IQNA

Miji mitatu ya Iran kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani

12:17 - April 17, 2018
Habari ID: 3471468
TEHRAN (IQNA)-Mkuu wa Shirika la Wakfu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema miji mitatu nchini itakuwa mwenyeji wa mashindano kadhaa ya kimataifa ya Qur'ani.

Akizungumza na waandishi habari mjini Tehran, Mkuu wa Shirika la Wakfu la Iran Hujjatul Islam Ali Mohammadi amesema mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya Iran mwaka huu yatafanyika katika miji mitatu ya Tehran, Qum na Mashhad.

Ameongeza kuwa mashindano hayo yatakuwa na wageni 370 kutoka nchi mbali mbali duniani wakiwemo watakaoshindano, majaji na wageni wengine waalikwa.

Kwa mujibu wa Sheikh Mohammadi,  mwaka huu mashindano ya Qur'ani yatakuwa na washiriki kutoka nchi 84 na yanatazamiwa kuanza rasmi Aprili 19 hapa mjini Tehran.

Amesema mashindano ya mwaka huu yatajumuisha Mashindano ya 35 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran (ya kawaida maalumu kwa ajili ya wanaume) na pia kutakuwa na mashindano mengine ya Qur'ani ya wanawake, ya wenye ulemavu wa macho, ya wanafunzi wa vyuo vikuu na ya wanachuo wa vyuo vya kidini.

Mkuu wa Shirika la Wakfu la Jamhuri ya Kiislamu, ambalo huandaa mashindano hayo, amesema kauli mbiu ya mashindano ya mwaka huu ni "Kitabu Kimoja, Umoja Moja' na kuongeza kuwa nara hii inatokana na msingi wa Qur'ani kuhusu sisitizo la umoja wa Kiislamu.

Amesema pembizoni mwa mashindano hayo, kutakuwa na kongamano la kimataifa la Qur'ani Tukufu na mwaka huu kongamano hilo litajikita katika maudhui ya 'madola ya kiistikbari kwa mtazamo wa mafundisho ya Qur'ani.'

3706062

captcha