IQNA

Watu 132 wauawa katika hujuma dhidi ya mikutano ya kampeni za uchaguzi Pakistan

22:12 - July 13, 2018
Habari ID: 3471592
TEHRAN (IQNA)- Watu wasiopungua 132 wameuawa hii leo katika milipuko ya mabomu yaliyolenga mikutano miwili ya kampeni za uchaguzi nchini Pakistan.

Katika mlipuko mbaya zaidi Ijumaa hii, magaidi wameulenga msafara wa kampeni za uchaguzi mkoani Baluchistan kusini magharibi mwa Pakistan.

Vyombo vya habari vya Pakistan vimeripoti kuwa watu 128 wameuawa na wengine 120 wamejeruhiwa katika mlipuko huo uliotokea katika mji wa Mastung karibu na makao makuu ya mkoa ya Quetta.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa mkoa wa Baluchistan, Agha Umar Bungalzai amethibitisha kuwa mlipuko huo umemuua pia Siraj Raisan, ndugu wa Mr Aslam aliyekuwa Waziri wa zamani mkoani huo ambaye alikuwa akigombea kiti cha uwakilishi katika bunge la mkoa kupitia chama cha Awami Baluchistan. Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh limetangaza kuhusika na jinai hiyo.

Katika upande mwingine, mapema leo watu wengine 4 waliuawa na wengine 39 kujeruhiwa baada bomu lililokuwa limefichwa ndani ya pikipiki kuripuka karibu na  mkutano wa kampeni wa mwanasiasa Akram Khan Durran katika mji wa Bannu karibu na mpaka wa Afghanistan.

Tarehe 10 mwezi huu watu wasiopungua 22 waliuawa katika shambulio la bomu katika mkutano wa mwanasiasa anayelipinga kundi la kigaidi Taliban kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Mwezi Mei mwaka huu Rais Mamnoon wa Hussain wa Pakistan aliidhinisha tarehe 25 mwezi huu kuwa ni siku ya kufanyika uchaguzi mkuu ambao unatazamiwa kuiingiza madarakani serikali mpya.

Wanaharakati wa kisiasa nchini Pakistan wameitaka serikali iimarishe usalamda na idhamini usalama wa wanasiasa na wapiga kura.

Tume ya Uchaguzi ya Pakistan nayo pia imeitaka Idara ya Kitaifa ya Kupambana na Ugaidi (Nacta) itangaza hatua ilizochukua kuwalinda wanasiasa na wagombea viti katika uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika Julai 25.

3729634

captcha