabla ya kupitishwa kwake maelfu ya wakazi wa Tel Aviv katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu walifanya maandamano makubwa ya kuupinga na vilevile Mayahudi wa Marekani wakaupinga vikali na kutaka usipitishwe na Knesset kwa hoja kuwa ni wa ubaguzi wa rangi. Licha ya upinzani huo mkali lakini viongozi wa Wazayuni wameupitisha kwa lengo la kufikia malengo yao ya kibaguzi na kichokozi katika ardhi za Wapalestina wanazozikalia kwa mabavu. Kupitia sheria hiyo, watawala wa Kizayuni wana lengo la kudumisha mpango wa kutekeleza mauaji ya kizazi, kuwalazimisha wapalestina kuhama ardhi zao, kueneza mradi wa kubadilisha muundo wa kijamii wa Palestina na kuufanya uwe ni wa Kiyahudi, kudumisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kusimamisha mpango wowote wa kuwawezesha wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika radhi zao za jadi.

Turathi ya kikoloni

Kwa hakika sheria hiyo ni kudumishwa turathi ya kikoloni na ya ubaguzi wa rangi ambayo imejengeka katika msingi wa mauaji ya kizazi, kufutwa taifa la Palestina na kupuuzwa haki zao zote za msingi. Kuhusiana na suala hilo Swaib Arikaat, Katibu Mkuu wa Kamati ya Utendaji ya Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina PLO amesema kuwa sheria hiyo ni udumishwaji wa turathi ya kikoloni ambayo imesimama kwenye msingi wa mauaji ya kizazi na kupuuza kwa makusudi, haki za wakazi asilia wa ardhi hizo za kihistoria.

Kwa upande wake Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ambebainisha wasiwasi wake kuhusu sheria hiyo ya kibaguzi ya Israel.

Haki ni ya Wapalestina

Katika Ukanda wa Ghaza, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, Fawzi Barhoum amesema sheria hiyo imetambua rasmi 'ubaguzi wa Israel' na ni shambulizi hatari kwa haki ya kihistoria ya Wapalestina kumiliki ardhi yao ya jadi. Aidha amesema sheria hizo za Israel hazina msingi kwani haziwezi kubadilisha hali ya mambo na Wapalestina watabakia kuwa wamiliki halisi wa ardhi zao.

Hata kama hatua hizo za kinyama na za kibaguzi za utawala wa Kizayuni zimekuwa zikitekelezwa kwa miaka mingi dhidi ya Wapalestina, lakini zimepata kasi na msukumo mpya kutokana na uungaji mkono mkubwa inauopata utawala huo kutoka kwa serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani. Hivi majuzi Trump aliuhamishia ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Quds (Jerusalem) kutoka Tel Aviv na vilvile kuiondoa nchi yake Katika Baraza la Haki za Binadamu katika kuinga mkono Israel na hivyo kuthibitisha kivitendo kuwa nchi hiyo ni mshirika na muungaji mkono mkuu wa utawala huo wa kibaguzi unaoendelea kutenda jinai za kutisha dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina.

Kupitishwa kwa sheria hiyo inayotajwa kuwa 'Taifa la Mayahudi', bila shaka ni mfano mwingine wa wazi wa ubaguzi wa rangi na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Wapalestina na vilevile kukanyagwa misingi ya sheria za kimataifa.

3466310

captcha